UCHAMBUZI WA MAKADIRIO YA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI, 2021/2022 KWA MTAZAMO WA HAKI ZA BINADAMU

UCHAMBUZI WA MAKADIRIO YA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI, 2021/2022 KWA MTAZAMO WA HAKI ZA BINADAMU

Posted tokea miaka 3

UCHAMBUZI WA MAKADIRIO YA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI, 2021/2022 KWA MTAZAMO WA HAKI ZA BINADAMU

 

  1. Utangulizi

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefanya uchambuzi bajeti kufuatia wasilisho la Hotuba ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2021/2022 kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Mwigulu Lameck Nchemba mnamo tarehe 10 Juni, 2021 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lengo kuu la uchambuzi huu ni kutoa maoni ya LHRC katika mtazamo na maslahi ya haki za binadamu, pia kutoa tafsiri rahisi kwa wananchi kuhusu mapendekezo ya bajeti yatakayosaidia kuboresha bajeti hiyo kabla ya kupitishwa na Bunge.

Kipekee tunatoa pongezi kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa mapendekezo mbalimbali yanayolenga kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi kama vile; kuzingatia maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 9% hadi 8%, kufanya marekebisho ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi kupunguza kiwango cha mchango kutoka asilimia1.0% hadi 0.6%, pamoja na kuzingatia maslahi ya wakulima wa mbogamboga,

  1. Kuhusu sura ya bajeti:
  • Bajeti inapendekeza jumla ya shilingi trilioni 36.33 kukusanywa na kutumika.
  • Kati ya fedha hizo mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote.
  • Washirika wa Maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.96, sawa na asilimia 8.1 ya bajeti yote.
  1. Maoni ya LHRC kuhusu mapendekezo ya bajeti

Kwa mujibu wa Mh. Mwigulu Nchemba, mapendekezo ya bajeti yanalenga kurekebisha jumla ya sheria (19) pamoja na sheria nyingine kama ilivyoelezwa katika ukurasa 26 na 27 wa kitabu cha bajeti ya serikali, ikiwa na lengo la kufanya maboresho katika mfumo wa kodi kwa kupitia viwango vya kodi, tozo na ada.

Ni wazi kwamba, dhima la maboresho hayo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa vipaumbele vya taifa kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 pamoja na maeneo mahususi yaliyoelezwa na Mh. Waziri kama vile, kuboresha miundombinu ikiwemo barabara za mijini na vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini, afya na bima ya afya kwa wote, na elimu.

Hata hivyo, LHRC inapenda kutoa maoni yake katika mapendekezo ya marekebisho ya sheria hizo na masuala mengine kama ifuatavyo;

  1. COVID-19

Mbali na ukweli kwamba COVID -19 bado ipo bajeti ya serikali haijatenga fungu maalumu la kupambana na ugonjwa huu. Ugonjwa huu hautabiriki na kama tutashindwa kuonyesha kwenye bajeti namna ya kupambana nao kama hali ikibadilika itaathiri utekelezaji wa bajeti nzima.

  1. Sheria ya Petroli Sura, Na. 392

Mapendekezo ya kurekebisha sheria hii kwa kuongeza tozo ya mafuta ya taa kutoka shilingi 150 hadi 250 kwa lengo la kupunguza uchakachuaji wa mafuta si la manufaa kwa mwananchi wa kawaida ambaye anayetegemea mafuta ya taa kwa ajili ya shughuli za nyumbani na kiuchumi. Hivyo, tunapendekeza kwa Waziri wa Fedha na Mipango kutafuta namba mbadala ya kuweza kuzuia vitendo vya uchakachuaji wa mafuta, ikiwemo kuongeza udhibiti na ufuatiliaji bila kuongeza tozo kwenye mafuta ya taa. Pia tatizo la uchakachuaji tayari lina suluhisho lake kwani mafuta yanawekewa vinasaba. Ni kazi ya serikali kuongeza usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara kuliko kubebesha mwananchi mzigo huu bila sababu ya msingi.

  1. Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura Na. 438

Mapendekezo ya kufuta kifungu cha 92A ili kuipa mamlaka ya mahakama kukusanya mapato yanayotokana na adhabu na faini zinazolipwa mahakama badala kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) si pendekezo zuri. Ni muhimu kwa mahakama kubaki katika utekelezaji wa lengo lake kuu kama ilivyoainishwa katika ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 la kuwa chombo cha utoaji haki. Lengo ni kutoiongezea mahakama kazi nyingine ikizingatiwa kuwa hivi sasa bado mahakama ina jukumu kubwa linalohitaji nguvu zaidi katika suala la utoaji haki.

