
Tamko Kupinga Mamtumizi Mabaya ya Mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu katika muendelezo wa kufuatilia matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu kimepokea taarifa mbalimbali zinazoashiria kuongezeka kwa matumizi mabaya ya mamlaka ya kisheria chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa No. 9 ya mwaka 1997 kwa wakuu wa Wilaya na wakuu wa Mikoa. Kwa pamoja Kituo kinapinga ukamataji wa kiholela kwa amri za Wakuu wa Wilaya kuwakamata na kuwaweka ndani masaa 48 kinyume na Katiba na misingi ya Haki za Binadamu.
Mnamo tarehe 30 Julai, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Ndugu Alexandar Mnyeti alitoa kauli ya kumkamata na kumuweka ndani masaa 48 Mwanasheria, Wakili Meinrad Menino D’Souza pamoja na mteja wake akiwa anatimiza majukumu yake ya kiwakili.
Katika muendelezo huo Agosti 16, 2018 Mkuu wa Wilaya ya Hai Ndugu Lengai Ole Sabaya aliamuru kukamatwa kwa Wakili Edward John Mrosso ambaye baadae aliachiwa kwa dhamana akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake. Amri zote hizo zilitolewa kinyume na Tamko la Kimataifa la Majukumu ya Mawakili 1990 na Kinyume na haki ya uwakilishi kama inavyotambuliwa na Sheria ya Mawakili Sura ya 341 ya mwaka 2002.
Ifahamike kwamba, Wakili Meinrad Menino D’Souza na Edward John Mrosso walikuwa wakitimiza majukumu yao ya kiuwakili yaliyopo kisheria kwa kutoa huduma kwa mteja wao.
Kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Tamko la Kimataifa juu ya Majukumu ya Mawakili;
‘’Serikali zitahikiksha kwamba wanasheria wanaweza kufanya kazi zao za kitaaluma bila vitisho, vizuizi, kudhalilishwa au kusumbuliwa bila sababu na wanaweza kusafiri na kuwasiliana na wateja wao kwa uhuru ndani na nje ya nchi….’’
Mnamo Agosti 15, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Ndugu. Albert Chalamila aliamuru wanakijiji wa Kijiji cha Ngole wakamatwe na kuwekwa ndani kwa tuhuma za uharibifu wa miundo mbinu ya maji. Kitendo cha kuamuru wanakikiji wote wakamatwe ni kinyume na haki ya asili pamoja na dhana ya kutokuwa na hatia kwa mujibu wa Ibara ya 13(6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, Jeshi la Polisi limeonesha kutozingatia weledi kwa kukiri kutekeleza agizo hilo kitendo ambacho kinaweza kupelekea uvunjifu wa amani na madhara makubwa katika utekelezaji wake hususani kwa makundi mbalimbali ikiwemo wagonjwa, watoto, watu wanaoishi na ulemavu na wazee.
Pia, matumizi ya hovyo ya kifungu cha 7 na 15 cha Sheria ya Tawala za Mikoa, 1977 ni kinyume na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, Ibara ya 13(2) inayosema;
“Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”.
Hivyo, kuendelea kwa vitendo vya matumizi mabaya ya mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kunaweka mfano mbaya katika jamii juu ya utawala wa sheria nchini. Vitendo hivi pia vinapelekea mwendelezo mbaya wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Ikumbukwe hivi karibuni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Suleiman Jafo alitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutotumia mamlaka yao vibaya na kuwaweka watu mahabusu pasipo na sababu za msingi.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na jumuiya ya mawakili Tanzania na kote ulimwenguni kutetea uhuru wa mawakili na kuhakikisha wanafanya kazi zao pasipo kuingiliwa na maagizo ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwani vitendo hivyo vinanyima haki ya uwakilishi kwa wahitaji na kufanya wanajamii kushindwa kupata haki kwa wakati. Pia, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinawataka viongozi wa Serikali ya Tanzania kuheshimu Mikataba ya Kimataifa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria katika utekelezaji wa majukumu kwa lengo la kustawisha jamais ya Watanzania.
Imetolewa Agosti 18, 2018, na;
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji