TAMKO JUU YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA OPERESHENI SANGARA 

TAMKO JUU YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA OPERESHENI SANGARA 

Posted 6 years ago

Kituo cha Sheri na Haki za Binadamu katika muendelezo wa kupokea na kufuatilia taarifa mbalimbali za matukio ya ukiukwaji wa Haki za binadamu tumepokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi wanaoishi katika Kisiwa cha Ukerewe sambamba na maeneo mbalimbali yanayozunguka ziwa Victoria wakilalamikia kuvunjiwa haki zao na Serikali katika utekelezaji wa Operesheni Sangara. Aidha kituo Kimepokea malalamiko mbalimbali kutoka katika maeneo ya Uvuvi kama ziwa Manyara na Bwawa la Nyumba ya Mungu yote yakihusisha ukiukwaji wa haki za wavuvi na watu wanaojihusisha na biashara za uvuvi kufuatia operesheni mbalimbali zinazoendelea katika maeneo hayo. 

Katika kuthibitisha taarifa hizo tumefanya utafiti mdogo katika kisiwa cha Ukerewe kubaini sababu za malalamiko ya wavuvi na wananchi wa maeneo hayo. Kufuatia utafiti huo na ufuatiliaji wa kina, Kituo kimebaini mambo ya fuatayo;

  1. Matumizi ya Nguvu Kupita Kiasi: Kikosi kazi kinachotekeleza operesheni ya kuzuia uvuvi haramu( Operesheni Sangara) kimekuwa kikitumia nguvu kupita kiasi kinyume na sheria za nchi. Utafiti wetu umebaini kuwa zoezi limekuwa likifanyika wakati wa usiku na kuambatana na kuvunjwa kwa milango na kushambuliwa kwa watuhumiwa na familia zao kinyume na haki za binadamu na sheria za nchi. Ukamataji wa usiku na ukaguzi umekuwa ukufanyika bila vibali maalumu na maofisa wa Polisi wasiokuwa na vigezo kisheria . 
  2. Vitendo Vya Kikatili dhidi ya Raia: Kituo kimegundua pia kikosi kazi cha Operesheni Sangara kimekuwa kikifanya ukatili kwa wananchi  kwa kuwashambulia kwa kipigo pamoja na kuwafanyia vitendo vinavyotweza utu wa mtu  kinyume na Ibara ya 13 ya Katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waananchi wengi wamelalamika , kupigwa kwa magongo, kuchapwa bakora , kuzamishwa ndani ya maji na kupewa adhabu kali za kijeshi  pasipo sababu za msingi.
  3. Uharibifu wa mali na uporaji: Wananchi wanalalamikia  uharibifu mkubwa wa mali katika zoezi hilo , ikiwemo uchomaji na utaifishaji wa mitumbwi na zana nyingine za uvuvi, baiskeli, pikipiki vitendo ambavyo vimekuwa vikifanyika bila kufuata utaratibu wa sheria na watuhumiwa kutofikishwa mahakamani. Maofisa wanaoshiriki operesheni hiyo wamekuwa wakiingia kwa nguvu kwenye nyumba za wananchi na kupora mali zao kama fedha , na vitu  vingine vya thamani kinyume na sheria na wakati mwingine kuuza mali za wananchi kwa manufaa binafsi.
  4. Rushwa na tozo zisizo na viwango maalumu: Pamoja na kuwepo kwa kanuni ndogondogo za kuongoza utekelezaji wa Operesheni Sangara. Zoezi hilo limegubikwa na rushwa kupita kiasi wananchi wote wanaokamatwa wanalazimishwa kutoa fedha ambazo hazina viwango maalumu  nje ya utaratibu wa malipo ya serikali ili waweze kuachiwa. Viwango vinavyotozwa vinategemea uwezo wa mtu na si mwongozo wa sheria na hivyo kutengeneza mwanya wa mkubwa  rushwa baina ya watendaji.  
  5. Kukosekana kwa Usimamizi madhubuti wa watendaji wa operesheni: Kikosi kilichoundwa kupambana na uvuvi haramu hakipokei maelekezo yoyote kutoka kwa mkuu wa Wilaya , Mkurugenzi wa wilaya au Kamati ya Ulinzi na Usalama na hivyo kuathiri hatua mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa kisheria na vyombo hivyo ikiwepo ukiukwaji wa taratibu za kisheria. Kikosi kinapokea maelekezo moja kwa moja kutoka makao makuu ya Wizara ya Kilimo ,Mifugo na Uvuvi na  kuwanyima viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa usimamizi wa mambo ya kiutawala licha ya kuwa na uzoefu na maeneo wanayofanyia kazi..
  6. Kukamatwa kwa wananchi na kuwekwa kizuizini Kinyume na Sheria: Wananchi wamelalamikia vitendo vya watendaji wa operesheni vya kuwakamata na kuwaweka vituo vya polisi kwa kesi zisizokuwa na uthibitisho kwa nia ya kudai fidia na rushwa kinyume na sheria. Wengi wa wahanga wamewekwa kizuizini kwa kipindi cha kuanzia siku saba mpaka siku 14 wakilzazimishwa kutoa rushwa. Mashauri machache huelekezwa mahakamani kwa wale wanaoshindwa kulipa na kutupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.
  7. Mapungufu ya Sheria ya Uvuvi: Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 bado inamapungufu makubwa mabayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka ili kukuza sekta ya uvuvi.Sheria imetoa mamlaka makubwa kwa maofisa uvuvi , wasimaizi wa Fukwe (BMU) na Waziri wa Uvuvi ambayo yanapaswa kutazamwa upya na kufanyiwa marekebisho kisheria.

Hata hivyo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kama mdau mkubwa wa mazingira na ulinzi wa rasilimali za nchi, tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na uharibifu wa makusudi wa rasilimali na mazingira. Ili kuboresha sekta ya uvuvi na kuleta tija katika zoezi la kupambana na uvuvi haramu, Kituo cha Sheria na Haki za  Binadamu kinapendekeza mambo yafuatayo:

  1. Vyombo vyote vinavyoundwa kwa ajili ya kusimamia operesheni mbalimbali za uvuvi haramu vifanye kazi kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na sheria za nchi ili kuhakikisha haki za raia zinalindwa wakato wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
  2. Taasisi za serikali zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa,  Utawala Bora   pamoja na Ulinzi na Usalama wa Taifa kufanya uchunguzi wa kina kuhakikisha wale wote wanaokiuka sheria za nchi katika utekelezaji wa mamjukumu yao wanachukuliwa hatua.
  3. Serikali kuhakikisha wananchi  na viongozi wa serikali za mitaa wanashirikishwa ipasavyo   ili kuhakikisha operesheni zote zinatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
  4. Serikali kwa kushirikiana na asasi za kiaraia kuhakikisha elimu kwa uma inatolewa kwa kiwango cha kutosha ili kuwajengea uwezo  wananchi waweze kutambua umuhimu wa kuhifadhi mzingira na uvuvi  wa kisasa na kuwafanya  kuwa wasimamizi wa kwanza  wa shughuli za uvuvi.
  5. Serikali kuchukua hatua za haraka kuwaondoa haraka na kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wote wa operesheni sangara watakaobainika kukiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao  kama sehemu ya uwajibikaji kisheria.

Mwisho Serikali ichukue hatua za haraka kutengeneza mpango madhubuti wa kutatua  changamoto zinazowakabili wavuvi pamoja na sekta ya uvuvi kwa ujumla ili kunusuru sekta hiyo.

 

Imetolewa November 23, 2018 na; 

Bi. Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji