TAMKO KUKEMEA UDHALISHAJI ULIOFANYWA NA POLISI KWA MAMA MJAMZITO, BI AMINA RAPHAEL MBUNDA,

TAMKO KUKEMEA UDHALISHAJI ULIOFANYWA NA POLISI KWA MAMA MJAMZITO, BI AMINA RAPHAEL MBUNDA,

Posted 6 years ago

Wadau wa kupinga ukatili kwa wanawake na watoto wamesikitishwa na taarifa zilizowafikia kutoka kwa waangalizi wa haki za binadamu na vyombo vya habari vikieleza kwamba Bi Amina Raphael Mbunda, mkazi wa Kitongoji cha Kaswanya, Tarafa ya Man’gula, Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro alikamatwa Tarehe 31/05/2018, saa 3 usiku na Afisa wa Polisi kwa tuhuma zinazomhusu mumewe ambaye alikuwa anatafutwa kwa tuhuma za kununua kitanda kinachohusishwa na wizi. Bi Amina alikuwa mjamzito na Afisa wa Polisi alimuweka kizuizini katika Kituo cha Polisi Mang’ula kinyume na sheria na taratibu za nchi na bila kuzingatia hali aliyokuwanayo  na kusababisha Bi Amina kupata uchungu na kujifungua saa tisa usiku katika mazingira hatarishi na yakudhalilisha  utu wake. Tumesikitishwa sana kuona kuwa wasimamizi wa sheria ndio wamekuwa wavunja sheria.

Wadau wa Kupinga Ukatili kwa wanawake tunakemea vikali ukamatwaji wa kiholela usiozingatia sheria za nchi hasa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya 2002 na Sheria za Polisi sura ya 322 ambazo kwa pamoja haziruhusu mtu kukamatwa kwa kosa la jinai analotuhumiwa kufanya mtu mwingine bila kujali uhusiano wao. Ibara ya 13(6)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mambo mengine inataka vyombo vya dola kuzingatia uhifadhi wa haki ya usawa wa binadamu, na heshima ya mtu katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu. Kwa mujibu wa Ibara hii ya katiba vitendo vyote vya unyanyasaji wa raia wanapokuwa kizuizini ni kinyume na sheria na havikubaliki.

Pamoja na hayo kitendo hichi kimeweka hatarini maisha ya mama na mtoto tukifahamu haki ya afya na uzazi salama ni haki za wanawake zinazotambulika kimataifa na kitaifa. Tanzania ina Sera na Mikakati mbali mbali ya kusaidia uwepo wa afya na huduma stahiki za uzazi kwa wanawake na watoto. Kitendo hichi kilichofanywa na jeshi la polisi kimehatarisha afya na uzazi salama wa Bi Amina na mwanae. Wadau wanalikumbusha Jeshi la Polisi kuzingatia weledi katika utendaji kazi hasa kuheshimu sera na sheria zilizopo. Bi Amina hakuwa mtuhumiwa wa wizi na kulingana na hali na afya yake hakutakiwa kuwekwa kizuizini/rumande. Tukio hili pia linaendeleza kuongezeka kwa idadi ya matukio ya watu kufanyiwa ukatili na udhalilishwaji wa utu wakiwa mikononi mwa polisi kama ambavyo yamekuwa yakiripotiwa katika vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni.

Wadau wa Kupinga Ukatili kwa Wanawake tunamtaka Mkuu wa Jeshi la polisi nchini kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wake ambao wameshindwa kufanya kazi kwa weledi na kusababisha kuweka hatarini maisha ya Bi Amina na mwanae pamoja na udhalilishaji wa utu. Pia Wadau wanawataka maafisa wa jeshi la polisi nchini kuzingatia miongozo katika utekelezaji wa kazi zao na kutambua na kuheshimu misingi ya haki na utu wa binadamu na hasa wajibu wao wa kulinda haki za raia. Mwisho tunawahamasisha wadau wote wa haki za binadamu hasa wananchi kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wote wanaokiuka sheria na misingi ya haki za binadamu hasa haki za wanawake na watoto katika muktadha huu.

Imetolewa leo Juni 8, 2018 na

Wadau wa Kupinga Ukatili kwa Wanawake na Watoto

Tamko Kupinga Ukatili dhidi ya Bi Amina