Uchambuzi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria na Mapendekezo ya Maboresho ya Mifumo ya Utoaji Haki

Uchambuzi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria na Mapendekezo ya Maboresho ya Mifumo ya Utoaji Haki

Posted 5 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeshiriki kwa ukaribu maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka 2020 yaliyoratibiwa na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Wiki ya Sheria huadhimishwa Februari 1 hadi Februari 6 kila mwaka kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu sheria na namna mifumo ya sheria inavyofanya kazi katika utoaji wa huduma za haki. Tunaipongeza Mahakama kwa maandalizi mazuri yaliyoshirikisha wadau wengi zaidi ikiwemo wananchi, Serikali, asasi za kiraia, Bunge na wadau wa maendeleo. 

Maadhimisho hayo yameibua hoja za msingi zilizojikita katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini hususani mfumo wa haki jinai. Katika kilele cha wiki ya sheria Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliweka msisitizo katika masuala ya msingi yanayolenga kuboresha mfumo wa utoaji haki kwa kugusia changamoto zinazojitokeza na kujirudia hususani katika uendeshaji wa kesi za makosa ya jinai. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaamini kwamba, maadhimisho haya yamekuwa alama ya mabadiliko ya kisera na kisheria katika kulinda haki za binadamu nchini. 

Katika kuongeza msisitizo katika mambo chanya yaliyojadiliwa na kutolewa mapendekezo katika kilele cha Wiki ya Sheria mwaka 2020, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tumechambua hoja zifuatazo na kutoa mapendekezo: 

Mfumo wa haki jinai  
Tunaungana na kauli iliyotolewa na Mhe. Rais kuhusu changamoto katika uendeshaji wa kesi za jinai. Katika hotuba yake kama mgeni rasmi, Mhe. Magufuli alinukuliwa akisema;


“…kwa kweli bado kuna changamoto kubwa ya upelelezi wa kesi, jambo linalopelekea watu kunyimwa haki...ninawaomba Kitengo cha Upelelezi na wasimamizi wa sheria kitengo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahusika wote hili mlifanyie kazi. Watu wanateseka. Nimeshuhudia ukienda kwenye magereza, watu wanalia na wengine ni kesi za kusingiziwa”.

Kauli ya Mhe. Rais inaashiria kwamba Serikali inatambua changamoto zilizopo na iko tayari kuchukua hatua katika kudumisha ustawi wa haki za binadamu nchini hususani katika eneo la mfumo wa haki jinai. 

Tunapendekeza kwamba, Wizara ya Katiba na Sheria ifanye mabadiliko ya Sheria kuweka ukomo wa upelelezi kwenye kesi za jinai. Ikiwa mamlaka husika itashindwa kumaliza upelelezi ndani ya muda husika basi Mahakama iwe na mamlaka ya kufuta shauri husika. Pia makosa yote yawe na dhamana kwa kubadilisha masharti ya dhamana kulingana na aina ya kosa. Pendekezo hili litapunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa mahabusu kwenye magereza ambapo kwa mujibu wa takwimu asilimia 56.7 ya watu walioko magerezani ni mahabusu. Mabadiliko haya pia yatadumisha dhana ya mtu kutooneka kuwa na hatia mpaka pale mahakama itakapothibitisha. 

Pili, tunashauri kuwa Jamhuri/ofisi ya mwendesha mashtaka ufanye uchunguzi kikamilifu kabla ya kukamata na kushikilia watuhumiwa kwa muda mrefu. Kwa kuzingatia sheria za nchi, watuhumiwa wasishikiliwe zaidi ya saa 24 bila kufikishwa mahakamani na wapate haki ya kuwasiliana na ndugu au wanasheria wao wakati wote wa mahojiano.

Suala la Mabaraza ya Ardhi 
Tunaungana na Mheshimwa Rais katika hoja ya udhaifu wa utendaji wa Mabaraza ya Ardhi katika kutatua migogoro ya ardhi. Katika hotuba yake Mhe. Magufuli alinukuliwa akisema;

“Changamoto nyingine ambayo bado naiona ni kuendelea kukithiri kwa migogoro ya ardhi,… na pia dhulma dhidi ya wanawake hususani wanawake wajane. Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi ya namna hii kila ninapofanya ziara maeneo mbalimbali nchini. Sina uhakika kama mabaraza ya ardhi yanafanya kazi zao vizuri…nafikiri imefika wakati Mabaraza ya Ardhi yawe chini ya Mahakama ili utendaji wake uweze kudhibitiwa”.

Kwa mwaka 2019 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia vituo vyake vya msaada wa sheria kilipokea malalamiko ya migogoro ya ardhi yaliyohusisha Mabaraza ya Ardhi kwa kiwango cha asilimia 36 % ya kesi zote. 
Ni wazi kwamba, wananchi wanakumbana na changamoto hii katika Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Wilaya katika kutatua migogoro. Jambo hili linatokana na kukosa uweledi na uwezo mdogo katika kutatua kesi za ardhi. Tunaendelea kupendekeza maboresho ya sheria ili kuunganishwa Mabaraza ya Ardhi na mfumo wa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweka usimamizi mzuri na uwajibikaji wake. 

Mwisho, tunaendelea kuungana na wadau wa haki za binadamu nchini katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini ili kustawisha utu, umoja na mshikamano nchini. Lengo la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni kufikia Jamii yenye Haki na Usawa – jamii ambayo kila mmoja anaheshimu na kulinda haki za binadamu. 

#SimamiaHaki 
Imetolewa Februari 10, 2020 na, 
Anna Henga, 
Mkurugenzi Mtendaji