TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA

Posted 2 years ago by admin

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) tunapenda kuwataarifu, wanachama wetu, mashirika rafiki, serikali, wadau wa maendeleo, wanahabari na umma kwa ujumla juu ya maamuzi ya kufunga ofisi na kufanya kazi kutoka nyumbani kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za nchi na ulimwengu mzima za kukabiliana na mlipuko wa Virusi vya Corona (COVID-19). Ikumbukwe kwamba punde baada ya kupata taarifa kutoka kwa mamlaka husika kuhusu mlipuko wa COVID-19 nchini Tanzania, LHRC tulichukua hatua za haraka kukabiliana na hatari ya maambukizi kwa timu yetu pamoja na wadau wetu. Baadhi ya hatua za haraka tulizochukua ni pamoja na kusitisha kazi zinazohusisha mikusanyiko ikiwemo mikutano, mafunzo na huduma za moja kwa moja za msaada wa kisheria. Katika ofisi zetu nne tumefuata maelekezo ya namna ya kujikinga na kudhibiti maambukizi ikiwemo kudumisha usafi wa ofisi, kutumia sanitizers, sambamba na kudumisha utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka misongamano kama ilivyoelekezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.

Hata hivyo, tumeendelea kufuatilia kwa karibu muendelezo wa hali ya maambukizi kwa mujibu wa taarifa rasmi za serikali na mashirika ya kimataifa na tumefikia maamuzi ya kufanya kazi kutoka nyumbani kama sehemu ya kupunguza uwezekano wa timu yetu kuambukizwa au kusababisha maambukizi. Maamuzi haya yatatekelezwa kuanzia Machi 30, 2020 mpaka Aprili 14, 2020; na maamuzi haya yatahusisha ofisi zetu zote nne yaani Ofisi ya Makao Makuu Kijitonyama (Dar es Salaam), Kituo cha Msaada wa Kisheria Kinondoni, Ofisi ya Arusha na Ofisi ya Dodoma.

Kwa upande wetu kufanya kazi kutoka nyumbani inamaanisha kwamba tunaepuka mwingiliano wa mara kwa mara kama invyoshauriwa kitaalamu. Tunaahidi kuendelea kuwahudumia wananchi na wadau wetu kupitia majukwaa mbalimbali ya digitali hivyo tunawasihi wananchi na wadau kutumia barua pepe, mawasiliano ya simu, mitandao ya kijamii sambamba na Mfumo wa Kidigitali wa Kuripoti Matukio ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu – Haki Kiganjani kutufikia wakati wowote. Mfumo wa Haki Kiganjani unaweza kupatikana kupitia wavuti (https://hakikiganjani.humanrights.or.tz/sw/ripoti-tukio), SMS (0699 695 486) na kupitia Haki Kiganjani App inayopatikana kwenye simu yako ya Android.

Katika wakati huu ambapo sintofahamu juu ya maradhi ya Virusi vya Corona ikiendelea, tunawasihi wananchi na wadau wetu kuendelea kufuata maelekezo na taratibu za kujikinga kama zinavyotolewa na mamlaka. Endelea kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka, epuka misongamano na zaidi pata huduma ya daktari pale unapopata dalili za Virusi vya Corona.

Sisi LHRC tunaamini kwamba ‘Mtetezi wa Haki za Binadamu ni Bora pale anapokuwa Hai na mwenye Afya Njema’.

Imetolewa Machi 29, 2020 na;

Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji