
Ufafanuzi wa Kisheria Kuhusu Makubaliano ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining)
Utangulizi
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Makosa ya Jinai kupitia Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria yaliyoletwa kupitia Muswada namba 4 wa mwaka 2019.
Marekebisho hayo yanaanzia Kifungu cha 3, na kuongeza kifungu 194A hadi 194H cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Mwaka 1985 (Sura ya 20). Ufafanuzi huu umejikita kuelezea dhana ya Plea Bargaining (Makubaliano ya Kukiri Kosa).
Sababu ya ufafanuzi huu ni kuelimisha umma kuhusu dhana hii mpya katika mfumo wa utoaji haki nchini Tanzania. Pia, kutoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha dhana ya Makubaliano ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining) inatumika kwa usahihi katika mchakato wa upatikanaji haki nchini kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.
Ufuatao ni ufafanuzi wa kisheria;
Makubaliano Maalumu ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining)
- Plea Bargaining ni makubaliano maalumu katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na Mshitakiwa ambapo Mshitakwa anakubali kukiri kosa moja au zadi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ilia pate nafuu ya kesi hiyo.
- Pia, Mshitakiwa anaweza kukubali kutoa ushirikiano kwa Mwendesha Mashtaka utakaowezesha kupatikana kwa taarifa zinazohusiana na kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
- Mwendesha Mashtaka baada ya kufanya mahojiano na mtu aliyetendewa kosa au Mpelelezi wa kesi hiyo anaweza kuingia katika makubaliano maalumu na mshtakiwa na Wakili wake kuhusu kosa hilo. Hivyo, nia ya kuanza kufanya makubaliano hayo itatakiwa kupelekwa Mahakamani kwa ajili ya taarifa. Hata hivyo, Mahakama haitohusika katika majadiliano hayo.
Matokeo ya Makubaliano Maalum ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining)
- Mwendesha Mashtaka anaweza kupunguza makosa makubwa katika hati ya mashtaka na kuacha makosa madogo au kufuta kabisa makosa mengine.
- Mshtakiwa anaweza kukiri kosa aliloshtakiwa kwa makubaliano ya kufutwa kwa makosa mengine.
- Mshtakiwa naweza kuamriwa kurudisha au kulipa fidia ya vitu vilivyopatikana kwa njia ya uhalifu, au vilivyotumika wakati wa kutenda uhalifu.
Utaratibu wa Kufanya Makubaliano ya Kukiri Kosa (Plea Bargaining)
- Makubaliano hayo yanatakiwa kuwa kwenye maandishi ikijumuisha taarifa zote za muhimu zitakazojadiliwa katika kikao hicho.
- Makubaliano yatatakiwa kusomwa na kuelezewa kwa Mshitakiwa katika lugha atakayoweza kuelewa.
- Makubaliano hayo yatatakiwa kukubaliwa na Mshitakiwa.
- Pia, makubaliano hayo yatatakiwa kutiwa saini na Mwendesha Mashtaka, Mshitakiwa na Wakili wake kama anaye.
Kumbuka: Endapo Mshitakiwa alifanyiwa utafasiri wa makubaliano hayo kwa kutumia mtaalamu wa tafsiri, mtaalamu huyo atatakiwa kuweka uthibitisho kisheria kwamba ni mbobevu katika lugha hiyo, na ametoa tafsiri sahihi katika makubaliano hayo kwa mujibu wa maudhui husika.
Wajibu wa Mahakama katika Makubaliano hayo
- Kujiridhisha kwamba makubaliano hayo yamefanyika bila shuruti.
- Kusajili Makubaliano hayo.
- Kutamka maamuzi ya makubaliano hayo au kutoa maamuzi endapo kuna ulazima wa kuyatoa au kukataa makubaliano hayo kwa sababu za msingi ingawa pande hizo zinaweza kufanya makubaliano mengine baada ya Mahakama kukataa makubaliano ya awali.
- Mwisho makubaliano hayo yatawekwa katika kumbukumbu za Mahakama endapo yatakubaliwa na Mahakama kwa kufuata taratibu maalumu.
Mambo ya Msingi ya Kufahamu Juu ya Makubaliano ya Kukiri Kosa
- Mshitakiwa hatokuwa na haki ya kusikilizwa na Mahakama yaani kupelekwa makamani na kutoa utetezi au Ushahidi juu ya kosa hilo.
- Mshitakiwa hatokuwa na haki ya kukata rufaa kuhusu uendeshaji wa kesi yake isipokuwa anaweza kukata rufaa kupinga utaratibu uliotumika wakati wa kutolewa kwa hukumu.
- Mwendesha Mashtaka anaweza kutumia maelezo yoyote dhidi ya Mshtakiwa katika kesi inayohusu kutoa taarifa ya uongo au uzushi.
Makosa yasiyoruhusiwa kufanyiwa Makubaliano Maalumu ya Kukiri Kosa
- Makosa ya udhalilishaji wa kingono yenye adhabu ya kufungwa Zaidi ya miaka mitano, au udhalilishaji dhidi ya mtu aliyechini ya umri wa miaka 18.
- Makosa ya uhaini
- Kumiliki au kusafirisha madawa ya kulevya yenye thamani inayozidi shilingi milioni 10
- Ugaidi
- Kumiliki nyara za Serikali zenye thamani inayozidi shiling milioni 10 bila idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
- Makosa mengine yoyote yatakayoelekezwa na Waziri husika.
Wito wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
- Ni vema kufahamu kwamba makubaliano ya kukiri kosa ni lazima yafanyike bila shuruti wala masharti yoyote yaliyo nje sheria.
- Mshtakiwa atatakiwa kuwa huru kadri atakavyoona inafaa kabla na wakati wa kufanya Makubaliano hayo.
- Nafuu hii ya kisheria itumike kwa washtakiwa wa makosa mbalimbali bila kujali kiwango cha pesa au aina ya kosa bila kuathiri sheria.
- Utaratibu wowote utakaofanyika bila kuzingatia sheria inayoweka fursa hii utakuwa nje ya sheria na utapaswa kupingwa kisheria.
Imetolewa September 25, 2019 na;
Anna Henga,
Mkurugenzi Mtendaji