Taarifa juu ya Kusitishwa kwa Leseni ya Kuchapisha na Kusambaza gazeti la Tanzania Daima

Taarifa juu ya Kusitishwa kwa Leseni ya Kuchapisha na Kusambaza gazeti la Tanzania Daima

Posted 2 years ago by admin

Tukio la Kusitishwa kwa Uchapishaji na Usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima ni Ishara nyingine ya Kuminywa kwa Uhuru wa Habari na Uhuru wa Kujieleza nchini Tanzania.

Mnamo Juni 23, 2020, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Idara ya Habari-Maelezo ilitangaza rasmi kufungia uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima ndani na nje ya Tanzania. Taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Tanzania Daima inadaiwa kurudia mara kwa mara kuchapisha habari za uongo, uchochezi na udhalilishaji dhidi ya Serikali mbali na maonyo kadhaa yaliyotolewa dhidi yao juu ya kuacha kitendo hicho kwani ni kwenda kinyume na Sheria Namba. 12 ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016.

Juni 9, 2020, Mahakama ya Afrika Masharika ilitoa uamuzi na kuitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua stahiki kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ili kuendana na Mkataba unaounda jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999 ambao Tanzania ni mwanachama. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania tangu mwaka 2016 baada ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari kutungwa na kuanza kutumika Tanzania, magazeti mengi yakiwemo Mwananchi,The Citizens, Mawio, Mseto, Tanzania Daima na Nipashe yamepata adhabu za mara kwa mara ikiwemo faini, kufungiwa na kufutiwa leseni ya uchapishaji na usambazaji wa taarifa mbalimbali.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinasikitishwa na matukio yanayoendelea kuminya Uhuru wa Kujieleza na Uhuru wa Habari Tanzania na kinapenda kutoa wito kwa Serikali kulinda na kutetea Uhuru wa Kujieleza na Uhuru wa Habari kwa kutekeleza hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Afrika Mashariki kwa kurekebisha vifungu vya sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari vinavyominya uhuru wa habari.

Imetolewa leo Juni, 24 2020 na;

 

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji