Barua ya Wazi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kuhusu Utekelezaji wa Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali

Barua ya Wazi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kuhusu Utekelezaji wa Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali

Posted 3 years ago by admin

Mheshimiwa Waziri Mkuu

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikai, lisilotengeneza faida, lisilofungamana na itikadi yoyote ya kisiasa wala dini linaloshughulika na utetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania kupitia utoaji wa msaada wa kisheria, utafiti na ufuatiliaji wa haki za binadamu.

Awali ya yote, Kituo kinapenda kukupongeza sana kwa kazi nzito na nzuri ya kuwaletea watanzania maendeleo, ni ukweli kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaridhishwa sana na juhudi zako katika kuwajibisha watu na makundi mbalimbali kwenye masuala ya maadili.

Kwa kutambua kuwa kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Waziri Mkuu ni Kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeamua kukuandikia barua ya wazi kuhusiana na masuala kadha yanayotokana na Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Pamoja na mambo mengine, barua hi inalenga kuishauri Ofisi yako kama kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.

52.-(1) Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. (2) Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, anatambulika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Ibara ya 143, kama mtu pekee mwenye jukumu la kufanya ukaguzi wa hesabu za Serikali na mashirika ya umma na kuishauri serikali namna bora ya kuondokana na changamoto zinazojitokeza. Kwa nafasi yake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anasimama kama nguzo ya kudumisha uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,

Utakuwa unatambua mvutano uliopo kati ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa maoni yetu, bila kuathiri taratibu zozote za haki, kibunge na kiutendaji; Kituo kinaaminii kwamba, mvutano huu si wenye manufaa wala na tija Nchini. Kitendo cha Bunge kufikia uamuzi wa kujitenga na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Assad kunaleta sintofahamu kwa watetezi wa haki za binadamu husani katika suala la uwajibikaji na utawala bora. Katika hili, tunaamini kwamba kwakuwa Waziri Mkuu ndiyo Mtendaji Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni ni vema kuishauri Serikali kupitia Baraza la Mawaziri na Bunge kupitia vikao rasmi vya Bunge, kutengua maamuzi yake ya kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kuondoa mgogoro wa Kikatiba unaotengenezwa, pamoja na kulinda dhana ya uwajibikaji wa maslahi ya Taifa. Mvutano huu pia unalenga kudhoofisha juhudi za mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli za kupambana na ubadhirifu serikalini.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,

Mbali ya mgogoro uliopo kati ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuna jambo la msingi ambalo linapaswa kufanyiwa kazi chini ya usimamizi wako. Ni wazi kwamba, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hutoa ripoti zake kila mwaka zikiambatana na mapendekezo kwa Serikali juu ya namna sahihi ya kuondokana na matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ufanisi wa taasisi za Serikali. Aidha, kumekuwa na kulegalega kwa utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na Mkaguzi Mkuu kwa miaka mbalimbali.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo zinategemewa kututazamisha tulikotoka na tuendako, hazipewi uzito zinayostahili hususani katika kutekeleza mapendekezo yanayotolewa. Mathalani, mnamo April 8, 2019, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Juma Assad, ametoa taarifa yake ya mwaka wa fedha 2017/2018 unaoishia tarehe 30 Juni 2018 ambapo imeonesha kwamba, kwa mwaka 2016/2017, kati ya mapendekezo 4,108 ni mapendekezo 1,543 yaliyofanyiwa kazi sawa na asilimia 38% ya utekelezaji. Kwa mwaka 2017/2018, kati ya mapendekezo 4,282 ni mapendekezo 1,459 yaliyofanyiwa kazi sawa na asilimia 34% ya utekelezaji.

Ni wazi kuwa kwa ulinganifu wa utekelezaji wa mapendekezo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa miaka miwili ya ukaguzi unaonesha kushuka kwa asilimia 4% ya utekelezaji wa mapendekezo yake. Hali hii ni tishio dhidi ya uwajibikaji wa taasisi za serikali husani katika kuhakikisha mipango na matumizi halali ya fedha za umma kama ilivyopitishwa katika Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Waziri Mkuu,

Kwa hali hii, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunatoa mapendekezo yafuatayo:

  1. Ofisi yako iwahimize wakuu wa Wizara na taasisi za Serikali zilizotajwa ndani ya ripoti hii na za nyuma kutekeleza mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ili kuongeza uwajibikaji wa fedha za umma.
  2. Ofisi yako ifanye jitihada za makusudi kusukuma uwajibikaji wa matumizi ya fedha kulingana na mapendekezo ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  3. Ofisi yako itoe wito na agizo la kuwachukulia hatua za kinidhamu, kiutawala ama za kijinai watu wote waliyohusika katika matumizi ya fedha yaliyo kinyume na viwango vya ukaguzi kwa mujibu wa sheria za nchi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.
  4. Kuendelea kuhimiza ushirikiano baina ya Wizara, taasisi za Serikali na mashirika ya umma kuendelea kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kuongeza uwajibikaji na kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

 

Kwa kutambua kuwa barua hii ni ya wazi kwako, Kituo kinatoa rai kwa vyombo vingine vitavyoiona barua hii kuhakikisha kwa nafasi ya kila mmoja kuchochea uwajibikaji wa fedha za umma, ikiwemo kuchukua hatua za mahususi kwa mamlaka ya kila mmoja kulingana na sheria husika.

 

Wako katika kujenga Jamii yenye Haki na Usawa,

 

Bi. Anna Henga (Wakili)

Mkurugenzi Mtendaji

Aprili 18, 2019