Kuipongeza serikali kwa kuruhusu wanafunzi walioachishwa shule kwa sababu ya mimba kurudi shule

Kuipongeza serikali kwa kuruhusu wanafunzi walioachishwa shule kwa sababu ya mimba kurudi shule

Posted 2 years ago

Mimba za utotoni ni pale mtoto wa kike wa kuanzia umri wa miaka 10 hadi 19 anapopata ujauzito na kujifungua. Mara nyingi kundi la umri huu huwa shuleni katika ngazi ya msingi au sekondari. Kulingana na taarifa za shirika la Afya Duniani takribani wasichana 14 hadi 15 milioni hupata ujauzito katika umri mdogo, hali hii huwadumbukiza wasichana wengi katika wimbi la umasikini na kupoteza ndoto zao hasa za elimu. Kwaa taarifa ya BEST ya mwaka 2020 takribani wasichana 4000 waliacha shule kwa sababu ya ujauzito na kupelekea ndoto za wasichana hawa kupotea lakini taifa kupoteza nguvu kazi amabyo ingesaidia kupeleka gurudumu la maaendeleo mbele.

Sababu zinazopelekea watoto wengi wa kike kupata ujauzito katika umri mdogo ni pamoja na ukosefu wa elimu hasa ya afya ya uzazi, umasikini, kutokuwa na usawa wa kijinsia, ndoa za utotoni Pamoja, ubakaji na ukatili wa kingono.

Kwa muda mrefu sana wanafunzi wa kike waliokuwa wakipata ujauzito Tanzania Bara hawakuruhusiwa kurudi shule na kuendelea na masomo yao. Tanzania Bara haijawahi kuwa na mwongozo au sera inayoweza kuruhusu watoto wa kike kurudi shule na hivyo kufanya ndoto zao na maendeleo yao kielimu kuteketea.

Bunge la Tanzania mnamo mwaka 2016 lilipitisha marekebisho katika sheria ya elimu ambayo yalilenga kumlinda mtoto wa kike aliyeko shuleni dhidi ya mahusiano ya kimapenzi ambayo hupelekea mimba na madhara mengine. Pamoja na sheria hii kutoa adhabu kali kwa watu wanaogundulika kuhusika na mapenzi na wanafunzi bado mtoto wa kike ambaye ni mhanga wa kuonewa amekuwa akifukuzwa shule na hivyo kusababisha mhanga pia kupewa adhabu kitu ambacho hakikuwa sawa.

Kutokana na Tanzania kutokuwa na sera maalumu ya kuwarudisha watoto wa kike shuleni wasichana wengi wamepoteza nafasi zao za kuendelea na masomo yao. Japo Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha elimu, bado suala hili limekuwa kikwazo kikubwa katika kuhakikisha elimu kwa wote bila ubaguzi.

Kwa kuona hili Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirkiana na shirika la kimataifa Centre for Reproductive Rights mwaka 2019 tulifungua shauri mbele ya African Committee of Expert on the Rights and Welfare of the Child (ACERWC) kupinga ukiukwaji huu wa haki za mtoto wa kike. Shauri hili lilisikilizwa tarehe 22 Novemba 2021 na sasa linasubiria hukumu.

Hata hivyo, kabla ya hukumu kutoka tarehe 24 mwezi Novemba 2021, Waziri wa Elimu Mhe. Joyce Ndalichako alitoa tamko kuwa sasa wanafunzi wote walioacha shule hata kwa sababu ya ujauzito wataweza kurudi shule katika mfumo rasmi, tamko hili lilifuatiwa na waraka namba 2 ambao utatumika katika kuwarejesha wasichana hao shuleni.

Hii ni hatua kubwa kwa serikali, jamii na kwa wasichana ambao kwa muda mrefu wamekosa haki zao za elimu kwa sababu ya kutokuwa na mfumo wa kuwaruhusu kurudi shule katika mfumo rasmi.

Tunaiomba serikali pia kubadili sheria ya ndoa na kuruhusu umri wa ndoa kuwa miaka 18 kwani ndoa za utotoni pia zimekuwa zikichangia sana mimba za utotoni na kusababisha wasichana wengi kuwa wazazi katika umri mdogo.

Tunaiomba pia serikali kuhakikisha wanatengeneza mwongozo utakaosaidia kutekeleza waraka namba 02 wa mwaka 2021 wa kuruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali kurejeshwa shuleni. Hii itasaidia kuhakikisha wanafunzi hawa hawabaguliwi, kutengwa na pia kuwezeshwa kuhudumia watoto wao ambao wanaweza kuwa wamejifungua. Pia mwongozo huu ueleze pale mtoto wa kike anapopata ujauzito ni huduma gani shule inatakiwa kutoa na kumsaidia kuweza kuendelea na masomo bila kuathrika.

Tunaipongeza serikali kwa hatua hii kubwa na ya muhimu.

Imetolewa leo Tarehe 25/11/2021 na;

Kituo cha heria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji

Download