Wadau waitaka Serikali Kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya

Wadau waitaka Serikali Kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya

Posted 5 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeandaa mdahalo kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo, serikali, asasi za kiraia, taasisi za kidini, taasisi za kielimu, vyama vya siasa na vyombo vya habari kujadili mchango wa katiba bora katika kudumisha Amani nyakati za chaguzi.

Katika mkutano huo uliofanyika Machi 2, 2018 jijini Dar es Salaam, wadau kwa pamoja wameitaka serikali kuzingatia kilio cha wananchi kutaka katiba mpya na kuona haja ya kukamilisha mchakato kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Akichangia katika mdahalo huo mwakilishi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Prof. Mwesiga Baregu ameeleza hofu yake kwa Tanzania kwenda kwenye uchaguzi mkuu mwingine bila kuwa na katiba inayotokana na wananchi. Prof. Baregu amesema nchi ina ombwe la katiba na hii inatokana na ukweli kwamba wananchi walishaaminishwa kuwa katiba iliyopo haifai na wakawa tayari kwa katiba mpya. Katika kutoa mapendekezo, Prof. Baregu ameishauri Serikali kuangalia namna tatu ambazo serikali inaweza kutumia ili kukamilisha mchakato kabla ya uchaguzi mkuu ujao; moja ikiwa ni kuchagua kwenda kwenye kura ya maoni, pili kuunda Bunge Maalumu kutengeneza katiba pendekezwa mpya au tatu kuiga mfano wa Kenya wa kuunda jopo maalumu la wataalamu ambao wataandaa katiba pendekezwa.

Kwa upande wa taasisi za dini, Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padri Daniel Dule amepongeza hatua iliyochukuliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu akisisitiza kwamba majadiliano ni msingi wa kudumisha umoja, ushirikiano , Amani na utu ambao ndio msingi wa haki za binadamu. Padri Dule ameitaka serikali kusikiliza sauti ya wengi “kama wananchi wengi wanataka (katiba mpya) basi iendelezwe ili kutii kiu ya wananchi hao”.

Akizungumzia muundo wa chaguzi nchini, Wakili John Seka amesisitiza umuhimu wa nchi kupitia na kufanyia marekebisho mfumo wa kusimamia chaguzi kwa kubadilisha sheria zilizopo sambamba na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.

Kwa ujumla, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga amesisitiza kuwa Katiba Mpya ni jawabu la changamoto mbalimbali nchini hasa zilizoibuliwa katika chaguzi kuu za 2005 na 2015.