TAMKO: SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

TAMKO: SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

Posted 2 years ago

“TUTEKELEZE AJENDA 2040, KWA AFRIKA INAYOLINDA HAKI ZA MTOTO”

Siku ya mtoto wa Afrika imekuwa ikiadhimishwa kila tarehe 16 mwezi Juni ambapo siku hii ilianzishwa na Umoja wa Afrika kama njia ya kuwakumbuka Watoto wote walioshiriki katika maandamano ya Soweto ya kutetea haki za Watoto hasa kwenye elimu na kupinga ubaguzi.

. Siku hii inalenga kutoa elimu kuhusu hali na ustawi wa Watoto wa Afrika kama ilivoainishwa katika ibara ya pili hadi ya 22 ya Mkataba wa Afrika wa haki na Ustawi wa Mtoto

Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwa mwaka 2021 yanajikita katika kauli mbiu isemayo “Tutekeleze ajenda 2040; kwa Afrika inayolinda haki za mtoto”. Ajenda 2040 ilianzishwa na kamati ya Afrika ya Haki na Ustawi wa Mtoto hapo mwaka 2016 ikiwa na lengo kuu la kuiandaa Afrika kuwa bora zaidi kwa ustawi wa mtoto, ikiwemo kuhakikisha mipango endelevu kwa watoto kwenye elimu, afya, ustawi na ulinzi wa mtoto wa kiafrika. Ajenda 2040 inataka mataifa wanachama wa umoja wa Afrika kujiwekea mipango mikakati ya miaka 25 ya kulinda ustawi wa mtoto katika maeneo kumi muhimu.

Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na ya kikanda inayolinda na kutetea haki na ustawi wa mtoto. Tanzania pia ilitunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ikiwa na lengo la kusimamia zaidi kuhusu haki za watoto nchini. Pamoja na hayo Tanzania imetengeneza miongozo mbalimbali na mipango mikakati katika ulinzi wa mtoto ikiwemo mpango mpya wa ulinzi wa watoto wanaokinzana na sheria. Pamoja na yote haya bado haki za watoto nchini Tanzania hazijasimamiwa ipasavyo.

Watoto wa Tanzania wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi sana hasa watoto wanaokinzana na sheria ambapo upatikanaji wa haki na huduma bora kwao bado ni changamoto. Watoto wa kike wengi wameshindwa kufikia ndoto zao kutokana na kupata ujauzito wanapokuwa shuleni na kutoweza kurejea shuleni. Mwaka 2020 watoto zaidi ya 6000 wa shule za msingi na Sekondari walipata ujauzito na kukatisha masomo yao hiyo ni kulingana na taarifa ya BEST. Watoto pia wanakumbwa na vitendo vya ukatili uliokithiri ambapo taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2020 imeendelea kuonesha ukatili ukiongezeka kwa watoto hasa ukatili wa kingono.

Katika kuungana na wote kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa serikali kulinda haki na ustawi wa mtoto ikiwemo kwenye nyanja za elimu, afya, haki hasa kwa watoto wanaokinzana na sheria pamoja na ulinzi wa jumla wa watoto wa Tanzania. Ni matumaini yetu kuwa Tanzania ikisimamia ipasavyo sheria zetu, mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusu watoto tutaweza kusaidia kulinda haki za watoto nchini Tanzania.

Kituo cha sheria na Haki za Binadamu tunaiomba serikali kutenga bajeti inayozingatia mahitaji katika ulinzi wa Watoto dhidi ya vitendo vya Ukatili na ulinzi wa haki za Watoto.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, tunaamini kuwa tukisimamia na kutekeleza ipasavyo ajenda 2040, tutatengeneza Tanzania inayoheshimu, inayolinda na inayosimamia haki za Watoto.

Imetolewa na leo tarehe 16/06/2021 na;

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu