MATUKIO YA ASKARI KUJIUA MFULULIZO: NINI CHANZO?

MATUKIO YA ASKARI KUJIUA MFULULIZO: NINI CHANZO?

Posted 4 years ago by admin

Katika kipindi cha wiki moja (Julai 9 -13, 2018) matukio 3 ya askari polisi kujiua yameripotiwa. Kiujumla Matukio ya watu kujiua yameendele kuwa moja ya mambo 10 yanayopelekea ukiukwaji wa Haki ya Kuishi Duniani. Sababu kuu ya askari hao kujiua inatajwa kuwa Msongo wa Mawazo (psychological stress) unaosababishwa na watu kushindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii kama mahusiano/ndoa, pamoja na changamoto za kiuchumi ikiwemo ugumu wa maisha. Matukio haya kwa jeshi la polisi yamekuwa ya kujirudia mara kwa mara.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watu laki 8 hadi milioni  1 hujiua kila mwaka kwasababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Kifungu cha 216 na 217: Kushawishi mtu Kujiua au Kujaribu Kujiua ni Kosa la Jinai. Kifungu cha 216 kinafafanua:

Mtu yeyote ambaye;

(a) anasababisha mtu mwingine ajiuwe; au (b) anamshauri mtu mwingine ajiuwe na akamshawishi kufanya hivyo; au (c) anamsaidia mtu mwingine ajiuwe, atakuwa anatenda kosa na atahukumiwa kifungo cha maisha.

Kujaribu kujiua, kifungu cha 217 kinafafanua: Mtu yeyote anayejaribu kujiua ana hatia ya kosa.

WITO KWA JESHI LA POLISI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuboresha mazingira ya kazi ya maafisa wa jeshi hilo ili kuwaepushia msongo wa mawazo unaoweza kutokana na ugumu wa maisha na mazingira ya kazi.

WITO KWA WANANCHI

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinawashauri wananchi kujitahidi kuepukana na vitendo vinavyopelekea msongo wa mawazo na kuchukua hatua stahiki za utatuzi wa migogoro kijamii na kisheria.

#HakiYaKuishi ni haki ya kwanza na ya msingi zaidi kwa binadamu, tuilinde.