Maadhimisho ya 19 ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Adhabu ya Kifo

Maadhimisho ya 19 ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Adhabu ya Kifo

Posted 3 years ago

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinaungana na wadau wa haki za binadamu katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Kupinga Adhabu ya Kifo. Kila tarehe 10 ya mwezi wa 10 dunia hufanya maadhimisho ya kupinga adhabu ya kifo. Kwa mwaka huu itakuwa ni maadhimisho wa 19 ikiwa na kauli mbiu ya mwaka huu “Wanawake waliyohukumiwa kunyongwa ukweli uliyofichika”.

Mtandao wa Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani (World Coalition against Death Penalty) ambao LHRC ni mwanachama umeona ni muhimu maadhimisho ya mwaka huu kuangalia zaidi wanawake waliyohukumiwa adhabu ya kifo na madhila ambayo yanatokea kwa familia zao kama vile, kuvunjika kwa familia pamoja na watoto kukosa malezi na huduma muhimu za kijamii.

Adhabu ya kifo ni adhabu ya lazima kwa Tanzania inayotolewa kwa mtu aliyehukumiwa na Mahakama Kuu kwa kosa la mauaji ambapo mtu hunyongwa hadi kufa kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 197.

Haki ya kuishi imeanishwa katika ibara ya 1 ya Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, pia ibara ya 6(1) ya Mkataba wa Umoja wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) imeanisha haki ya kuishi, Ibara ya 4 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu inaweka haki ya kuishi na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inaweka haki ya kuishi kwa kila mtu.

Nchini Tanzania, Mahakama Kuu iliwahi kutoa maamuzi juu ya adhabu ya kifo katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Mbushuu Dominick Mnyaraje na mwenzake kwa kusema kwamba, adhabu ya kifo adhabu isiyo ya kibinadamu, ya kikatili, na ya kudhalilisha na utekelezaji wake unakiuka misingi ya haki za binadamu lakini uamuzi huu ulitenguliwa na Mahakama ya Rufaa.

Mwaka 1992 Ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali; ilitoa mapendekezo ya kufanya marekebisho ya sheria ili kuondoa adhabu ya kifo kwa kuwa ni ya kikoloni na isiyo ya kibinadamu. Pamoja na mapendekezo hayo hadi sasa mapendekezo hayo hayajafanyiwa kazi.

Nchini Tanzania, wakati wa uongozi wa awamu ya tano (5) ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Hayati Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli wafungwa wote wa hukumu ya kifo walisamehewa na Rais na adhabu yao ilibadilishwa kutoka adhabu ya kifo hadi kifungo cha maisha na hii ilikuwa ishara ya vitendo kuwa rais alikuwa haungi mkono adhabu ya kifo.

Ni wazi kwamba, uwepo wa adhabu hii haufanyi watu waogope kutenda makosa badala yake inaongeza maumivu kwa jamii. Adhabu ya kifo haimfanyi mtendaji kujutia na kurekebisha tabia yake, hivyo ni sahihi kusema kwamba adhabu haifanyi watu wabaya kuwa wazuri katika jamii, kuna uwezekano mkubwa wa makosa yanayoadhibiwa na adhabu hii kuendelea siku hadi siku.

Kwa upande mwingine adhabu ya kifo sio adhabu tu bali ni kitendo ambacho huharibu kabisa maisha ya mwanadamu ambayo hayawezi kurejelewa hata pale itakapogundulika ilitekelezwa kwa makosa.

Ni wakati muafaka sasa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta adhabu ya kifo kwa kuwa nchi ni ya kidemokrasia na inayofuata misingi ya Haki za Binadamu. Pia, historia ya adhabu hii unamizizi ya kikoloni ambayo kimsingi ilikuwa ni ya kinyonyaji, uonevu na ukatili.

Tunatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho ya sheria ya Kanuni ya Adhabu ili kuondoa vifungu vinavyoweka adhabu ya kifo ili kulinda haki ya kuishi kwa kuweka adhabu mbadala. Pia, kuridhia Mkataba wa Nyongeza ya Pili ya Hiari ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Kiraia na Kisiasa.

Imetolewa na;

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Bi. Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji