
Wanaharakati, wanahabari kudumisha utetezi wa haki za kiraia na kisiasa
Wadau wa vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za binadamu wamekutana Februari 14, 2018 katika ofisi za Makao Makuu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kujadili namna bora ya kutatua ongezeko la ukandamizwaji wa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya haki za kiraia na kisiasa.
Mkutano huo umewakutanisha wawakilishi kutoka asasi mbalimbali ikiwemo Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), TWAWEZA, Mfuko wa Wanawake Tanzania, Policy Forum, WiLDAF, Umoja wa Vyama vya Siasa (TCD), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRAGG), TGNP, pamoja na wadau wa vyombo vya habari kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF. Washiriki wamekubaliana kudumisha ushirikiano katika kushawishi Serikali kufanya maboresho kisheria na kiutendaji ili kulinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika kwa lengo la kudumisha ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa taifa.
Kupitia kikao hicho, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetambulisha mradi mpya ambao unalenga kuongeza uelewa wa wananchi juu ya sheria zinazosimamia masuala ya habari na mawasiliano sambamba na kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya kiraia na kisiasa.