
Siku ya Mtoto wa Afrika: Tusimwache Mtoto Nyuma katika Kupinga Ukatili dhidi ya Watoto
Juni 16 kila mwaka bara la Afrika huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tangu kuidhinishwa kwa siku hiyo na Umoja wa Afrika mwaka 1991. Umoja wa Afrika ulianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika kama sehemu ya kuwakumbuka na kutambua mchango wa watoto waliopoteza maisha katika mauaji yaliyotokea huko Soweto, Afrika ya Kusini wakati watoto walipoandamana kudai haki zao za msingi.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu huungana na jamii ya kiafrika kuadhimisha siku hiyo maalumu katika kutambua mchango wa watoto katika jamii, sambamba na kuamsha uelewa wa serikali na jamii kwa ujumla katika kutetea haki za watoto ikiwemo haki ya elimu na haki nyinginezo. Katika maadhimisho ya mwaka huu 2018 dhima kuu kwa Afrika ni "Usimwache Mtoto Nyuma katika Maendeleo ya bara la Afrika" na dhima ya Tanzania ni "Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tusimwache Mtoto Nyuma". Kituo kinaadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli mbalimbali ambazo zina maslahi ya moja kwa moja kwa watoto.
LHRC itakuwa moja kwa moja katika mikoa mitatu tofauti ambayo ni Shinyanga, Mara na Dar es Salaam. Mkoani Shinyanga Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatarajia kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wanawake kwa lengo na kutatua kero mbalimbali za kisheria ikiwemo zinazohusiana moja kwa moja na migogoro ya kifamilia, masuala ya UKIMWI, malezi ya watoto, ukatili wa kijinsia, ndoa, mirathi naajira. Katika kutekeleza hili timu ya LHRC itakuwa katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga katika viwanja vya Fire kuanzia Jumatatu Juni 11 hadi Jumatano Juni 13, 2018 kuanzia Ijumaa Juni 14 Jumamosi Juni 16, 2018 katika viwanja vya Kambarage. Muda wa huduma ni kuanzia saa 3.00 Asubuhi hadi saa 10.00 Jioni.
Mkoani Mara, timu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu itaungana na Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Shirika la Amref watakuwa Kata ya Majimoto wilayani Serengeti kufanya uhamasishaji kupinga ukatili kwa watoto hususani mila ya ukeketaji ambayo inaathiri kwa namna mbalimbali maslahi ya watoto wilayani humo. Mkutano wa hadhara utakaohudhuriwa na viongozi wa wilaya na wananchi katika kuhamasisha jamii kuachana na mila potofu. Jijini Dar es Salaam, LHRC itaadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuwakutanisha watoto kutoka shule 5 za msingi kwa lengo la kujadili mustakabali wao kama watoto. Kituo kimeandaa Bunge la wanafunzi kutoka shule ya Msingi Kijitonyama (Kinondoni), Shule ya Msingi Mji Mwema (Kigamboni), Shule ya Msingi Mkombozi (Ubungo) Shule ya Msingi Mkoa, Shule ya Msingi Temeke (Temeke) kama wawakilishi na itafanyika Jumanne Juni 19.
Sambamba na maadhimisho hayo Kituo kinaendelea kuwataka watanzania kuheshimu na kulinda haki za watoto kwa kuzingatia kwamba haki za watoto zimekuwa hatarini. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2017, matukio ya ukatili kwa watoto hususani vitendo vya ubakaji na ulawiti, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukatili wa kimwili vimezidi kuongezeka. Hata hivyo baadhi ya matamko ya viongozi wa serikali kwa mfano tamko la Rais Magufuli linalozuia watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za Serikali limeendelea kuathiri haki ya elimu hasa kwa watoto wa kike.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaukumbusha umma wa watanzania kuachana na mila kandamizi zinazodidimiza maslahi ya mtoto na badala yake kulinda haki za watoto hasa kwa kuzingatia watoto ni moja ya makundi yanahitaji ulinzi mbadala. Jamii pia inahusiwa kuwashirikisha watoto katika kufanya maamuzi yanayogusa maslahi yao ili kufanya maamuzi sahihi kwa kundi hilo.
Tusimwache Mtoto Nyuma katika Kupinga Ukatili dhidi ya Watoto.