UJUMBE KWA MWENDESHA MASHTAKA (DPP) KUHUSU COVID-19 NA HAKI ZA WATU WALIOPO KIZUIZINI KWA KUKOSA DHAMANA

UJUMBE KWA MWENDESHA MASHTAKA (DPP) KUHUSU COVID-19 NA HAKI ZA WATU WALIOPO KIZUIZINI KWA KUKOSA DHAMANA

Posted 4 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea kuungana na mamlaka zote za nchi katika kuchukua hatua ya udhibiti wa mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19) unasababisha madhara ya kiafya ikiwemo kusababisha vifo vya watu. Hili ni janga la kimataifa na kila mtu, taasisi na mamlaka nyingine kila moja kwa nafasi yake lazima isimame kupambana kuzuia kuenea kwa hivi virusi.

Ni wazi kwamba, ibara ya 59B inampa mamlaka mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) kusimamia mashtaka yote ya jinai nchini. Mamlaka haya yamebainishwa zaidi katika sheria mbalimbali za makosa ya jinai ikiwemo sheria ya Criminal Procedure Act, 1985 na National Prosecutions Service Act, 2008. Hii ni pamoja na uwezo wa kutoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhusu upelelezi, kuendelea kumshikilia mtuhumia hadi hapo ofisi yake itakapoweza kukamilisha ushahidi kwa ajili ya kushtaki.

Idadi kubwa ya watu waliyopo magerezani ni mahabusu ambao wengi wao wamekumbwa na suala la mamlaka ya DPP kukamilisha ushahidi kwa ajili ya mashauri kusikilizwa kwa mshauri yasiyokuwa na dhamana. Pia wapo ambao dhamana zao zimefungwa na DPP kwa mujibu wa sharia wakati mahsuri yao yanadhaminika. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2019 iliyozinduliwa tarehe 29/04/2020 jijini Dar es salaam imebainishwa zaidi ya asilimia 50% ya watu waliyo magerezani ni mahabusu.

Kufuatia mlipuko wa janga hili la COVID-19, watu waliyopo kizuizini ni kati ya watu walio kwenye hatari kubwa sana ya kuathirika na virusi hivi. Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa njia kuu ya kuepuka usambazaji wa virusi hivi pamoja na nyingine nyingi ni kuepuka kukaa maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Ni wazi kwamba, magereza yetu yanakabiliwa na tatizo la msongamano mkubwa wa watu na hivyo, usambazaji wa virusi hivi unaweza kutokea kwa ukubwa sana na kuathiri watu wengi zaidi kwa muda mfupi kama ikitoke.

Ikumbukwe kwamba, haki za watu hawa walio kizuizini zinapaswa kulindwa ili kuwaepusha na kuwalinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu wa COVID-19.

Haki ya msingi kabisa ya kuangaliwa ni haki ya kuishi kama ilivyoainishwa chini ya Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Haki hii imebeba haki nyingi ndani yake lakini katika muktadha huu wa mlipuko wa virusi vya corona, watu waliopo kizuizini wanapaswa kuhakikishiwa upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo hatua muhimu za usaidizi wa kiafya, kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za usafi zikiwemo sabuni, maji tiririka pamoja na vitakasa mikono. Pia, kutoa elimu kwao juu ya njia za kujikinga na kuzuia maambukizi ya virusi hivi.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali ina jukumu la kuchukua hatua ili kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa maambukizo wa ugonjwa wa COVID-19 kutokana na baadhi ya watuhumiwa kuendelea kuwa vizuizini bila dhamana wala kukamilika kwa upepelezi wa kesi zao.

Jambo la muhimu kuliangalia ili kuzuia hali zinazotishia afya ya watu waliopo kizuizini hasa gonjwa hili la COVID-19 ni kupunguza msongamano wa watu gerezani. Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa sana kudhibiti mlipuko wa virusi hivi magerezani. Ni muhimu kwa ofisi ya mwendesha mashtaka kuchukua jitihada za makusudi kupunguza mrundikano wa watu mahabusu magerezani.

Kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kimeainisha baadhi ya makosa ambayo yanamnyima mshitakiwa haki yake ya kupatiwa dhamana.

Hii hupelekea watu hawa kuwekwa kizuizini huku wakisubiri kusikilizwa kwa mashauri yao ambapo ni kinyume na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inayosema “ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo,”

Katika kipindi hiki ambapo taifa linapambana na kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 katika maeneo mbalimbali, ni vema kwa ofisi ya DPP kuchukua hatua kwa kuhimiza upelelezi ukamilike haraka na kuacha tabia ya kufungua mashauri mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika.

Kwa kuongezea, watu walioko kizuizini pia wana haki ya kupewa taarifa kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 18(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, “kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.” Hivyo, katika utoaji wa taarifa mbalimbali juu ya ugonjwa wa Covid-19 ihakikishwe kuwa taarifa hizi muhimu pia zinawafikia watu wote mpaka wale waliopo kizuizini.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya merekebisho ya kifungu cha 148 kwa kupunguza makosa yasiyo na dhaman ili kupunguza mrundikano usiyo wa lazima katika magereza. Hii itaonesha nia ya dhati ya kupambana kwa kuenea kwa ugonjwa huu hatari.