Wanachama wa LHRC Wataka Kuongezeka kwa Jitihada za Utetezi wa Haki nchini

Wanachama wa LHRC Wataka Kuongezeka kwa Jitihada za Utetezi wa Haki nchini

Posted 5 years ago

Mei 25, 2019, Kituo ch Sheria na Haki za Binadamu kilifanya Mkutano Mkuu wa 18 wa Mwaka wa Wanachama wa Kituo hicho jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo uliotanguliwa na warsha iliyokuwa na dhima “Ulinzi na Usalama kwa Watetezi wa Haki za Binadamu” wanachama walieleza furaha yao juu ya utendaji kazi wa shirika huku wakitoa maoni namna ya kuboresha kazi za shirika kwa lengo la kudumisha ulinzi wa haki za binadamu nchini Tanzania. 

Akiendesha mafunzo kwa washiriki wa warsha ya mkutano wa mwaka wa wanachama, Mshauri wa Masuala ya Tehama, Bi. Fatumata Betere aliwasihi watetezi wa haki za binadamu kuzingatia taratibu za ulinzi na usalama katika utendaji wa kazi za utetezi wa haki za binadamu kwani kazi za utetezi zinahusisha hatari mbalimbali za kiusalama. 

Katika warsha hiyo pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu aliwasilisha taaarifa ya kazi zilizofanyika mwaka 2018 ikibainisha mafanikio kadha wa kadha ikiwemo LHRC kuendelea kuwa kimbilio la wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria, kuendelea kufanya utetezi kwa ajili ya maboresho ya sera na sheria mbalimbali, kuendelea kutoa elimu ya sheria na haki za binadamu kwa watanzania sambamba na kuwezesha uendelevu wa shirika.

Wakitoa maoni na mapendekezo kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wanachama wamekipongeza Kituo kwa kutokutetereka mbali na kubadilisha uongozi mwaka 2018. Mkurugenzi Mtendaji mstaafu Dkt. Helen Kijo-Bisimba ambaye ni moja ya wanachama wenye mapenzi ya dhati kwa LHRC alieleza furaha yake ya kuhudhuria mkutano wa kwanza wa mwaka wa wanachama akiwa si kiongozi tena wa LHRC na kuendelea kuona uendelevu wa shirika chini ya mrithi wake Bi. Anna Henga.

“Ninawashukuru sana wanachama na LHRC kwa ujumla kwa upendo wenu mkuu kwani mliniaga kwa heshima kubwa ambayo sikutarajia. Namshukuru sana Mungu kwa kuniweka kushuhudia Kituo chetu kikiendelea mbele chini ya uongozi mpya wa Bi. Anna Henga, nina furaha sana siku ya leo” – alisema Dkt. Helen kwa hisia.

Katika kupokea shukrani na mapendekezo ya wanachama, Mkurugeniz Mtendaji aliwashukuru wanachama kwa kuendelea kulijali na kulipenda shirika na kuahidi kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuendeleza kazi za utetezi wa haki za binadamu nchini. 

Mkutano wa 18 wa Wanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa mwaka 2019 ulihudhuriwa na wanachama kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mkutano Mkuu wa wanachama pia ulipitisha majina wadau wengine waliiomba kuwa wanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.