Pongezi kwa Serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua dhidi ya ACACIA kwa tuhuma za uchafuzi wa mazingira 

Pongezi kwa Serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua dhidi ya ACACIA kwa tuhuma za uchafuzi wa mazingira 

Posted 4 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini ambapo mnamo Machi 6, 2019, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko alitoa onyo kwa kampuni ya uchimbaji madini ya ACACIA Mining Plc. kuchukua hatua kufuatia tuhuma dhidi ya kampuni hiyo kuchafua mazingira kwa kutiririsha maji yanayosadikiwa kuwa na sumu katika maeneo ya makazi ya watu yanayozunguka mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo, wilayani Tarime mkoani Mara. 

Kwa kipindi kirefu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimekuwa kikifuatilia na kutolea taarifa tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu zinazodaiwa kufanywa na kampuni ya ACACIA kwa wananchi kwa wanaoishi kuzunguka eneo la mgodi wa North Mara. Miongoni mwa tuhuma ni pamoja na mauaji yanayotekelezwa na askari polisi na walinzi wa mgodi, kupigwa na kuumizwa kwa wakazi, uchafuzi wa mazingira, waathirika wa shughuli za uchimbaji madini kukosa/kutopata fidia stahiki pamoja na ACACIA kutokushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa haki ipasavyo. 

Katika Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara  mwaka 2015 na mwaka 2017, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kiliripoti ukiukwaji huu wa haki unaodaiwa kufanywa na ACACIA. LHRC pia kwa kuungana na wadau kama RAID waliandika barua kwa ACACIA kuwataka kuutazama upya mfumo wao wa malalamiko (ACACIA Community Grievance Mechanism) ili kuhakikisha unaendana na kanuni za kimataifa za haki za binadamu na biashara. LHRC kwa kushirikiana na wadau pia iliandika barua kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kumsihi kuzingatia suala la ukiukwaji wa haki za binadamu linakuwa moja ya ajenda muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold Corporation ambao ni wamiliki wenye hisa kubwa katika kampuni ya ACACIA. 

Hata hivyo, kampuni ya ACACIA kupitia taarifa katika tovuti yake imekiri kutokea kwa tatizo hilo na  kuwa imeshalifanyia kazi na pia imeshaanza kutekeleza magizo ya serikali ili kudhibiti tuhuma za uchafuzi wa mazingira.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaisihi serikali kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya makampuni hasa makampuni ya uchimbaji wa madini ili kuhakikisha yanazingatia misingi ya haki za binadamu sambamba na matakwa ya utunzaji wa mazingira. LHRC inaisii Serikali kuhakikisha inasimaia maslahi ya wananchi wanaovunjiwa haki zao na makampuni kwa kuhakikisha wananchi wanapata nafuu ya kisheria ikiwemo fidia pale haki zao zinapovunjwa. LHRC itaendelea kuwa mdau wa serikali katika kuhakikisha shughuli za uwekezaji nchini Tanzania zinazingatia misingi ya haki za binadamu na kuwanufaisha watanzania kwa lengo la kufikia maono ya uchumi wa kati. 

Imetolewa na;

Felista Mauya 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji