SIKU YA KUPINGA AJIRA KWA WATOTO - Juni 12, 2019

SIKU YA KUPINGA AJIRA KWA WATOTO - Juni 12, 2019

Posted 3 years ago by admin

Siku ya Kupinga Ajira kwa Watoto inaadhimishwa tarehe 12 mwezi Juni kila mwaka. Ilianzishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002 kwa dhumuni la kutoa elimu na kufanya utetezi kuzuia ajira kwa watoto. Shirika la kazi kupitia Mkataba wa Kimataifa Na. 138, liliweka umri wa ajira kuwa miaka 15 na kuendelea na katika mkataba Na. 182 liliorodhesha ajira zisizokubalika kwa watoto na ambazo zinatakiwa kuzuiwa.

Siku hii inakutanisha makundi mbalimbali ikiwemo serikali, mamlaka za umma, mashirika binafsi na mashirika ya kimataifa ili kufanya utetezi juu ya ajira kwa watoto na jinsi ya kutatua tatizo hilo. Siku hii pia ilianzishwa kwa madhumuni ya kuangalia hali ya ajira kwa watoto, hatua za kuchukua na jinsi ya kuondoa tatizo hilo. Lengo namba 8.7 la maendeleo endelevu linaelekeza jamii kwa ujumla kuchukua hatua za lazima kukomesha ajira kwa watoto, kukomesha utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; na kuhakikisha kuwa ajira zisiziokubalika kwa watoto zinakomeshwa ikiwemo kuwatumia watoto kama wanajeshi na kuondoa kabisa ajira zisizokubalika kwa watoto kufikia mwaka 2025.

Ujumbe wa mwaka huu ni “watoto wasifanye kazi mashambani, bali wafanyie kazi ndoto zao” ikiwa na maana kuwa tuwaache watoto wakue, na kukuza ndoto zao kupitia njia mbalimbali ikiwemo elimu. Kuna jumla ya watoto 152 milioni wanafanyishwa kazi duniani kote na hawapati nafasi ya kuhudhuria shule, wengi wao wakitumikishwa katika sekta ya kilimo. Kuna aina nyingi za ajira kwa watoto ikiwemo watoto wanaofanya kazi mashambani na viwandani, watoto wanaotumika katika vita, watoto wanaolazimishwa kuwa ombaomba kwa maslahi ya watu wengine, na wengine huhusishwa katika aina mbaya zaidi za ajira kwa watoto kama kufanyishwa biashara za ngono, kushirikishwa katika biashara za madawa ya kulevya na kazi nyingine zisizofaa.

Nchini Tanzania, ajira nyingi za watoto ziko katika mifumo ya wafanyakazi wa ndani, wafanyakazi wa mashambani, ombaomba na wanaofanyishwa biashara za ngono. Ajira hizi zinaathiri sana watoto kwani wanashindwa kukua kiakili lakini pia wanashindwa kuhudhuria masomo. Sheria ya Mtoto, Namba 21 ya mwaka 2009 inatoa maana ya mtoto kuwa ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya 18. Pia inatoa ufafanuzi kuwa ukatili kwa watoto unajumuisha ajira kwa watoto ikiwemo ajira zinazowanyonya watoto.

Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mtoto kinaeleza kuwa mtoto hatahusishwa katika kazi yoyote ambayo inaweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake. Ni kosa la jinai kumuajiri mtoto katika kazi zisizofaa na zenye madhara kama ilivoelezwa na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini katika kifungu cha 5. Sheria hiyo pia imeweka umri wa ajira kuwa ni miaka 14. Hii inapingana na Mkataba namba 138 uliowekwa na Shirika la Kazi Duniani ambapo umri wa ajira umebainishwa kuwa ni miaka 15. Hata hivyo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inaeleza wazi kuwa mtoto ataajiriwa katika kazi zinazofaa ambazo sio ngumu na zisizo na madhara. Kazi hizo hazitakiwi kuathiri mahudhurio ya mtoto shuleni na haki nyingine. Lakini nchini Tanzania watoto wengi wanafanyishwa kazi na hawahudhurii shule.

Ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya elimu kwa wote bila ubaguzi, lakini watoto wengi wanaofanyishwa kazi na kushindwa kuhudhuria shuleni. Mtoto ambaye kamaliza shule ya msingi na ana umri wa miaka 14 na zaidi anaruhusiwa kufanya kazi lakini isizidi saa 6. Kinyume chake ni kuwa, watoto wengi hufanyishwa kazi zaidi ya muda huo na jamii haitambui kuwa wanavunja haki za msingi za watoto. Watoto wanatakiwa wapate pia muda wa kucheza na kushiriki na watoto wenzao kwa ajili ya ukuaji wao.

Japokuwa sheria ipo wazi, lakini watoto wengi hufanyishwa kazi ngumu na zisizofaa, tena katika umri ambao hauruhusiwi kisheria na mara nyingi zadi ya muda uliowekwa kisheria. Watu wengi hawaelewi ukubwa wa madhara ya ajira kwa watoto. Sababu nyingi za ajira kwa watoto ni pamoja na umasikini, kutokuwa na uelewa juu ya madhara ya ajira kwa watoto na hali hii inaathiri zaidi watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwani wanahitaji kufanya kazi ili waweze kukimu mahitaji yao na wengi wao hawahudhurii shule kabisa. Watoto wanaofanyishwa kazi wanapitia changamoto nyingi ikiwemo kukosa masomo, kupitia katika ukatili wa kingono na kimwili, kunyonywa kiuchumi, matatizo ya kiafya na athari zaidi katika ukuaji wao

  • Tunaomba jamii iwe mstari wa mbele kukomesha ajira kwa watoto wanaoajiriwa kama wafanyakazi wa ndani, mashambani, viwandani na wanaofanyishwa biashara za ngono.
  • Serikali ichukue jitihada binafsi na za ziada kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kuhudhuria shule na kuwasaidia katika mahitaji yao ya kila siku kwa kujenga mifumo bora ya kuwasaidia.
  • Serikali iwawajibishe kisheria watu wote wanaoajiri watoto na kuwafanyisha kazi ngumu na zisizofaa
  • Wazazi wahakikishe wanawatunza, kuwalinda na kuwajibika katika mahitaji ya watoto wao, kuhakikisha watoto wanahudhuria shule na wasiwachukulie watoto kama kitega uchumi cha familia kwa kuwafanyisha kazi ngumu, zisizofaa na zinazowaathiri.
  • Serikali ihakikishe inaweka umri wa ajira kuwa angalau miaka 15 na iwe kwa sababu maalumu

Watoto ni taifa la kesho, tunatakiwa tuhakikishe wanafanyia kazi NDOTO zao sio zetu

 

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu