TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KULAANI TUKIO LA  MAUAJI LINALOMHUSISHA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA ITIGI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KULAANI TUKIO LA  MAUAJI LINALOMHUSISHA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA ITIGI

Posted 6 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesikitishwa na tukio la mauaji ya Bw. Peter Chambalo linalodhaniwa kufanywa na Mkurugenzi wa Wilaya ya ya Itigi Mkoani Singida Bw. Pius Luhende ndani ya Kanisa la Sabato siku ya Jumamosi Februari 2, 2019. Kitendo hicho ni uvunjifu wa haki ya kuishi kinyume na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inayoainisha haki ya kuishi  kama haki ya msingi ya binadamu. Pia ni ukikwaji wa   ibara ya 6 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, 1966 unaoainisha haki ya kuishi pamoja na kuweka jukumu la kulinda haki hiyo kisheria. 

“kila mtu ana haki ya kuishi”

Kanuni ya utawala wa sheria inaweka sharti la kutumia utaratibu maalamu kwa mtu yoyote uliowekwa kisheria katika kutekeleza majukumu bila kujali cheo, hadhi au nasaba ya mtu. Kwa tukio hilo ni wazi kwamba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi alijichukulia hatua mikononi bila kufuata misingi iliyowekwa kisheria katika kufanya jambo hilo. Pia, kitendo cha kuingia Kanisani kimeingilia uhuru wa kuabudu pamoja na faragha ya Kanisa hilo wakati wa kuabudu. 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinalaani na kinakemea tukio hilo lililotweza utu pamoja na kuondoa haki ya kuishi ya mtu huyo. Kituo kinalaani tukio hilo kwani lilifanyika kikatili na kutia hofu na taharuki wakazi wa eneo hilo waliokuwa wamekusanyika kwa Amani wakifanya ibada siku ya Sabato.  Kituo  kinatoa rai kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuzingatia misingi ya Katiba na sheria zilizopo katika kutekeleza majukumu yao. 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinafuatilia kwa ukaribu tukio hili na kinatoa wito kwa vyombo vya dola kuendele kuchunguza na kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanatuhumiwa kwa mauaji haya. 

Kituo pia kinatoa wito kwa uongozi wa Mkoa wa Singida na Wilaya ya Ikungi kuwahakikishia wananchi wa Itigi usalama wa maisha na mali zao na  na kuhakikisha haki ya kuishi inalindwa kwa mujibu wa sheria za nchi. 

 

Imetolewa Jumanne February 05 2019 na,

Paul Mikongoti

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji