UFAFANUZI WA KISHERIA KUHUSU MAMLAKA NA MIPAKA YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CONTORLLER AND AUDITOR GENERAL – CAG)

UFAFANUZI WA KISHERIA KUHUSU MAMLAKA NA MIPAKA YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CONTORLLER AND AUDITOR GENERAL – CAG)

Posted 4 years ago

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni ofisi ambayo imeundwa kikatiba kupitia Ibara ya 143 na 144 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.

Ibara hiyo kwa ufupi inaeleza ifuatavyo;

143.-(1) Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano. (2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na jukumu juu ya mambo yafuatayo: 

(a) kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe; 

(b) kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizo husika na matumizi ya fedha hizo na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo; na 

(c) angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge. 

(3) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na kila mtumishi wa Serikali aliyeruhusiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na haki ya kuchunguza vitabu, kumbukumbu, hati nyinginezo zote zinazohusika na hesabu za aina yoyote iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. 

(4) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho. Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu wa Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge. 

(5) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa pia na jukumu la kutekeleza kazi na shughuli nyingine, na atakuwa na madaraka mengine ya namna mbalimbali, kama itakavyoelezwa na sheria kuhusu hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au hesabu za vyombo vya Umma au hesabu za Mashirika. 

(6) Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.

Uwajibikaji/Kuwajibishwa kwake

    i.Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anawajibika kwa Rais sio kwa Bunge. Ibara ya 143 (4). Bungeni huwasilisha taarifa ambayo imetoka kwa Rais.

    ii.Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikai halazimiki kufuata Maagizo ya mtu yeyote Ibara ya 143 (6).

    iii.Mahakama ina uwezo wa kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii ama sivyo. Ibara ya 143 (6).

    iv.Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ataondoka kazini kwa yafuatayo;

    a.Kustaafu

    b.Kuugua

    c.Kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ibara ya 144

v. Kuondolewa kazini kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni mchakato mrefu unaoanza na Rais kuteua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili. Ibara ya 144 (3).

 

Imetolewa Januari 8, 2019, na;  

Bi. Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu