Maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho katika Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2018

Maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho katika Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2018

Posted 4 years ago

1) Mamlaka yaliyopitiliza anayopewa Msajili wa Vyama vya Siasa kwenye masuala ya ndani ya chama
Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2018 unabadilisha jukumu la msingi la Msajili wa vyama vya siasa kutoka kuwa “msajili” mpaka kuwa “mdhibiti”. Mamlaka makubwa anayopewa Msajili katika Mswada huu yanafanya utekelezaji wa majukumu yake kwenda kinyume na misingi ya demokrasia na Katiba. Mswada unampatia Msajili mamlaka makubwa ya kudai taarifa – orodha ya wanachama, taarifa ya fedha ya chama, na “taarifa yoyote itakayohitajika.” Zaidi, ikiwemo mamlaka ya kuingilia masuala ya ndani ya uongozi wa chama, kama orodha ya wanachama, kuweka vikwazo kwenye katiba za vyama, na masuala ya kinidhamu ya ndani ya chama.

Kwa kuzingatia kuwa msajili anateuliwa na (na anaweza kuondolewa na) Rais, ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala, hii inaleta mgongano wa kimaslahi. Msajili hapaswi kuwa na mamlaka kwenye masuala yanayohusiana na taarifa nyeti au mchakato wa kufanya maamuzi ndani ya chama, kazi yake ijikite katika kanuni za usajili wa chama.

Mapendekezo

 • Ili kuepuka mgongano wa maslahi, Msajili anapaswa kuandaa miongozo kwa vyama vya siasa kusimaia shughuli zake za utendaji bila yeye (Msajili) kuingilia. Kifungu cha 4 (5)(e) kinapaswa kubadilishwa kumuondolea Msajili mamlaka ya kuingilia mapato na matumizi ya rasilimali za vyama vya siasa badala yake aandae miongozo itakayowezesha vyama kujisimamia na kuwajibika bila yeye kuingilia.
 • Rekebisha kifungu cha 5B kumuondolea mamlaka Msajili kuomba taarifa kwa viongozi au wanachama wa vyama vya siasa badala yake aombe taarifa kwa vyama kama taasisi sambamba na kufuata mapendekezo katika kutekeleza adhabu hizi:
 • Kumuondelea kinga ya kushtakiwa Msajili na maafisa wote katika ofisi ya Msajili kama ilivyopendekezwa katika kifungu cha 6.
 • Mamlaka ya Msajili yajikite katika (a) kusajili chama (b) kusajili viongozi wa kitaifa wa vyama na kutoa adhabu kwa kuzingatia mapendekezo haya:
 • Msajili anaweza kushauri vyama kubadilisha katiba zao lakini si kuvilazimisha. Utoaji wa adhabu unapaswa kufuata mchakato ulioanishwa.
 • Taarifa za vyama zinazoiwasilishwa kwa Msajili bila kuvunja sheria nyingine au haki za kikatiba. Adhabu zitolewe kwa kuzingatia mapendekezo haya:
 • Kinga zote zinazotolewa katika kifungu 19(2) na 19(3) cha Sheria ya sasa zijumuishwe kwenye kifungu cha 19A
 • Ondoa mabadiliko 22(a) na (b)
 • Vyama vya siasa vifanyiwe ukaguzi wa mapato na matumizi kwa mwaka na maamuzi yoyote ya kusitisha fedha zao za ruzuku yafanyike kwa kuzingatia ushahidi na yapendekezwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
 • Ondoa kabisa kifungu cha 21E kinachopendekezwa.

2) Mabadiliko yazingatie kuwa sheria haijengi hofu au kupendekeza adhabu kali

Kwa kiasi kikubwa Mswada unafanya marejeo kwenye adhabu, hii inajitokeza karibu kwenye marekebisho yote. Suaal hili linajenga hali ya hofu wakati mtu anaposoma muswada, kwamba upo uwezekano wa kufanya kosa fulani.

Vilevile, adhabu zilizowekwa kwa makosa mengi hasa makosa ya kiutendaji hazilandani na makosa. Hazizingatii misingi ya kisheria, hususani misingi ya sheria za utawala na makosa ya kanuni za adhabu.

Ingawa vyama vya siasa vinapaswa kudhibitiwa, lakini vilevile, katika demokrasia changa, vinahitaji kulelewa. Kuanzisha mchakato wa kutoa maonyo, adhabu kali na kutokuoneshwa wazi utofauti uliopo kati ya makosa binafsi na makosa ya taasisi ni suala la kutazamwa kwa umakini.

Mapendekezo

 • Makosa ya jinai yasirudiwe katika Sheria hii kwani tayari yapo kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
 • Ondoa marejeo yoyote ya adhabu kutoka kwenye sehemu kuu ya maelezo ya sheria na zielezewe kwenye kifungu cha nyongeza kwenye sheria na kuitwa: Makosa na Adhabu. Ama weka mchakato ulioelezewa hapo chini kwenye kila kifungu ukielezea kosa na adhabu husika. Hii ikihusisha vifungu 5A(4)(6); 5B(2)(3)(5); 8C(3)(4), 8D(4); 8E(3); 12C(4); 19A(3); 21D(1)(2)(3)(4).
 • Makosa ya kiutendaji, kama yalivyoainishwa katika sheria hii yanapaswa kufuata mchakato huu:

- Kwa kiwango cha chini, majibu yanatakiwa kutolewa baada ya barua tatu za onyo kutumwa.

- Kama hakuna majibu yaliyopokelewa au hatua iliyochukuliwa kurekebisha kosa, chama ama taasisi inaweza kutozwa faini ambayo inayoendana na uhalisia. 

- Kusimamishwa kwa muda, iwapo yafuatayo yamefikiwa: notisi ya maandishi ya

kutaka kukisimamisha chama ikiwemo maelezo ya kutosha kuhusu kosa lililofanyika, na nakala za barua zilizoandikwa na Msajili kukipa chama taarifa kuhusu makosa yake. 

- Kufuta usajili iwapo makosa yameendelea kutendeka baada ya kipindi cha kusimamishwa kwisha, au pale inapotokea kutoridhishwa na majibu ya suala lililosababisha kusimamishwa. 
- Uamuzi wa Msajili kufuta usajili wa chama uhusishe Baraza la Vyama vya Siasa na kuwepo na uwezo wa kukata rufaa mahakamani. 

3) Kukandamizwa kwa haki ya uhuru wa kujieleza 
Marekebisho yaliyoainishwa kwenye Mswada yamegusa maeneo matatu yanayoingilia haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza . 
Kwanza kuna katazo jipya kwa vyama vinavyofanya kazi kama vikundi vya uhamasishaji au vikundi vya harakati, vikundi hivyo vinaelezwa kuwa ni “vikundi vinavyoshawishi mitazamo ya wananchi au matendo ya serikali.” Kazi hizo ni msingi muhimu wa kazi za chama chochote cha siasa na hazipaswi kuzuiwa. 
Pili, muswada umeainisha kuwa ni kosa kwa chama “kutoa kauli ambazo si za kweli” Kimsingi kifungu hiki kinatishia demokrasia na haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza kwani ni ngumu kuainisha upi ni ukweli na upi ni uongo hasa katika masuala yenye utata hasa inapotokea mvutano wa kimtazamo au itikadi za kisiasa. Vifungu kama hivi pia vinaweza kusababisha kukosekana kwa usawa katika utekelezaji wa sheria. 
Tatu, Mswada unampa malaka Msajili kuruhusu au kutokuruhusu elimu ya uraia na shughuli za kuvijengea vyama vya siasa uwezo. 

Mapendekezo 

 • Katika kifungu cha 3(a)(5)(g), Msajili anaweza kutoa miongozo ya utoaji elimu ya uraia kwa vyama vya siasa lakini si kusimamia.
 • Ondoa uwezekano wa Msajili kuzuia shughuli za kuvijengea uwezo vyama vya siasa, badala yake anaweza kutoa ushauri au kuweka miongozo. 
 • Ondoa (7) kutoka Kifungu cha 6A na hariri (6) kuruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli za kuhamasisha umma na kushawishi utendaji wa serikali
 • Kuweka wazi kuwa kipengele 21D(2) kinahusika tu na kauli zinazotolewa kwa Msajili 
 • Kurejesha hitaji la vyama kuchapisha rejesta kwenye kipengele cha 8C(3). 

4) Vikwazo pale vyama vinapotaka kuungana na kushirikiana 
Marekebisho yamekuja na kanuni kwenye eneo ambalo hapo awali halikuwa limefafanuliwa kwa kina na sheria iliyoko ya Vyama Vya Siasa – suala la vyama kuungana na kushirikiana. Katazo hili jipya linasema kuwa vyama vitaruhusiwa kuungana “ndani ya siku 21 kabla ya kupendekezwa kwa wagombea wa uchaguzi mkuu” – kikwazo ambacho kinaweza kusababisha vyama vishindwe kuungana. Zaidi, na muhimu mno, Sheria inampa mamlaka waziri kutengeneza kanuni za kusimamia kuungana kwa vyama – huu ni mgongano wa wazi wa kimaslahi ukizingatia kazi ya waziri kwenye chama cha siasa. 

Mapendekezo 

 • Sheria mpya iruhusu vyama vya siasa kuungana muda wowote kabla ya kampeni kuanza na iondoe takwa la Waziri kutengeneza kanuni zitakazosimamia muunganiko wa vyama. Izingatiwe pia Sheria iliyopo imeweka muda wowote.

5. Marekebisho ya sheria yametumia vifungu na maneno yasiyo na maana ya moja kwa moja ambayo kisheria yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja hivyo kuruhusu maamuzi yasiyo na usawa.
Baadhi ya vifungu katika sheria hii vinampa Msajili mamlaka ya kufanya maamuzi yenye madhara makubwa kwa vyama kwa kufuata kile “anachokiamini” au kwa “kutoridhishwa" na jambo fulani.

Mapendekezo

 • Vifungu na maneno yoyote yenye utata na yanayoweza kutoa mianya ya maamuzi yasiyo na usawa yatolewe maana au kuondolewa kabisa katika sheria.