Anna Henga kutunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Duniani 

Anna Henga kutunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Duniani 

Posted 4 years ago

Machi 6, 2019 Dar es Salaam 

Mwanaharakati mashuhuri na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga amepata heshima ya kutajwa kama miongoni mwa wanawake 10 watakaotunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri (mwenye uthubutu) Duniani (International Women of Courage Award), 2019, tuzo inayoandaliwa na Ikulu ya Marekani chini ya Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo.

Kwa mujibu wa taarifa katika tovuti ya Ikulu ya Marekani, Bw. Pompeo atawatunuku tuzo wanawake 10 waliofanya mambo kwa ujasiri/uthubutu zaidi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao. Hafla ya utoaji tuzo itafanyika Machi 7, 2019 saa 4:00 Asubuhi kwa saa za Washington DC sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Dar es Salaam na Mke wa Rais wa Marekani Bi. Melania Trump atakuwa mgeni wa heshima. 

Bi. Anna Henga ametajwa kama moja ya wanawake watakaotunukiwa tuzo hiyo kufuatia juhudi zake katika utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania. Wanawake wengine tisa watakaotunukiwa tuzo hiyo wanatoka katika mataifa yafuatayo; Bangladesh, Burma, Djibouti, Egypt, Jordan, Ireland, Montenegro, Peru na Sri Lanka.

Hafla ya utoaji tuzo itakuwa wazi kwa vyombo vya habari na itarushwa moja kwa moja kupitia tovuti ya ikulu ya Marekani www.state.gov

Pia itakuwa moja kwa moja kupitia mtandao wa Twitter @humanrightstz na @StateDept kupita kiunzi cha #WomenofCourage na #MwanamkeJasiri 

Tuzo ya International Women of Courage ilianzishwa mwaka 2007 kutambua mchango wa wanawake wanaojitoa kwa nguvu na ujasiri kama viongozi katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao bila kujali hatari ya maisha yao binafsi. Mpaka sasa, kupitia tuzo ya IWOC, Ikulu ya Marekani imetambua mchango wa wanawake zaidi ya 120 kutoka nchi zaidi ya 65 katika kutetea haki za binadamu, kudumisha afasi ya wanawake katika jamii na kudumisha amani na utawala bora katika nchi zao. 

 

Kwa ufafanuzi na maswali wasiliana na;

Michael Mallya - Afisa Mahusiano na Umma na Mawasiliano 

Baruapepe: mallya@humanrights.or.tz 

Simu: +255789147255