Tamko kuhusu Kushikiliwa kwa Sheikh Issa Ponda

Tamko kuhusu Kushikiliwa kwa Sheikh Issa Ponda

Posted 2 years ago by admin

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimepokea taarifa za kukamatwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye ni Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania mnamo tarehe 11 Julai, 2020.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa tarehe 14 Julai 2020 na Kaimu Katibu Mkuu Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda alikamatwa na jeshi la polisi mnamo majira ya saa 11 jioni akiwa ofisini kwake Ilala-Dar es Salaam na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kati kwa mahojiano.

Hata hivyo, mpaka hivi sasa haijulikani Sheikh Issa Ponda anashikiliwa katika Kituo kipi cha Polisi pamoja na kuwa jeshi la polisi limekiri kumshikilia kwa mahojiano. LHRC tunasisitiza kufuatwa kwa utaratibu wa haki za mtuhumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwendeno wa Makosa ya Jinai, (Sura ya 20) ya mwaka1985.

Sheria ya Mwendeno wa Makosa ya Jinai inatoa haki ya mtuhumiwa kuwasiliana na ndugu zake akiwa kizuizini, haki ya kuwasiliana na mwanasheria wake kwa wakati wote akiwa chini ya kituo cha polisi pamoja na hayo sheria hii inaweka haki ya mtuhumiwa kupata dhamana kwa kosa lolote linalodhaminika chini ya sheria hii.

Kifungu cha 30 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaelekeza kwamba afisa wa polisi aliemkamata mtuhumiwa wa kosa lolote anapaswa kumuachia mtuhumiwa kwa dhamana kulingana na sheria au kumfikisha mahakamani bila kuchelewa. Kifungu cha 33 cha Sheria hii kinaelekeza kuwa Mkuu wa kituo cha polisi anatakiwa kutoa taarifa mahakamani ndani masaa 24 juu ya kesi zote za watuhumiwa waliokamatwa katika mipaka ya kituo chake.

LHRC tunatoa rai kwa jeshi la polisi kuzingatia maslahi na haki za mtuhumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwendeno wa Makosa ya Jinai (Sura Na. 20) ya mwaka 1985.

 

Imetolewa Julai 18 2020 na,

 

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji