
Tito Magoti na Theodory Giyani wasota rumande miezi sita sasa
Ni takribani miezi sita tangu kukamatwa kwa Tito Magoti ambaye ni Afisa wa LHRC na mwenzake Theodory Giyani. Tito na Theodory walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambapo mpaka sasa wapo rumande kwani makosa hayo hayana dhamana.
Disemba 20, 2019, LHRC ilipokea taarifa za kutekwa kwa Tito na Theodory ambapo masaa matano baada ya kupaza sauti, jeshi la polisi lilijitokeza na kuthibitisha kuwashikilia wawili hao. Hata baada ya kukiri kuwashikilia, jeshi la polisi halikutoa haki ya dhamana wala haki ya uwakilishi kwa Tito na Theodory. Tito na Theodory walishikiliwa kwa takribani siku tano wakihojiwa na polisi bila uwepo wa mawakili wala ndugu.
Mchana wa Disemba 24, 2019 wawili hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam na kutuhumiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi ikiwemo utakatishaji fedha katika kesi Na. 137 ya mwaka 2019.
Tangu hapo kesi imekuwa ikitajwa na kuahirishwa kwa mara zaidi ya 13 kwa sababu kwamba upelelezi haujakamilika. Upande wa Jamhuri umekuwa ukiiambia mahakama kwamba upelelezi uko katika hatua nzuri lakini bado haujakamilika. Mahakama imekuwa ikiisihi Jamhuri kukamilisha upelelezi bila mafanikio.
Leo Juni 23, 2020 kesi ya Tito na Theodory imetajwa kwa mara ya 14 na kuahirishwa tena hadi Julai 8, 2020 ambapo bado upande wa Jamhuri umeendelea kurudia kwamba upelelezi uko katika hatua nzuri lakini haujakamilika. Upande wa utetezi wameendelea kuisihi mahakama kutoa haki kwa watuhumiwa hasa kwa kuzingatia kwamba makosa yao hayana dhamana na upande wa upelelezi hauwajibiki kuhakikisha mchakato huo unakamilika ili kesi iweze kusikilizwa.
Misingi ya haki ya asili na haki jinai inatamka kwamba kila mtu atahesabiwa kutokuwa na hatia mpaka pale itakapothibitishwa na mahakama. Ucheleweshaji wa haki ni moja ya changamoto kubwa kwa wananchi kupata haki zao ikiwemo haki ya kuwa huru na kuwa sawa mbele ya sheria. Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amenukuliwa akionesha kusikitishwa na ucheleweshaji wa kesi unaopelekea kulundikana kwa watuhumiwa mahabusu wakisubiri upelelezi kukamilika.
Kama watetezi wa Haki za Binadamu, LHRC tunazisihi mamlaka husika kukamilisha upelelezi ili hatua za kusikilizwa kwa kesi zianze na hatimaye vijana hawa kupata haki zao.