Ufafanuzi kuhusu Haki za Mtuhumiwa wa Makosa ya Jinai

Ufafanuzi kuhusu Haki za Mtuhumiwa wa Makosa ya Jinai

Posted 5 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasikitishwa na vitendo wa uvunjwaji wa haki za watuhumiwa wa makosa ya jinai ambavyo vinazidi kushamiri siku hadi siku. Vitendo hivi vimeshamiri zaidi hususani kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma na Mwanza ambapo tumeshuhudia mara nyingi jeshi la polisi likiwakamata na kuwahoji watuhumiwa mbele ya vyombo vya habari sambamba na kuwafanyia vitendo vingine vya kutweza utu. Kituo, kinapinga vikali vitendo hivyo kwani ni kinyume na misingi ya haki za kikatiba na sheria za nchi kama ilivyofafanuliwa hapa;
 

Dhana ya kutokuwa na hatia
Kitendo cha kumtangaza mtuhumiwa kwamba amefanya kosa la jinai mbele ya vyombo vya habari ni kinyume na haki ya kutokuwa na hatia, msingi huu unawekwa chini ya Ibara ya 13(6) b ya Katiba ya Jamhuri ya Mundane wa Tanzania, 1977 kwamba;

‘ ‘Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo’’.
 

Kuingilia uhuru wa mahakama 
Katika upande mwingine, suala la Jeshi la Polisi kumhoji na kumtangaza mtuhumiwa mbele ya vyombo vya habari kwamba ametenda kosa la jinai ni kuingilia uhuru wa mahakama. Ibara ya 4(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambayo) imeanisha vizuri utekelezaji wa shughuli za mamlaka za nchi. Kimsingi Mahakama ndiyo chombo pekee cha utoaji haki katika Jamhuri ya Muugano wa Tanzania kama ilinavyoainishwa katika Ibara ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. Jeshi la Polisi ni chombo cha usimamizi wa sheria na ulinzi wa haki lakini si combo. chenye mamlaka ya hukumu.

Dhana ya kulinda utu wa binadamu
Kitendo cha kualika vyombo vya habari na kutoa habari za mtuhumiwa ikiwemo picha yake kwa umma ni kinyume na Ibara ya 13(6)d ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977;
 

‘‘Kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu’’.


Hata hivyo, kitendo cha kuwaanika wahalifu pia kinaweza kuharibu upelelezi na kuathiri uendeshaji wa kesi endapo shauri litafikishwa mahakamani.
Pia, kifungu cha 55 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura 20 ya Mwaka 1985 kinaainisha kwamba; mtu akiwa kizuizini, atatakiwa kutendewa kiubinadamu na kwa kufuata misingi ya utu wa binadamu, (2) mtu akiwa kizuizini, hatapaswa kutendewa ukatilii kinyume na ubinadamu au kudhalilishwa.

Haki ya faragha 
Kitendo cha kumhoji mtuhumiwa mbele ya vyombo vya habari ni kinyume na ibara ya 16 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977;

‘‘ Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi’’.

 

Misingi ya ubaguzi
Ibara ya 13 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, inatoa misingi ya mtu kutokubaguliwa kwa aina yoyote. Jeshi la polisi limekuwa likikiuka misingi ya Katiba, mfano kuhusisha ukabila na uhalifu katika kuwahoji wahalifu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza hiv karibuni alinukuliwa akimzungumzia mtuhumiwa kwa kutumia kabila lake “mchaga aliyejaribu kujiteka”.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vitendo hivyo na kulitaka Jeshi la Polisi kujiendesha kwa kuzingatia weledi, misingi ya Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Sheria za nchi.

Imetolewa Agosti 8, 2018, na 
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji