Ujumbe kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha Bunge la Bajeti 2020/21

Ujumbe kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha Bunge la Bajeti 2020/21

Posted 2 years ago by admin

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa ujumbe huu katika kipindi ambacho Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea na mjadala wa bajeti wa wizara mbalimbali kuelekea katika majumuisho ya bajeti ya taifa kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Ikumbukwe kwamba, bajeti ya mwaka 2019/20 ilipitisha masuala mbalimbali na Kituo cha Sheria kama mdau kilifanya uchambuzi na kubaini masuala yenye maslahi ya haki za binadamu kama ifuatavyo;

  1. Ustawi wa Afya ya Mtoto

Bajeti ya 2019 ilipunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya kutengeneza taulo za watoto (Baby Diaper) zinazotengenezwa nchini kwa mwaka mmoja.

Ni imani yetu kwamba, bajeti ya mwaka 2020/2021 itaendelea kulinda kipengele hiki kwa kujali ustawi wa afya ya mtoto. Pia, Serikali iimarishe mifumo ya ulinzi wa mtoto kwa kuzingatia changamoto zinazowakumba watoto nchini. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2019 iliyotolewa na LHRC imeanisha jumla ya visa 14,419, vya matukio ya ukatili dhidi ya watoto.

  1. Kuhamasisha uchumi wa wakulima

Bajeti ya 2019/20 ilipunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya mbegu vianavyotumiwa na wazalishaji wa mbegu hapa nchini. LHRC inatoa wito kwa Serikali kuendeleza punguzo hili la ushuru wa forodha ili kuendelea kuhamasisha uchumi wa wakulima katika mwaka wa fedha 2020/21.

  1. Kuchochea uchumi wa wajisiriamali wadogo

Bajeti ya 2019/20 ilisamehe kodi kwenye mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne (4,000,000/=) kwa wenye vitambulisho vya wajasiriamali na kupunguza kiwango cha chini cha kodi kutoka shilingi laki moja na nusu (150,000/=) kwa mwaka hadi shili laki moja (100,000/=) kwa mwaka. LHRC inatoa wito kwa bajeti ijayo iweke nafuu zaidi ili kusaidia kundi kubwa la wajasiriamali wadogo nchini.

  1. Mazingira Rafiki ya ukusanyaji kodi

Kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilima 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye machine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Electronic Fiscal Device). Hatua hii ilikuwa hatua nzuri ya kupongezwa katika bajeti ya mwaka 2019/20, imesaidia kuhamisha mazingira mazuri ya ukusanyaji kodi.

  1. Punguzo la ushuru katika Sukari

Bajeti ya mwaka 2019/20 iliupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 100 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo la uzalishaji hapa nchini. LHRC inatoa wito kwa Serikali kuweka punguzo zaidi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21.

Kwa mwaka fedha 2020/21 LHRC inatoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzingatia masuala yafuatayo ili kulinda masuala ya haki za binadamu yanayotegemea hatua za kibajeti;

  1. Kuongeza bajeti ya kutoa elimu kwa ujumla juu ya uelewa wa sheria mbalimbali ikiwemo sheria za kodi, haki jinai, pamoja na sheria za madai ili kuwawezesha wananchi kufikia haki zao. Bado kumekuwepo kwa tatizo kubwa la wananchi kutojua sheria mbalimbali huku bajeti ikiwa na upungufu wa kutatua tatizo hilo.
  2. Kurudisha msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike katika bajeti ya 2018/19 na kuwabana wafanyabiashara watakaothibitika kunufaika na katazo hilo kinyume cha sheria.
  3. Kuongeza bajeti ya kuboresha maabara ya uchunguzi wa teknolojia ya jinai ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la mrundikano wa watuhumiwa wa makosa ya jinai magerazani kwa kusubiri upelelezi kukamilika.
  4. Pia, ushuru wa forodha kuendelea kuwa asilimia 25 badala ya asilimia 35 kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (semi-refined, refined/double refined oil) mfano mafuta ya alizeti, mawese, mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k ili kuwawezesha wananchi kupata mafuta ya kupikia kwa bei nafuu.
  5. Ushuru wa forodha kuendelea kuwa asilimia 25 badala ya asilimia 60 kwenye maji (mineral water) kama inavyopendekezwa sasa. Ili kuwezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa bei nafuu hususani katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya janga la COVID-19.
  6. Ushuru wa forodha kuendelea kuwa asilimia 25 kama iilivyo sasa katika bidhaa za mbogamboga (horticultural products) kwani mpendekezo yakuongeza ushuru huo hadi 35 itaathiri uchumi wa wakulima wa zao khilo pamoja na walalji wa bidhaa hizo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea kutoa rai kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuzingatia hali ya ugonjwa wa corona katika kupitisha bajeti za wizara na taasisi mbalimbali ili ziendane na mapambano ya ugonjwa huu.

Soma hapa uchambuzi wa awali

 

Imetoleawa Mei 22, 2020 na,

Kituo cha Sheria na Haki za Bindamu