TAMKO: SIKU YA WANAWAKE WA VIJIJINI  “Mwanamke anayeishi kijijini ni msingi wa ustawi na maendeleo ya Nchi”

TAMKO: SIKU YA WANAWAKE WA VIJIJINI “Mwanamke anayeishi kijijini ni msingi wa ustawi na maendeleo ya Nchi”

Posted 3 years ago

Siku ya Wanawake wa Vijijini ilianzishwa mwaka 2008 kwa lengo maalum la kutambua mchango wa wanawake wa vijijini katika maendeleo ya kilimo, maendeleo ya vijijini, na kuondoa umasikini katika jamii zetu sambamba na kukabiliana na changamoto wanazopitia.

Watu wa vijijini hasa wanawake ni muhimu sana katika kuleta maendeleo na kuondoa umasikini lakini ndio kundi ambalo limekuwa likikosa kipaumbele. Ukosefu wa huduma mbalimbali vijijini ikiwemo ajira, huduma bora za afya, elimu, umeme, maji na uhafifu wa miundombinu hufanya watu wengi kuhamia au kutamani kuhamia mijini. Kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kijamii kisiasa na kiuchumi kuna haja kubwa ya kuangalia mahitaji na umuhimu wa kulinda wanawake na wasichana wa vijijini lakini zaidi kutambua mchango wao mkubwa na kuweka mazingira wezeshi ya kuwawezesha kusonga mbele.

Wanawake wa vijijini ni zaidi ya robo ya watu wote duniani ambapo asilimia 43% hujishughulisha zaidi na kilimo hasa katika nchi zinazoendelea. Katika idadi ya wanawake nchini Tanzania asilimia 77.9% ni wanawake wa vijijini na 22.1 ni wanawake wa mijini. Wanawake na wasichana wengi wa vijijini hawana elimu na hawawezi kuingia katika ushindani wa ajira na pia wamekuwa wakiathiriwa zaidi na mila na desturi na kutokuwa na usawa wa kijinsia vitu vinavyoongeza vikwazo katika kufikia haki pale wanapofanyiwa vitendo vya kikatili.

Muundo wa kisheria

Hakuna sheria maalumu nchini Tanzania ya kulinda wanawake wa vijijini lakini Tanzania imetia saini mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Kupinga Aina Yoyote ya Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) pamoja na Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake wa Afrika (Maputo protocol) ambayo yote imetoa vifungu maalum vya kutetea haki za wanawake wa vijijini.

Ibara ya 14 ya Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Aina Yoyote ya Ubaguzi Dhidi ya Wanawake inataka nchi wanachama kuangalia kwa kina matatizo wanayokutana nayo wanawake wa vijijini na mchango wao katika jamii na kuhakikisha haki zao zinalindwa. Mkataba huo umeenda mbele zaidi na kusema kuwa nchi wanachama zihakikishe kuwa wanaondoa aina zozote za ubaguzi dhidi ya wanawake wa vijijini ili kuhakikisha kuna usawa kati ya wanawake na wanaume na kuwa wanawake wa vijijini wanashirikishwa ipasavyo na wananufaika katika maendeleo ya nchi yao. Kwa kufanya hivyo nchi wanachama watahakikisha kuwa wanawake wa vijijini wanashirikishwa na wanaeleweshwa kuhusu mipango ya maendeleo, wanapata huduma ya afya ipasavyo, wananufaika kutokana na huduma mbalimbali za kijamii, wanapata elimu na mafunzo mbalimbali kuhusu maisha na maendeleo yao, wanaanzisha vikundi mbalimbali vya maendeleo ili kupata nafasi sawa katika ajira na biashara, wanashiriki na kushirikishwa katika shughuli za jamii, wanapata nafasi kupata mikopo na masoko kuhusu bidhaa zao za kilimo, wanafurahia maisha bora katika viwango vinavyofaa.

Mwaka 2016 kamati ya CEDAW ilitoa mapendekezo ya jumla namba 34 ambayo yaliomba nchi wanachama kuhakikisha haki za wanawake na wasichana wa vijijini kuhusu ardhi, usawa wa kijinsia na usalama wao vinapewa kipaumbele.

Japo Tanzania imechukua juhudi za makusudi kuhakikisha tunafikia usawa wa kijinsia, bado wanawake wa vijijini wamekuwa wakipitia changamoto nyingi ambazo zinahitaji juhudi zaidi kuweza kusaidia. Changamoto hizo ni pamoja na sheria kandamizi hasa katika masuala ya mirathi na ndoa, kutokuwa na usawa katika upatikanaji wa masoko na umiliki ardhi vijijini, mila na desturi zilizopitwa na wakati ikiwemo ukeketaji ambao kwa vijijini ni asilimia 13.1 ukilinganisha na mijini ambapo ni aslimia 5.5.

Changamoto nyingine ni pamoja na mfumo dume ambao umeshamiri sana vijijini, ukosekanaji wa huduma bora za afya , ukosekanaji wa elimu bora na mwamko wa elimu hiyo, kukosekana kwa wanawake wengi kutoka vijini katika ngazi za maamuzi na uongozi, ajira kwa watoto hasa wa kike, ukosefu wa ajira na changamoto nyingine nyingi ikiwemo zaidi ukatili wa kijinsia ambao umeshamiri sana kila mahali na zaidi vijijini, ukosekanaji wa haki kutokana na kutokuwa na elimu kuhusu haki zao.

Mapendekezo kwa lengo la maboresho

 • Serikali ihakikishe kuwa sheria za kimila zinazokandamiza wanawake wa vijijini ziweze kufutwa na kuhakikisha matumizi zaidi ya sheria za nchi.
 • Kuhamasisha wadau wa vijijini, kikanda na kitaifa kutambua umuhimu wa wanawake na wasichana na ushirikishwaji wao katika masuala ya jamii na yanayowaathiri.
 • Kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijijini yanazingatia upatinakaji wa taarifa kuhusu wanawake wa vijijini
 • Kusaidia kuundwa kwa vikundi mbalimbali vya wanawake wa vijijini na kuwajengea uwezo kuhusu haki zao na pia kupata fursa mbalimbali
 • Kuhimiza watoto wa kike kwenda shule na kuboresha miundombinu ikiwemo usalama wao.
 • Kuwashawishi na kuwahimiza wanawake wa vijijini kushiriki katika ngazi za maamuzi ikiwemo midahalo ya sera
 • Kuunda mifumo bora ya elimu itakayopunguza ajira kwa watoto wa kike vijijini na kuwasaidia hasa wanapopitia changamoto za ndoa na mimba za utotoni.
 • Kuweka miundombinu bora ikiwemo afya na barabara ili kuwasaidia wanawake wa vijijini kupata msaada pale wanapohitaji
 • Kuachana na mila potofu na zilizopitwa na wakati ili kuhakikisha haki za wanawake wa vijijini zinalindwa ipasavyo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaamini kwamba usawa wa kijinsia utaharakisha maendeleo hasa vijijini ambapo kuna idadi kubwa ya wanawake. Jamii inapaswa kuamini katika usawa ili kuwapa wanawake fursa sawa na kutambua mchango wao.

#AminiaUsawa

Imetolewa na; Kituo cha Sheria na haki za Binadamu pamoja na Mtandao wa kupinga Ukeketaji Tanzania.