
Uvunjifu wa Katiba na Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba Kuwa na Mgombea Binafsi
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimefuatilia kwa karibu msuguano unaondelea kati ya Spika wa Bunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juu wa wabunge waliokosa sifa kwa kuvuliwa uanachama au kuhama chama kwa ridhaa yao. Mgogoro huu sio tu unasigina demokrasia lakini kwa upande mwingine unavunja katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Misingi ya demokrasia inatawaliwa na dhana ya ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi juu ya mambo ya msingi yanayowahusu katika taifa lao, kwa Tanzania kama ilivyokatika nchi nyingi duniani uwakilishi wa wananchi katika ngazi za maamuzi unafanywa kwa uwakilishi wa watu wachache waliyochaguliwa na wananchi hao yaani indirect democracy.
Kwa mujibu wa ibara 21, 39, 47 and 67 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa haki ya mtu kuwawakilisha wananchi katika ngazi za maamuzi kwa sharti la kupitia au kudhaminiwa na chama cha siasa. Hivyo, kwa Katiba ya sasa suala la udhamini wa chama cha siasa katika ngazi za maamuzi ni takwa la msingi. Kwa mujibu wa ibara ya 71(1)(e), Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge endapo mbunge huyo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge.
Hatua ya Spika wa Bunge Mh. Job Ndungai kuendelea kutambua wabunge waliovuliwa uanachama na CHADEMA kwa tafsiri ya moja kwa moja ni sawa na kuvunja Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyoainishwa.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatambua umuhimu wa uwakilishi wa wananchi katika ngazi za maamuzi pasipo changamoto za kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Ni wazi kwamba, changamoto za kikatiba zilizojitokeza katika hatua ya CHADEMA kuwavua uanachama wabunge wake na Spika wa Bunge kuendelea kuwatambua wabunge hao ni uvunjifu wa Ibara ya 71(1)(e). Katika suala hili, Kituo kinaona haja ya kufanyika mabadiliko ya kikatiba kutambua mgombea binafsi ili kuepuka hatari ya kuvunja Katiba ikizingatiwa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria. Ikumbukwe kwamba, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilitoa uamuzi wa kuhusu haki ya mgombea binafsi kutambuliwa katika ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Katika upande mwingine, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018 hadi 2020 kumeshuhudiwa matumizi makubwa ya rasilimali za wananchi kwa kufanya chaguzi za marudio katika majimbo na kata mbalimbali kutokana na wabunge na madiwani kutoka chama kimoja kwenda chama kingine cha siasa. Ni muhimu kurekebisha katiba ya sasa pamoja na sheria ili kuruhusu haki ya wananchi kuwakilishwa pasipo kufanyika marudio ya uchaguzi ikiwa mbunge au diwani atahama chama chake.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito wa kurudisha mchakato wa katiba ili kusawazisha changamoto za kikatiba zilizopo sasa.