
UKEKETAJI WAENDELEA KUWA TISHIO LA MAISHA YA MTOTO WA KIKE TANZANIA
UKEKETAJI WAENDELEA KUWA TISHIO LA MAISHA YA MTOTO WA KIKE TANZANIA
Imeandaliwa na Kituo cha sheria na Haki za Binadam
Utangulizi
Kila ifikapo Februari 6 kituo cha sheria na haki za binadam kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia, tunaungana na Jamii ya kimataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji kwa wasichana na wanawake.Kwa miaka mingi ukeketaji kwa wanawake umekuwa moja kati ya aina ya ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa wanawake kwa baadhi ya jamii zinazoamini katika mila na desturi zilizopitwa na wakati.Kwa faida ya wale wasiofahamu ukeketaji ni kitendo kinachohusisha kukata au kuondoa sehemu ya uke wa msichana au mwanamke.Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya Afya na Malaria Tanzania wa Mwaka 2015/2016, (Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey TDH-MIS 2015-2016) ni kwamba mikoa ya Mara, Arusha, Dodoma,Manyara na Singida ndio inayoongoza kwa ukeketaji wa wanawake nchini Tanzania.
Tukiangazia mkoa wa Mara ukeketaji hushamiri sana hasa katika kipindi cha mwisho wa mwaka. Kwa mujibu wa mashuhuda ambao ni wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoani Mara, watoto wa kike hukeketwa kwa njia ya kikatili na isiyosalama kwa kipindi cha mwezi wa 12 kwa kuwa wasichana hawa wanakuwa wako katika likizo yao ya masomo ya mwisho wa mwaka. Nchini Tanzania ukeketaji ni kinyume na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na pia ni kinyume na Mkataba wa Kimataifa wa kupinga aina yoyote ya Ubaguzi dhidi ya Wanawake/Au Maputo protocal wa mwaka 1981.Ingawa sheria inakataza ukeketaji na wadau wengine kukemea vikali vitendo vya ukeketaji lakini bado wenyeji wa mkoa wa Mara wanaendelea kukeketa wasichana mchana kweupe huku wakishangilia kwa nyimbo na ngoma za kitamaduni barabarani.
Mathalani vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike vimekithiri sana mwishoni mwa mwaka 2020 kwasababu kwa mujibu wa mila na desturi za wenyeji wa mkoa wa Mara, zoezi la ukeketaji linatakiwa kutekelezwa kwa miaka inayogawanyika kwa mbili wakiamini kuwa, endapo watakiuka utaratibu huu watapata mkosi.Kukithiri kwa vitendo vya ukeketaji wa wasichana mkoani Mara kumesababisha kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaokimbia familia zao na kutafuta hifadhi katika nyumba salama zilizoanzishwa na wadau wakupinga ukatili dhidi ya watoto Mkoani Mara.
Mchichana ambaye jina lake limefichwa mwenye umri wa miaka 16 kutoka wilaya ya Butiama Mkoani Mara, yeye alikeketwa baada ya kushindwa kujiokoa dhidi ya ukeketaji.Baada ya kukeketwa Winifrida alifanikiwa kukimbia na kujiokoa dhidi ya ndoa za utotoni.
“Baba alinilazimisha mimi na dada yangu tukeketwe akasema kwamba tusipokeketwa atatuuwa,Akatukeketa! na alipotukeketa akampeleka dada yangu shule akaniacha mimi,Akaniambia kwamba ‘wewe nataka unipe Mahari.Mwaka 2019 wachumba wakaanza kuja, akanichagulia mume akasema, “Wini sasa nataka uolewe ili nipate Mahari”.Nikasema baba mimi sitaki Mimi ni mdogo, akasema kwamba “sitaki kusikia upuuzi wako na utaolewa kwa lazima ng’ombe 11 hizo siwezi kuziacha”.Nikatoroka nyumbani nikalala na kushinda njaa siku mbili Mama kurwa alikuja usiku saa 10 akaniokoa akanileta shirika la hope”
Wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia ambao ni Shirika la Hope for girls and women in Tanzania (HGWT) pamoja na Association for Termination of female genital mutilation (ATFGM) kwa kushirikiana na serikali wameanzisha nyumba salama Tatu katika wilaya za Serengeti, Butiama na Tarime kwa dhumuni la kusaidia wasichana waliokimbia familia zao kwa kuhofia ukeketaji.
Kwa mwaka 2020 kituo cha kuhifadhi watoto kilichopo wilayani Tarime cha ATFGM Masanga kwa mwezi disemba pekeake walipokea jumla ya wasichana 438 waliokimbia familia zao kwa kuhofia kukeketwa pamoja na ndoa za Utotoni.Kila mtoto wa kike aliyewasili katika kituo cha kulea watoto waliokimbia ukeketaji kilichopo Masanga ametumia mbinu na jitihada za kipekee kufika kituoni, baadhi yao walilazimika kutoroka usiku wa manene ili kujiokoa dhidi ya ukeketaji.
Msichana ambaye jina lake limefichwa mwenye umri wa miaka 14 kutoka katika wilaya ya Rorya Mkoani Mara alitoroka Nyumbani kwao usiku baada ya wazazi wake kushirikiana na kutaka akeketwe.Msichana huyu alifanikiwa kujiokoa baada ya kupata msaada wa karibu alipopiga namba 116 ambayo ni maalum kwa ajili ya kutoa msaada kwa wasichana walioko katika hatari ya kukeketwa.
“Wazazi wangu walishirikiana na kutaka kunikeketa, nilivyogundua wanataka kunikeketa nilitegeshea baada ya kula chakula cha usiku nikatoka nje kama vile naenda kukojoa nikapitiliza hukohuko, nikaenda huko porini na kulala huko huko,nilivyoamka asubuhi nikakutana na mwanamke mmoja aliyekuwa amekwenda kuchanja kuni akaniuliza “wewe mbona uko huku”? Nikamwambia nimekimbia ukeketaji, huyo mama naye alikuwa ameshaelimika,akapiga simu gari la Shirika la Hope likanifata kule kijijini kwetu”
Shirika la Hope for girls and Women in Tanzania (HGWT) lenye makao yake makuu katika kata ya Mugumu wilayani Serengeti wao walipokea jumla ya wasichana 198 kwa mwezi disemba ambapo inafanya jumla ya watoto waliokimbia familia zao kwa mwezi disemba Mkoani Mara kufikia 636.Hii ni idadi ya baadhi tuu ya watoto wa kike wenye ujasiri walioweza kujiokoa dhidi ya ukeketaji.Lakini kwa mujibu wa wadau wanaopinga ukeketaji waliopo Mkoani Mara wakiwemo wawakilishi wa kamati za MTAKUWWA wanaeleza kwamba viashiria vinaonyesha mamia ya watoto wa kike wamekeketwa kwa mwaka 2020 jambo ambalo linakwenda kinyume na maagizo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo jeshi la polisi dawati la jinsia mkoani Mara kwa muda mrefu wamekuwa wakiendesha operesheni maalum zinazoratibiwa mara kwa mara mahsusi kwa ajili ya kuokoa watoto wa kike dhidi ya ukeketaji.Kwa weledi mkubwa operesheni hizi zimekuwa zikifanywa kwa kushirikiana na wasamaria wema wanaotoa taarifa kwa wadau wakupinga ukeketaji baada ya kuona viashiria au maandalizi ya kukeketa wasichana katika vijiji vyao. Fatuma Mbwana ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Nyamwaga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia Tarime Rorya anaelezea namna wanavyopambana kutokomeza tatito hili.
“Sisi kama serikali tunapigana na tunatoa jasho sana kuhakikisha wasichana hawa tunawaokoa wasifanyiwe hivyo vitendo vya ukeketaji na Hapa mkoa huu wa Tarime Rorya tuna nyumba salama moja ambayo ni MASANGA na tunashirikiana kwa karibu na Asasi hiyo ya ATFGM MASANGA lakini pia na wadau wengine kuna asasi mbalimbali zilizoko kwenye hii kanda yetu kuna asasi kama sita hivi lakini pia tunashirikiana na wizara nyingine kuhakikisha tunamwokoa huyu mtoto wa kike , kama ustawi wa jamii na watu wa Hospital tunashirikiana nao kama serikali ili kuhakikisha huyu mtoto wa kike tunamuweka salama”
Kwa nini Watoto wa kike hukeketwa Tanzania?
Kwa mujibu wa wenyeji wa mikoa inayotekeleza ukeketaji kwa wanawake hasa mkoa wa Mara, zipo sababu kadha wa kadha zinazopelekea kukeketa wasichana. Kwanza wanajamii au wanafamilia wanaamini kuwa ili mtoto wa kike aweze kuvuka kutoka katika hautua ya kuwa msichana mdogo kwenda kwenye hatua ya kuwa mtu mzima au mwanamke kamili ni lazima akeketwe. Kwa bahati mbaya mila hii imekuwa ikichochea ndoa za utotoni kwani mara nyingi msichana akisha keketwa wanaume huanza kupeleka posa katika familia husika wakiamini kuwa tayari katika familia ile kuna binti aliye tayari kuolewa.Na kutokana na kuwepo kwa ndoa hizi za utotoni watoto wa kike mkoani mara wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi kama vile kupata elimu na kukosa uhuru wa kufurahia haki nyingine za watoto.
Elimu ni moja kati ya haki muhimu wanayonyimwa baadhi ya watoto wa kike mara tuu baada ya kukeketwa kwa kuwa mara nyingi watoto hawa hulazimishwa kuolewa baada ya kukeketwa.Hii imekuwa ni changamoto kubwa na ya muda mrefu inayohitaji ufumbuzi kwa kuwa baadhi ya watoto wa kike wanashindwa kutimiza malengo yao kwa kukosa elimu. Suzani Mwita ni msichana wa miaka 16 kutoka Serengeti Mkoani Mara, msichana huyu amejawa na matumani baada ya kukimbia ukeketaji na kufanikiwa kupata malezi bora pamoja na kupewa fursa ya elimu inayotolewa na shirika la hope girls and women in Tanzania lenye makao yake makuu wilayani Serengeti mkoani Mara.
“Kwanza nyumbani nilikuwa sisomi lakini katika kituo hiki nimepata huduma ya ufadhili wa elimu amapo nimesoma English Medium and primary Little flower,Na sasa hivi najua kingereza ambapo nilikuwa sijui naelewa vitu vingi na vikubwa ambavyo nilikuwa sielewi na sasaivi nimeelimika sio kama zamani na matarajio yangu mimi nina ndoto ya kuwa Rubani, kwasababu katika jamii yetu wanaelewa kwamba msichana hawezi kufanya vitu vikubwa katika jamii, kwahiyo rubani ni kitu kikubwa katika jamii na katika dunia nzima kwasababu, watu wanajua hivi hamna mwanamke anaweza kupaisha ndege kwahiyo nataka kuwa Rubani ili watu waelewe kuwa naweza, baba yangu na nduguzangu wote waelewe hivyo”
Sababu nyingine kubwa inayofanya wanajamii wa mikoa inayokeketa wasichana hasa mkoa wa Mara kukeketa watoto wakike ni uwepo wa Imani thabiti katika mila na utamaduni ikiwemo kutambikia mizimu ikiwa ni moja kati ya desturi za wazee wa mila ambapo wanamiini ukeketaji huondoa mikosi na balaa katika ukoo au familia husika.Vilevile kukosekana kwa kipato cha kutosha katika familia husika kumekuwa chanzo kwa wanajamii kuendeleza mila hii ya ukeketaji kwa wanawake na wasichana.Mara zote ifikapo msimu wa ukeketaji familia hupata fedha kupitia michango ya sherehe zinazoandaliwa kwa mchichana aliyekeketwa pamoja na zawadi mbalimbali ikiwemo fedha anazozawadiwa mchichana aliyekeketwa.Vilevile Ngariba anayekeketa wasichana hupata malipo ya fedha au malipo mengine yoyote kulingana na makubaliano au Mila na desturi za ukoo au familia husika.
Juhudi za kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto
Kwa mujibu wa mwongozo wa uratibu wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (mtakuwwa) 2017/18 – 2021/22 uliotolewa na Vizara ya Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto august 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekua ikifanya juhudi mbalimbali katika kukabiliana na vitendo vya ukatili nchini kupitia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Mipango ya kisekta. Baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na kuandaliwa kwa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), kupitishwa kwa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 na Kanuni zake, kuanzishwa Dawati la Jinsia kwenye Wizara zote, kuanzishwa kwa mifumo ya ulinzi wa mtoto katika Halmashauri 63 nchini, kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia na Watoto kwenye vituo vya polisi 417 na kuanzishwa kwa mahakama za kusimamia kesi za watoto katika Halmashauri 131. Pamoja na juhudi hizo kumekuwepo na changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji mdogo wa rasilimali fedha na watu, mfumo usio fungamanishi wa uratibu na kutokuwepo kwa mfumo thabiti wa upatikanaji wa taarifa na takwimu za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.Ifahamike kwamba mojawapo ya majukumu ya kamati za MTAKUWWA ni pamoja na Kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto na shughuli za utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi unaendana na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa ya haki na Ustawi wa Wanawake na Watoto pamoja na Sera, Sheria na Miongozo ya Serikali.
Serikali pamoja na wadau wakipanga na Wazee wa Mila wanapanga
Kwa kuwa athari za ukeketaji kwa wanawake na wasichana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 2000 imekuwa ikitekeleza mipango nane (8) ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwa ni jitihada za kuleta usawa katika Jamii. Mipango hiyo ni pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji Tanzania (2000-2015).Pia serikali ilianzisha Mpango Kazi wa Taifa wa Kuendesha Dawati la Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi; na Mpango Mkakati wa Utoaji wa Haki ya Kisheria kwa Watoto (2013-2017).Pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa na serikali lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa kikwazo kikubwa katika mapambano dhidi ya ukeketaji mkoani Mara. Amosi Chekushemeire ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa shirika la Hope for girls and women in Tanzania anaelezea namna wanasiasa wanavyokwamisha mapambano dhidhi ya ukeketaji mkoani Mara
“Msimamo wa serikali kwa ujumla ni wa kutuunga mkono kwasabau serikali ndio inayosimamia sharia na sharia ziko wazi kwamba serikali inapinga vitendo vya ukeketaji na unyanyasaji wa kijinsia na serikali imeunda dawati la jinsia, Lakini watu mmojammoja hususani wanasiasa ni watu wenye vinywa viwili, mkiwa nae anawaunga mkono kwasababu anajua kabisa serikali inapinga zile mila lakini hana ujasiri wa kuambatana na nyie na kutamka hadharani kwamba nalaani na nakemea na naunga mkono mapambano dhidi ya matukio haya hasa ya ukeketaji sasa hiyo ni changamoto kubwa sana kwasababu utakumbuka wanasiasa ni watu wanaoheshimika na kusikilizwa sana na jamii kwahiyo chinichini akikutana na wazee wa mila anaunga mkono ukeketaji”
Hata hivyo tangu kuanzishwa kwa mpango wa serikali wa kutokomeza Ukeketaji kwa wanawake wazee wa mila na desturi wamekuwa wakiendeleza mila hizi zilizopitwa na wakati ambazo mara nyingi zimekuwa na madhara makubwa kwa watoto wa kike.Wazee hawa wamekuwa wakitafuta njia mbadala za kuendelea kutekeleza Ukeketaji kwa wanawake mkoani Mara.Kwa sasa mbinu zinazotumika ni pamoja na kwanza; kubadilisha mavazi ambapo watoto wa kike wakisha keketwa huvalishwa mavazi ya kiume pamoja na kuvalishwa kofia za kiume kichwani ili wasijulikane kama ni wasichana.Pia mbinu ya kuwachanganya watoto wa kike na wa kiume katika misafara ya watoto wa kiume wanapokuwa wakitoka katika tohara.Vilevile kwa kipindi hiki wamekuwa wakibadilisha umri wa kukeketa wasichana ambapo zamani walikuwa wakikeketa wasichana wa mika 13 au 14 waliohitimu darasa la saba lakini kwa sasa mangariba hukeketa hata wasichana wadogo wenye umri wa kuanzia mika 6 au 7 yaani wanaoanza darasa la kwanza.Mbinu nyingine iliyotumika hasa kwa mwaka huu 2020 ambapo wanasiasa waliokuwa katika kampeni za uchaguzi mkuu walitamka kuunga mkono ukeketaji jambo lililochochea kwa kiasi kikubwa kuendelea kushamiri kwa Ukeketaji licha ya kuwa ni kosa kisheria.
Asasi za Kiraia zinavyopambana kutokomeza Ukeketaji Mkoani Mara.
Kwa takribani miaka 7 kituo cha sheria na Haki za Binadam (LHRC) kimekuwa mratibu wa Mtandao wa kupinga ukeketaji Tanzania na kwa kushirina na wadau wengine kama vile kamati za MTAKUWWA katika ngazi ya mkoa wa Mara wamekuwa wakiendesha shughuli mbalimbali za kutokomeza ukeketaji na kuokoa watoto dhidi ya Ukeketaji hasa katika kipindi cha mwezi desemba ambapo ukatili huu umekithiri.Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za Binadam (LHRC) Anna Aloyce Henga anaeleza madhara makubwa yanayowapata watoto wanaopitia ukeketaji mkoani Mara pamoja na Mikoa mingine inayotekeleza mila na desturi hii iliyopitwa na wakati.
