
Utambulisho: Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Aloys Henga
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinayofuraha kuutangazia umma wa watanzania na marafiki wa haki kote ulimwenguni uteuzi wa Bi. Anna Henga (Wakili) kuwa Mkurugenzi Mtendaji akichukua nafasi ya Dkt. Helen Kijo-Bisimba ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Uteuzi wa Bi. Anna Henga umehalalishwa na mchakato wa ndani ya shirika uliosimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ya LHRC na kuanzia Julai 1 mwaka huu 2018 ataanza rasmi kazi hiyo.
Wasifu wa Anna Henga
Bi. Anna Henga kwa sasa ni Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Kabla ya kuteuliwa kuchukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji Anna amepata nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa Uongozi kwa kukaimu nafasi hiyo mara kadhaa wakati Mkurugenzi Mtendaji akiwa hayupo.
Anna alijiunga rasmi na LHRC mwaka 2006 akiwa katika programu ya mafunzo kwa vitendo na baadaye akapata nafasi ya kuwa afisa sheria wa kujitolea katika Kituo cha Msaada wa Kisheria Arusha na baadae kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Afisa Sheria Dawati la Jinsia, Mratibu wa PROGRAMU YA MAREKEBISHO YA KaATIBA na pia Mratibu wa Shirika la Msaada wa Sheria Kusini mwa Afrika (SALAN).
Anna Henga amehitimu Shahada ya Uzamili kuhusu Sera za Maendeleo na Utawala wa Asasi za Kiraia (Chuo Kikuu cha Mzumbe), Stashahada ya Usimamizi wa Biashara (Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM), Shahada ya Sheria (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) sambamba na Stashahada ya Masuala ya Jinsia (Chuo cha Sweden Institute of Public Administration).
LHRC imevutiwa na umahiri na kujituma kwake katika kutetea na kulinda haki za binadamu na tunafurahi kumpata Anna kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya. Tunawaomba watanzania na marafiki wa haki kote ulimwenguni kumuunga mkono Bi. Anna na LHRC kwa ujumla katika kuendeleza ulinzi wa haki za binadamu.
Chini ya uongozi wa Bi. Anna Henga tuna imani kuwa ndoto yetu ya kufikia Jamii yenye Haki na Usawa itakuwa kweli.
Mawasiliano
Bi. Anna Henga anapatikana kwa mawasiliano yafuatayo:
Barua pepe: ahenga@humanrights.or.tz
Twita: @HengaAnna