
TAMKO: KUKEMEA VITENDO VYA UNYANYASAJI NA UKEKETAJI DHIDI YA WATOTO
Tarime, Mara Tanzania
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakemea vikali vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watoto hasa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike vinavyofanywa katika mkoa wa Mara hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka. Kwa mujibu wa mashuhuda ambao ni wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoani Mara, watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 17 hukeketwa kwa njia ya kikatili kwa kipindi cha mwezi wa 12 kwa kuwa watoto hawa wanakuwa wako katika likizo ya mwisho wa mwaka.
Mathalani vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike wenye umri mdogo vimekithiri sana mwishoni mwa mwaka huu 2020 kwasababu kwa mujibu wa mila na desturi za wenyeji wa mkoa wa Mara zoezi la ukeketaji linatakiwa kutekelezwa kwa miaka inayogawanyika kwa mbili wakiamini kuwa endapo watakiuka utaratibu huu watapata mkosi. Kukithiri kwa vitendo vya ukatili huu unaoendelea mkoani Mara mpaka sasa umesababisha kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaokimbia familia zao na kutafuta hifadhi katika nyumba salama zilizoanzishwa na wadau wakupinga ukatili dhidi ya watoto Mkoani Mara.
Mpaka sasa kituo cha kuhifadhi watoto kilichopo wilayani Tarime cha ATFGM Masanga kwa mwezi Disemba peke yake wamepokea jumla ya watoto 438 waliokimbia familia zao kwa kuhofia kukeketwa. Kila mtoto amewasili katika kituo hicho kwa njia yake wengine wametoroka usiku wa manene ili kujiokoa. Vilevile Shirika la Hope for Girls and Women lenye makao yake makuu katika Mugumu wilayani Serengeti kimepokea jumla ya watoto 198 kwa kipindi cha Novemba hadi mwezi huu wa Disemba pekee ambapo inafanya jumla ya watoto waliokimbia familia zao kwa kipindi cha Novemba hadi Disemba hapa mkoani Mara kufikia 636. Hii ni baadhi tu ya watoto wenye ujasiri walioweza kutoroka ukeketaji kwa kuhofia maisha yao lakini wengi zaidi wamekeketwa.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Aloys Henga ameeleza madhara makubwa yanayowapata watoto wanaopitia ukeketaji mkoani Mara;
‘Ukeketaji kwa watoto wa kike ni unyanyasaji mkubwa kwa watoto na huweza kupelekea kuvuja damu nyingi na majeraha makubwa, pia inasikitisha sana kuona wanajamii hasa wa mkoa wa Mara kuendeleza mila zilizopitwa na wakati ambazo mara nyingi husababisha maumivu makali na kuweza kupelekea vifo kwa watoto, Nawasihi sana kuachana na unyanyasaji huu mkubwa.Nakemea vitendo hivi vya ukeketaji kwa nguvu zote na nawasihi wadau pamoja na wanajamii kupinga vitendo hivi vya kikatili kwa watoto’’
Kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binadamu inayotolewa na Kituo cha sheria na Haki za Binadam ya mwaka 2019, matukio ya ukatili wa kimwili yanaendelea kuwa changamoto katika ufurahiaji na utekelezaji wa haki za watoto kwa mwaka 2019. Ukatili wa kimwili dhidi ya watoto husababisha madhara makubwa kama vile kupelekea watoto kupata majeraha mbalimbali katika miili yao, yakiwemo majeraha ya kudumu, kupata ulemavu, na hata kufariki. Ripoti ya haki za binadamu imeonyesha pia kuwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2019, LHRC ilikusanya jumla ya matukio 26 ya ukatili dhidi ya watoto yaliyopelekea vifo vya watoto hao.
Kwa takribani miaka 7 sasa LHRC imekuwa mratibu wa Mtandao wa kupinga ukeketaji Tanzania na tumekuwa tukishiriana na wadau wengine pamoja na serikali ili kukomesha ukatili kwa wanawake na watoto. Ingawa kumekuwa na jitihada kubwa za kupinga na kukomesha ukatili dhidi ya watoto hasa ukeketaji bado wanajamii Mkoani Mara wanakeketa watoto na kufanya sherehe kubwa bila hofu yoyote. Ni vyema serikali kuu kuingilia kati suala hili ili kuweza kuokoa maisha ya watoto wa kike wanaopitia ukatili mkubwa na wengine kupoteza uhai hasa mkoani Mara ambapo uketetaji unafanywa waziwazi bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Imetolewa Disemba 21, 2020
Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na;
Anna Henga, Mkurugenzi wa LHRC,
Barua Pepe; ahenga@humanrights.or.tz