TAMKO LA KULAANI UFUKUAJI WA KABURI LA MAREHEMU HERI SHEKIGENDA KIJANGWA

TAMKO LA KULAANI UFUKUAJI WA KABURI LA MAREHEMU HERI SHEKIGENDA KIJANGWA

Posted 2 years ago

TAMKO LA KULAANI UFUKUAJI WA KABURI LA MAREHEMU HERI SHEKIGENDA KIJANGWA

Ndugu wanahabari,

Tumewaita leo kufuatia taarifa za kusikitisha tulizozipokea kuhusu tukio la kufukuliwa kwa kaburi la Marehemu Heri Shekigenda Kijangwa. Heri alikuwa ni mtu mwenye ualbino ambaye alifariki tarehe 4 July 2020 kwa maradhi ya kansa ya ngozi akiwa na umri wa miaka 45 na mwili wake kuhifadhiwa tarehe 7 July 2020 katika Kijiji cha Tanda Wilayani Lushoto Mkoani Tanga. Katika hali isiyo ya kawaida, tulipokea taarifa ya kufukuliwa kwa kaburi la marehemu Heri Kijangwa mnamo tarehe 24 Octoba 2021. Tukio hilo lilifanywa na watu wasiyojulikana na cha kusikitisha zaidi watu hao walinyofoa mguu wake wa kulia na kutoweka nao kusikojulikana.

Ndugu wanahabari,

Kwa mwaka 2021 tukio hili ni la pili kuripotiwa. Ikumbukwe kuwa kati ya Mei 3 na 4 mwaka huu wa 2021, iliripotiwa kwamba mwili wa mtoto mwenye ualbino aliyekuwa na umri wa miaka mitano uliokotwa ukiwa umekatwa mikono yote miwili huko Kijiji cha Nondo, Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora na taarifa ya uchunguzi haijawahi kutolewa na jeshi la polisi hadi leo.

Hizi ni habari mbaya kuanza kusikika tena kwenye masikio ya Watanzania na watetezi wa Haki za Binadamu kwa mwaka huu. Ni matukio yanayovunja haki, utu na heshima ya binadamu kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu pamoja na sheria za nchi yetu kama vile Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 (Marejeo ya 2019). Ni ukweli kwamba, hofu, wasiswasi na mashaka kwa watu wenye ualbino imeanza kurudi kufuatia mtiririko wa matukio haya. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita matukio haya yalikoma kabisa kutokana na jitihada madhubuti za serikali kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vya habari.

Ndugu wanahabari,

Kwa masikitiko makubwa, Kituo cha sheria na Haki za Binadaamu (LHRC) kwa kushirikiana Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) tunalaani vikali vitendo hivi vya kikatili na vya kinyama vinavyotweza utu wa binadamu na vya kudhalilisha maiti.

Kitendo cha kufukua mwili wa marehemu Heri Shekiganda Kijangwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 127 na 128 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 (kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019). Tunafahamu kwamba tukio hili limeripotiwa kwenye Kituo cha Polisi cha Bumbuli kilichopo Wilaya ya Lushoto. Tunahimiza Serikali pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba kesi hii haitaishia kwenye ngazi ya upelelezi badala yake watuhumiwa wote wafikishwe Mahakamani na adhabu kali itolewe ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria na haki za binadamu hapa nchini.

Limetolewa leo tarehe 01 Novemba 2021.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC); Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS); Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)