Siku ya Wanawake Duniani 2018: Tuimarishe Usawa wa Kijinsia

Siku ya Wanawake Duniani 2018: Tuimarishe Usawa wa Kijinsia

Posted 6 years ago

Machi 8 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kutambua nafasi na mchango wa wanawake katika kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa duniani.

Umoja wa Mataifa (UN) uliridhia na kuanza kuadhimisha rasmi Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 1975 kwa lengo la kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia. Uamuzi huu ulifikiwa kupingana na mfumo dume ambao ulitamalaki katika jamii mbalimbali ulimwenguni na kuminya haki za wanawake.

Katika maadhimisho ya siku hii muhimu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na jamii ya ulimwengu kutambua mchango wa wanawake katika kudumisha maendeleo endelevu. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinafanya juhudi kadha wa kadha kupambana na mitazamo hasi juu ya wanawake kwa kutoa elimu juu ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia kwa umma na kuwawezesha moja kwa moja wanawake kutekeleza majukumu yao kwa misingi ya haki na usawa.

Kwa mwaka huu (2018) Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimejipanga kutoa msaada wa kisheria maeneo mbalimbali ya Tanzania ambapo tayari kuanzia Machi 1, 2018 tumeanza jijini Arusha katika kata za Kaloleni, Elerai, Themi, Sakina na Olemoti. Kwa jiji la Dar es Salaam tutakuwa Wilaya ya Kigamboni, kata ya Somangila na Kibada kuanzia Machi 7 hadi 9, 2018 na katika wilaya ya Ilala kata ya Mnyamani na Kitunda kuanzia Machi 14 hadi 16, 2018.

Sambamba na hilo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeandaa warsha itakayowakutanisha wanawake nchini kujadili na kufanya tathmini ya haki za wanawake, mchango na nafasi ya wanawake nchini.

Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka 2018 ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini”.