Wito kwa Serikali kufanya Jitihada za Haraka Kupunguza Ukosefu wa Maji Nchini

Wito kwa Serikali kufanya Jitihada za Haraka Kupunguza Ukosefu wa Maji Nchini

Posted 1 year ago by admin

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefuatilia kwa ukaribu changamoto zinazoendelea nchini kwa ukosefu wa maji. LHRC inatoa rai kwa serikali kufanya jitihada za haraka kutatua shida ya maji iliyopo sasa. Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inaweka haki ya uhai ambapo, bila maji safi na salama haki hii haitoweza kufikiwa. Hivyo, serikali inawajibu wa kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama.

Mgao wa maji umeendelea kuleta athari za kiuchumi kwa wafanyabiashara, kijamii kwa wananchi kwa ujumla, kiusalama na kiafya hasa kuchochea visababishi vya magonjwa ya mlipuko katika jamii hasa kwa kundi la watoto na wanawake.

Ni ukweli kwamba, ukosefu wa maji unaendelea kutesa watoto na wanawake kwa kutembea umbali mrefu kutafuta maji hata kipindi cha usiku. Hali hii inachochea vitendo ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kuongeza migogoro ya kifamilia.

LHRC inatoa wito kwa Serikali kuchukua mikakati ifuatayo;

Mikakati ya muda mfupi

  1. kuchimba visima virefu ili kupunguza athari inayoendelea kukabili jamii katika kipindi hiki.
  2. Kufuatilia vyanzo vya maji na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha havihujumiwi na kufanya kazi jinsi inavyopaswa.
  3. Kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi na kuhakikisha wananchi wanapata maji.
  4. Kuchukua hatua stahiki kwa watu wote waliyoshindwa kutimiza wajibu wao katika suala hili.

Mikakati ya muda mrefu

  1. Kuangalia vyanzo mbadala na kuona jinsi gani vinaweza kutumika kupata maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji.
  2. Kuweka sera na sheria mbalimbali zitakazolinda na kudhibiti uharibifu wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji.
  3. Serikali kujifunza na kutafuta wataalam ambao watasaidia kufanya utafiti wa namna bora ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini.
  4. Kutenga bajeti ya kutosha ili kuweza kuvuna maji ya kutosha ili yatumike nyakati za upungufu wa maji.

 

Imetolewa leo tarehe 18 Novemba 2021 na;

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji