KUHUSU MAKALA YA GAZETI LA UHURU KUICHAFUA LHRC

KUHUSU MAKALA YA GAZETI LA UHURU KUICHAFUA LHRC

Posted 7 years ago

KUHUSU MAKALA YA GAZETI LA UHURU KUICHAFUA LHRC

Leo tarehe 1/2/2017 katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la Uhuru limeandika habari yenye kichwa cha habari kinachosomeka”Sweden na Norway Zainyima fedha LHRC”.

Habari kwenye gazeti hilo linalomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) zinadai kuwa wafadhili wamefanya hivyo kutokana na ubadhirifu uliosababisha mpaka wajumbe watatu wa bodi kujiuzulu. Pia imedai kuwa wafanyakazi wa LHRC hawajalipwa mishahara yao na wameombwa kujitolea. Taarifa hiyo imedai kwamba kwa miaka mitatu kumekuwa na madai ndani ya shirika yakimtaka ajiuzulu kwa vile anamkingia kifua Mkurugenzi wa Fedha ambaye ni chanzo cha matatizo yote.

Taarifa hii haitokani na gazeti la Uhuru pekee kwani wiki iliyopita (Mkurugenzi Mtendaji) alipokea simu kutoka kwa mwandishi wa Gazeti la Nipashe aliyehitaji maelezo kwenye masuala hayo hayo na kupata ufafanuzi kuwa hayakuwa na ukweli. Mwandishi wa gazeti la Uhuru pia alimpigia Mkurugenzi Mtendaji jana (31/1/2017) na kupewa ufafanuzi na kumwambia kuwa taarifa hizo si sahihi. Hata hivyo ameamua kuendelea kuandika na kuweka majibu aliyopata kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa uchache sana hasa sehemu ya mwisho ya taarifa tofauti na mwandishi mwenzake wa Nipashe ambaye hakufanya hivyo.

Maoni ya LHRC katika hili ni kuwa mwandishi wa habari hii hana nia njema kwani alishaelekezwa kupata ufafanuzi zaidi ubalozi wa Sweden na Norway na pia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC endapo alifikiri taarifa walizopewa hazikuwa sahihi. Kibaya ni kuwa hakufanya hivyo na badala yake habari ikasambazwa kupitia ukurasa wa kwanza na kusomwa na magazeti takribani yote na runinga ambazo huwa zinatoa taarifa za magazetini.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji amewasiliana na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Uhuru na kumuuliza sababu za kuchapisha habari za uongo ambazo tayari alishazitolea ufafanuzi na akasema atajaribu kuzisahihisha. Ni dhahiri kwamba habari hii imetolewa kwa makusudi na tumelipelekea gazeti hilo hati ya kisheria ya madai kuhoji sababu za kufanya hivyo na kuwataka wasafishe jina la Kituo ama la hatua za kisheria zitachukuliwa.

Dkt. Helen Kijo-Bisimba

Mkurugenzi Mtendaji