
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari: Wito kwa Serikali kuondoa vikwazo kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari
Mei 3 kila mwaka jamii ya ulimwengu huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari tangu Umoja wa Mataifa ulipoidhinisha siku hiyo. Lengo la siku hiyo ni kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kuzikumbusha serikali umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza kama inavyolindwa katika Ibara ya 19 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa watu haki yao ya kupata na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia. Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni chachu katika kukuza misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora kwani husaidia raia na serikali zao kupokea na kutoa taarifa au maoni kuhusu mambo yanaoathiri maisha yao ya kila siku.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) tunaungana na jamii ya ulimwengu kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuikumbusha jamii na serikali umuhimu wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari. Pia, LHRC tunapenda kutumia fursa hii kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo kwa wadau na serikali kwa lengo kuu la kuboresha hali ya uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari. Katika maadhimisho ya mwaka huu (2020) kauli mbiu inasema “Uandishi wa Habari bila Woga wala Upendeleo”.
Kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu, LHRC tunapenda kufanya uchambuzi wa hali halisi kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu 2019 ambayo inaakisi matukio ya hivi karibuni yanayotishia na kudidimiza uhuru wa vyombo vya habari sambamba na haki ya kupata taarifa, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni. Mambo makuu yanayoathiri uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania ni pamoja na;
Uwepo wa Sheria Kandamizi kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari; Sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na ufurahiaji wa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania. Mwezi Machi 2019, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ilitoa hukumu yake kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, kufuatia kesi iliyofunguliwa na LHRC, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Katika hukumu hiyo, Mahakama ilithibitisha vifungu vya 7(3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j); vifungu vya 19,20 na 21; vifungu vya 35,36,37,38,39 na 40; vifungu vya 50 na 54; vifungu vya 52 na 53; na vifungu vya 58 na 59 kuwa vinakiuka haki ya uhuru wa kujieleza na Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sheria nyingine ambazo ziliendelea kuminya uhuru wa kujieleza kupitia baadhi ya vifungu vyake ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji Habari ya mwaka 2016, na Kanuni za Maudhui ya Mtandao. Sheria hizi zinajumuisha vifungu ambavyo havikidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Uwepo na utekelezaji wa sheria hizi uliendelea kuchangia upunguaji wa nafasi ya ushiriki wa wananchi kwa mwaka 2019.
Adhabu Kali kwa Vyombo vya Habari; Kwa mwaka 2019 pekee, LHRC imekusanya matukio mbalimbali ya vyombo vya habari kupewa adhabu ya kufungiwa na kulipa faini kwa madai ya kukiuka Kanuni za Maudhui ya Mtandao, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutoendana na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza. Vyombo hivyo vya habari ni Gazeti la The Citizen, na televisheni za mtandaoni za Kwanza Online TV, Watetezi TV na Ayo TV. Hivi karibuni tumeshuhudia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikisimamisha gazeti la Mwananchi Mtandaoni kutochapa habari kwa miezi sita.
Mara nyingi makossa yanayotumika kuvifungia na kuvipiga faini kubwa vyombo vya habari yamekuwa ni makossa ambayo yangeweza kurekebishwa na vyombo hivyo kuendelea na utendaji bila kufungiwa.
Ukamataji na Uwekaji Kizuizini wa Waandishi wa Habari kinyume na sheria; Matukio ya ukamataji wa waandishi wa habari kinyume na sheria kwa mwaka 2019 ni pamoja na tukio la ukamataji wa Erick Kabendera na Joseph Gandye. Kwa mujimu wa THRDC, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2019, matukio 13 zaidi ya ukamati wa waandishi wa habari kinyume na sheria yaliripotiwa. Matuki haya na mengine yamekuwa yakitishia waandishi wa habari hasa wanaoandika habari zinazoibua changamoto za mamlaka na kuita uwajibikaji wa serikali na viongozi wake.
LHRC tunaikumbusha Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwamba hali ya Uhuru wa Habari ya Tanzania imezidi kushuka katika nyanja za kimataifa ambapo mwaka 2019, Tanzania ilishuka kwa nafasi 25, kutoka nafasi ya 93 kwa mwaka 2018 hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019. LHRC tunaamini kwamba uhuru wa habari ni nyenzo muhimu ya maendeleo, demokrasia ya kweli na ulinzi wa haki za binadamu.
Wito kwa Serikali; LHRC tunaisihi Serikali na Bunge kuchukua hatua kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zote zinazokandamiza uhuru wa habari ili sheria na kanuni hizo ziendane na viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza.Pia, Serikali na vyombo vyake vinapaswa kuacha vitendo vinavyotishia uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari kwa ujumla na kuheshimu uhuru wa maoni. Serikali inapaswa kutoa ulinzi kwa wanahabari hasa wanaoandaa habari za kiuchunguzi ili kusaidia kuibua mambo yatakayowezesha kupambana na rushwa, ufisadi na umasikini.
Wito kwa Wanahabari na Vyombo vya Habari; LHRC tunavisihi vyombo vya habari na wanahabari kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hii kwa mwaka huu (2020) kwa kuhakikisha wanatoa habari bila woga wala upendeleo.
Wito kwa Watanzania; LHRC tunawasihi Watanzania kusimamia haki zao za msingi ikiwemo haki ya uhuru wa kupata taarifa na haki ya kutoa maoni kwa kupingana na vitendo vyote vinavyolenga kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
LHRC tunaamini kwamba uhuru wa habari ni nyenzo muhimu kwa uwajibikaji wa serikali na jamii kwa ujumla katika kufikia malengo ya maendeleo. Uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari ni muhimu zaidi katika kulinda afya ya jamii hususani katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugojwa wa COVID-19 hivyo ni muhimu kuendelea kulinda uhuru huo.
Imetolewa Mei 3, 2020 na;
Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji