Miaka 23 ya LHRC: Mafanikio na Changamoto katika Utetezi wa Haki za Binadamu
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika binafsi, huru la hiari, lisilo la kiserikali, lisilofungamana na mrengo wowote wa kisiasa na lisiolotengeneza faida kwa ajili ya kugawana, ambalo linataamali jamii yenye haki na usawa. Kituo kina lengo la kuwawezesha watanzania ili kuendeleza, kuimarisha na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilianzishwa mnamo Septemba 26, 1995 na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitivo cha sheria chini ya mradi wa TANLET na baadae kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Sura na 212 ya mwaka 2002 na kufuata matakwa ya Sheria ya Asasi Zisizo za Kiserikali ya mwaka 2002.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinafuraha ya kuadhimisha miaka 23 tangu kuanzishwa kwake katika kupigania na kutetea haki za binadamu kwa lengo la kufikia jamii yenye haki na usawa. Katika miaka 23 ya utetezi wa haki za binadamu Kituo kinajivunia mafanikio kadhaa ikiwemo; kuwajengea watanzania uwezo juu ya sheria na haki za binadamu, kuwajengea uwezo wasaidizi wa kisheria zaidi ya 900 katika wilaya 30 za Tanzania bara kwa lengo la kuwezesha ufikiwaji wa huduma za haki. Pia Kituo kimeanzisha mfumo wa uangalizi wa haki za binadamu katika wilaya zote nchini ikiwa na takribani wangalizi 169 waliopo mikoa yote nchini kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu.
Katika kipindi cha miaka 23 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimefanikiwa kutekeleza mambo yafuatayo;
- Kuanzisha kampeni kubwa ya uelewa wa mchakato wa katiba nchini uliyopelekea vuguvugu kubwa la watu kushiriki katika Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba mwaka 2014.
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kuwa msaada kwa wananchi wasio na uwezo wa kufikia huduma za haki kwa kutoa msaada wa kisheria kupitia kliniki za msaada wa kisheria Kinondoni na Arusha sambamba na huduma ya msaada wa kisheria ya kuhamahama. Pia kituo kimesimamia wateja katika kesi zenye maslahi ya umma mfano, kesi ya Biwater Gauff (T) Limited (City Water) ambapo kituo kilitoa msaada wa kiufundi kwa Serikali ilisaidia Serikali kutopoteza fedha katika mahakama ya usuluhushi wa migogoro ya uwekezaji.
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimekuwa chachu ya mabadiliko ya sera na kutungwa kwa sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2018, ambayo inawatambua wasaidizi wa kisheria waliojengewa uwezo.
- Kuratibu Mtandao wa Waangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TACCEO) na kutoa taarifa ya uangalizi wa uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo za marudio nchini.
- Kuibua mambo mbalimbali yaliyopelekea uwajibikaji katika ulinzi wa rasimili za nchi ikiwemo kupelekea kutungwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Rasilimali za Nchi ya mwaka 2017
- Kuanzisha vilabu 27 vya haki za binadamu katika shule za sekondari na vyuo vikuu nchini kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo kuhusu sheria na haki za binadamu.
- Kuendelea kuwa chanzo cha kutegemea cha taarifa za hali ya haki za binadamu nchini kupitia Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ambayo huandaliwa kila mwaka pamoja na Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara kwa mfululizo mzuri.
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kuwa msaada kwa wananchi wasio na uwezo wa kufikia huduma za haki kwa kutoa msaada wa kisheria kupitia kliniki za msaada wa kisheria Kinondoni sambamba na huduma ya msaada wa kisheria ya kuhamahama.
- Kituo kimekuwa kikifanya tafiti mbalimbali zenye tija kuhusiana na masaula ya kisheria na haki za binadamu na kutoa machapisho mbalimbali kwa lugha nyepesi kama sehemu ya kujengea jamii uelewa wa masuala hayo na kutumia tafiti hizo kufanya utetezi wa maboresho ya sera, sheria na mienendo.
- Kituo kimeweza kuendesha kesi mbalimbali za kimkakati kwa kushirikiana na wadau tofauti kwa ajili ya kubadilisha sheria na sera mfano kesi ya mgombea binafsi mbele ya Mahakama ya Afrika, kesi ya Takrima, kesi ya kura ya maoni ya katiba mpya, kesi ya kutetea watu wenye ulemavu, madai ya wananchi wa Serengeti (Nyamuma) mbele ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na nyinginezo.
Pamoja na mafanikio tajwa katika kipindi cha miaka 23 ya utetezi wa haki za binadamu, Kituo kimekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo changamoto ya rasilimali watu na rasilimali fedha ili kukidhi matarajio ya wananchi. Kitendo cha Serikali kutokuelewa kazi za LHRC au kukwaza kazi za Kituo kwa makusudi ni moja ya changamoto. Katika vipindi tofauti Serikali imekuwa ikitishia na hata kuingilia moja kwa moja utendaji wa Kituo.
Tukio la Jeshi la Polisi kuvamia kituo cha uangalizi wa uchaguzi na kuwakamata maafisa wa Kituo pamoja na vifaa ikiwemo simu na kompyuta 25 zilizokuwa zikitumika kupokea taarifa za uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 bila sababu ya msingi ni mfano wa namna Serikali inavyojaribu kuzima juhudi za LHRC za kuifikia jamii yenye haki na usawa.
Changamoto nyingine ni uelewa duni wa haki za binadamu miongoni mwa wananchi ambayo hupelekea kushindwa kutofautisha kazi za Kituo na shughuli za kisiasa au vyama vya siasa. Hii hupelekea wananchi kuamini propaganda zenye lengo la kudhoofisha juhudi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu za kufikia Tanzania inayoheshimu misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.
Kituo kinatoa wito kwa jamii, asasi za kiraia, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za serikali na wadau wa haki za binadamu nchini kuendelea kukuza na kulinda haki za binadamu nchini ili kufikia jamii yenye haki na usawa.
Imetolewa Septemba 26, 2018, na;
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu