TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA KULAANI MAUAJI YA WATOTO 10 MKOANI NJOMBE ​​​​​​​

TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA KULAANI MAUAJI YA WATOTO 10 MKOANI NJOMBE ​​​​​​​

Posted 4 years ago

Sisi asasi za kiraia na wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) tumesikitishwa sana na  mauaji  ya kikatili ya  watoto kumi (10) yaliyotokea  huko Mkoani  Njombe Januari, 2019. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi chanzo kikuu cha mauaji hayo inasemekana kuwa ni imani za kishirikina kwani miili ya watoto hao ilikutwa ikiwa imekatwa makoromeo na sehemu za siri.

Kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambavyo vinatweza utu wa mtoto kama binadamu, vinamkosesha mtoto ustawi na ukuaji bora na pia matukio haya yanapelekea kupoteza maisha kwa watoto wengi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa nusu mwaka 2018 kumekuwa na ongezeko la ukatili dhidi ya watoto ambapo jumla ya matukio 6376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa. Ripoti hiyo pia inatanabaisha kwamba katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018 watu 17 wanauawa kwa sababu ya imani za kishirikina ambapo hadi kufikia Juni 2018 jumla ya watu 106 waliuawa. 

Watekelezaji wa matukio ovu dhidi ya watoto huwa wanawateka kisha kuwafanyia unyama na hatimaye kuwaua huku wakichukua baadhi ya sehemu za miili yao na kisha kuwatelekeza. Na ni dhahiri kwamba matukio ya utekaji hapa nchini yamezidi kushamiri licha ya jitihada mbali mbali zinazofanywa na jeshi la polisi pamoja na wananchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola, kwa kipindi cha miaka mitatu watu wapatao 75 walitekwa. Waziri Lugola alikaririwa akisema licha ya juhudi za polisi nchini, mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu 9 kutekwa lakini watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirikiano na wananchi. "Watu wanne hawakupatikana, katika kipindi hicho na ambapo watuhumiwa sita walikamatwa; watano walifikishwa mahakamani na mmoja aliuawa na wananchi," 

Waziri Lugola alisema kwa mwaka 2017, watu 27 walitekwa na polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa, huku watatu wakiwa hawajulikani walipo hadi sasa. Katika kipindi cha "Januari hadi Oktoba 11, 2018, watu 21 walitekwa ambapo kati yao 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi sasa. Watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani,"

Kuhusu utekaji wa watoto, Lugola amesema tangu mwaka 2016 ni watoto 18; (wakiume 6) na (wakike 12) waliokumbwa na adha hiyo. Aidha watoto 15 walipatikana wakiwa hai, wawili walipatikana wakiwa wamefariki huku mtoto mmoja akiwa bado hajulikani alipo hadi sasa.

Tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuheshimu na kulinda haki za watoto, sambamba na kulinda haki ya kuishi kwa kuzingatia kwamba haki hiyo ni haki ya msingi kwa kila binadamu. Haki ya kuishi inalindwa  na Katiba  yetu  ya  Jamhuri  ya  Muungano wa Tanzania, 1977 kupitia  Ibara  ya 14. Hivyo basi kuvunja haki hii ni kukiuka Katiba pamoja na mikataba mbali mbali ya Kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mwanachama. 

Pia, Tanzania imetia saini mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolinda haki ya kuishi na kutoteswa na pia Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 ambalo linalinda haki ya kuishi. Sheria ya Mtoto, 2009 kifungu cha 9 kinalinda haki ya kuishi na kifungu cha 13 kinalinda watoto dhidi ya matendo yanayotweza utu wao.

Pia ikumbukwe kuwa watoto ni kundi ambalo kwa namna moja au nyingine, hawawezi kupata baadhi ya haki zao bila kupata msaada wa wengine. Hivyo, jamii lazima iwe mstari wa mbele kulinda na kutetea haki za mtoto yeyote yule anayeonekana kuwa katika mazingira hatarishi na/ama ambaye haki zake zimevunjwa, zinavunjwa au inaelekea zitavunjwa. Tukumbuke kwamba; “mtoto wangu ni mtoto wako” na “mtoto wako ni mtoto wangu” 

Mauaji  yaliyotokea  mkoani Njombe  yanapaswa kukemewa vikali na kila mmoja wetu. Sisi asasi watetezi wa haki za binadamu tunawasihi Watanzania, wadau na Serikali kuheshimu haki za watoto na kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya kikatili kwa kufanya yafuatayo;

 1. Kuheshimu sheria zinazolinda haki za mtoto 
 2. Kutimiza wajibu wa kuwalinda watoto bila kujali uhusika wa moja kwa moja kwani mtoto anahitaji ulinzi kutoka kwa jamii nzima.
 3. Kutoa taarifa pale ambapo wanahisi mtoto hayuko salama na kumpeleka sehemu salama.
 4. Kuhakikisha wanawalinda watoto wao kwa kufatilia sehemu wanazokwenda na kuhakikisha wanakuwa karibu nao.
 5. Kuacha kuamini mila potofu ambazo zinapelekea uvunjifu wa haki za binadamu ikiwemo haki za watoto na kupelekea watoto kupitia mateso makali na hatimaye kupoteza maisha.

Wito wetu;

 • Tunatambua juhudi zinazoendelea kufanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na jeshi ka polisi na tunazidi kuisihi Serikali kupitia jeshi letu la polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika kubaini kiini cha mauaji hayo, na kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika kupanga na/ama kutekeleza mauaji haya ya kikatili dhidi ya watoto wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria. 
 • Tunaisihi Serikali kuchukua hatua za haraka na za makusudi za kuongeza  ulinzi dhidi ya watoto hasa katika maeneo yenye viashiria vya ukatili dhidi ya watoto. 
 • Tunawaomba waandishi wa habari kuendelea kukusanya habari na kuwaripoti wale wote wanaokiuka haki za watoto kwani ni imani yetu kwamba matukio makubwa kama haya ni zao la kufumbia macho matukio madogo madogo ya ukiukwaji wa haki za watoto.
 • Tunaishauri Serikali kuongeza udhibiti kwa waganga wa jadi wanaofanya ramli chonganishi kwa kuwachukulia hatua kali pale wanapothiditika kupelekea uvunjifu wa haki. 
 • Pia tunawaomba wafiwa wote na watanzania kwa ujumla, kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili hatimaye wahusika wote wabainike na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kukabiliana na mashataka dhidi yao. 

Mwisho tunatoa salamu za pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa haki ambao wameguswa na tukio hilo la kusikitisha na kuwaombea marehemu wote na Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi, Amina. 

Imetolewa Januari 31, 2019 na;

 1. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
 2. Msichana Initiatives
 3. Agape Aids Control Program
 4. Faidika Wote Pamoja
 5. Paralegal Primary Justice
 6. JUMAEWAPE
 7. PEMCO
 8. KIWOHEDE
 9. Children Dignity Forum
 10. K.O.K Foundation
 11. ZAFAYCO
 12. Msichana na Uongozi 
 13. Micheweni Islamic Development Environment Conservation and AIDs Control (MIDECAC)
 14. Door of Hope to Women and Youth Tanzania
 15. Zanzibar Aids Association and Support for Orphans (ZASO)
 16. New Hope New Winners Foundation
 17. Zanzibar Association for Children Advancement 
 18. Morogoro Paralegal
 19. Mbeya Hope for Orphans
 20. Tanzania Youth Potential Association
 21. Girl on Fire for Change
 22. Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC)
 23. TAWIA
 24. UVUUMA
 25. Child Watch