‘Ukeketaji kwa watoto wa kike ni unyanyasaji mkubwa kwa watoto na huweza kupelekea kuvuja damu nyingi na majeraha makubwa, pia inasikitisha sana kuona wanajamii hasa wa mkoa wa Mara kuendeleza mila zilizopitwa na wakati ambazo mara nyingi husababisha maumivu makali na kuweza kupelekea vifo kwa watoto, Nawasihi sana kuachana na unyanyasaji huu mkubwa.Nakemea vitendo hivi vya ukeketaji kwa nguvu zote na nawasihi wandau pamoja na wanajamii kupinga vitendo hivi vya kikatili kwa watoto’’
Kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binadam inayotolewa na Kituo cha sheria na Haki za Binadam ya mwaka 2019, matukio ya ukatili wa kimwili yanaendelea kuwa changamoto katika ufurahiaji na utekelezaji wa haki za watoto kwa mwaka 2019.Ukatili wa kimwili dhidi ya watoto husababisha madhara makubwa kama vile kupelekea watoto kupata majeraha mbalimbali katika miili yao, yakiwemo majeraha ya kudumu, kupata ulemavu, na hata kufariki. Ripoti ya haki za binadamu imeonyesha pia kuwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2019, LHRC ilikusanya jumla ya matukio 26 ya ukatili dhidi ya watoto yaliyopelekea vifo vya watoto hao.
Shirika la Hope for girls and women in Tanzania yenye makao yake makuu mjini Mugumu wilaya ya Serengeti pamoja na nyumba salama iliyo katika wilaya ya Butiama wana dhumuni kubwa la kutokomeza Ukeketaji Mkoani Mara. Vilevile taasisi ya ATFGM –MASANGA ambayo ni Assosiation for Termination of female genital Mutilation zenye makao yake katika wilaya ya Tarime Mkoani Mara inafanya kazi bega kwa bega kwa kushirikiana na Jeshi la polisi dawati la jinsia kuendesha operesheni maalumu za kuokoa watoto pindi wapatapo taarifa za unyanyasaji wa watoto wa kike wanaokimbia ukeketaji na kuwapa hifadhi katika nyumba salama mpaka kipindi cha ukeketaji kitakapopita.Kazi kubwa inayofanywa na mashirika haya yasiyokuwa ya kiserikali ni pamoja na kutoa elimu ya jinsi ya kujiokoa pindi wanapokuwa katika hatari ya kukeketwa.Elimu hii hutolewa kwa kushirikiana na jeshi la polisi jinsia pamoja na waalimu wa shule husika ambapo zoezi hili limekuwa likifanikiwa sana kwa kuwa watoto wengi wamekuwa wakielewa na hivyo kupiga simu ya bure ambayo ni namba 116 na hivyo kuweza kuokolewa kwa wakati.
Ingawa kumekuwa na mambamabo ya waziwazi ya kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike nchini Tanzania lakini bado unyanyasaji huu umeendelea kushika hatamu mkoani Mara hasa katika wilaya ya Tarime.Kwa kuwa ukeketaji unasababisha madhara makubwa katika afya ya watoto wa kike kama vile kupoteza uhai, kuvuja damu nyingi pamoja na kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI.Hivyo ni vyema serikali kulitazama upya suala hili la Mila na Desturi hii kandamizi iliyopitwa na wakati kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika Idara ya Maendeleo ya Jamii ili kuepukana na Madhara makubwa yanayowakumba wanawake hasa watoto wa kike kutokana na Ukeketaji.
Hitimisho
Kwa hitimisha ni vyema ikafahamika kuwa ukeketaji ni unyanyasaji mkubwa kwa wanawake.Vilevile Ukeketaji kwa wanawake ni ukiukwaji mkubwa sana wa Haki za Binadam unaofanywa katika Jamii zinazoamini katika mila na desturi zilizopitwa na wakati.Laini ni vyema jamii ya Tanzania kufahamu kwamba mila na desturi inayoweza kusababisha watu kupoteza uhai wao hazifai katika Jamii, hivyo ni vyema serikali ikaelekeza upya nguvu nyingi na kuendelea kusimama kidete kukemea na kupinga ukeketaji kwa watoto wa kike.Mojawapo ya suluhisho la haraka litakaloweza kukomesha kabisa vitendo hivi ni pamoja na viongozi wa wa ngazi mbalimbali katika serikali kusimama hadharani na kukemea vikali vitendo hivi kwani vinarudisha nyumba maendeleo nchini Tanzania.Vilevile ni vyema wadau wa kupinga ukatili waendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara makubwa yanayowapata wanawake waliokeketwa.Katika suala la kutoa elimu kuhusiana na madhara ya ukeketaji ni vyema kuwashirikisha wanaume katika michakato mzima wa kupinga ukeketaji Tanzania.