  1. Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kieletroniki, Sura Na. 306

Eneo hili limegawanyika katika sehemu mbili kama ifuatavyo;

  1. Kuhusu mapendekezo ya kutoza shilingi 10 hadi 10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa fedha utaongeza gharama kwa watumiaji wa mitandao wanaofanya miamala kwa njia ya simu. Aidha, inaweza kuchochea watumiaji hao kupunguza matumizi ya mitandao ya simu kama njia ya kufanya miamala kwa kukwepa gharama itakayotokana na tozo katika eno hili, badala yake ikarudisha na kuongeza idadi ya watu kutembea na fedha, jambo ambalo linaweza kuchochea kwa kasi vitendo vya uhalifu.

LHRC inapendekeza kuto toza eneo hili ili kuongeza hamasa ya watu kufanya biashara na shughuli nyingine za kifedha kwa njia ya simu ambayo ni rahisi na salama.

  1. Pia, mapendekezo ya kutoza kiasi cha shilingi 10 hadi 200 kwa siku kwa kila laini ya simu, yanaweka uwezekano wa ongezeko la gharama ya kufanya mawasiliano hususani kwa wananchi. Zaidi mapendekezo hayo yataleta madhara kwa wananchi kufikia haki ya kujieleza na haki ya kupata taarifa kama ilivyoainishwa katika ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Ikumbukwe kwamba, laini za simu ni nyenzo muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi ambapo watu hupata taarifa kwa kufanya mawasiliano ya kila siku. Jambo hili ni sawa na kuweka ada ya umiliki wa simu kwa siku. Pamoja na kuweka msamaha kwenye simu janja na vishkwambi kuweka tozo hii itachelewesha nchi kufikia lengo la kuwa na 80% ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46% ya sasa.

 

LHRC inapendekeza kutoweka tozo ya laini ya simu ili kupunguza gharama za mawasiliano nchini na urahisi wa kufanya mawasiliano.

 

  1. Sheria ya Usalama Barabarani, Sura Na.168

Pamoja na nia nzuri ya Serikali kupunguza kiasi cha faini kutoka shilingi elfu 30 hadi shilingi elfu 10 kwa Bodaboda kwa kurekebisha sheria hii, LHRC inatoa wito kwa Wizara kuongeza bajeti kwa kuweka programu maalum itakayolenga kutoa elimu ya usalama wa barabarani kwa kundi hili. Lengo ni kuhakikisha kuwa, watumiaji wa vyombo hivyo wanapata mafunzo ya mara kwa mara na ukaguzi endelevu wa vyombo vyao ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara. Ni ukweli kuwa waendesha bodaboda wamekuwa wavunjaji wakubwa wa sheria za barabarani bila kujali faini. Kuna shaka ya kuwa kpunguza faini kunaweza kuongeza uvunjaji wa sheria za barabarani zaidi kwenye kundi hili na kuzidi kuhatarisha usalama wa abiria na wananchi kwa ujumla.

  1. Kuanzisha tozo za umwagiliaji

Mapendekezo ya kutoza ada ya huduma ya umwagiliaji ya asilimia 5% ya mavuno ya msimu kwa eneo la vyama vya umwagiliaji yanaweza kurudisha nyuma ari ya uwekezaji katika eneo hili, wakulima kutofanya kilimo cha umwagiliaji kutokana na ongezeko la gharama ya kulipa ada ya asilimia 5% ya mavuno ya msimu. Hivyo, tunapendekeza Wazira ipitie upya mapendekezo hayo kwa kuangalia athari ya kuwa na tozo hiyo inayokwenda moja kwa moja kwenye mavuno ya msimu.

  1. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura Na. 148

LHRC inapongeza mapendekezo ya msamaha kwa Kodi ya Ongezeko kwa Taasisi zisizo za Kiserikali (NGO’s) kwenye bidhaa na huduma zinazotumika kwenye miradi, hata hivyo ni vema kwa Wizara kuweka usawa katika msamaha huo kwa kuangalia mashirika yote yanayonufaisha jamii, ni ukweli kwamba mashirika husajiliwa kwa lengo la kunufaisha jamii hivyo, ni vizuri kuwepo kwa vigezo sawa kwa wote na si yale yenye mikataba na Serikali pekee.

  1. Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura Na. 332

LHRC inapendekeza kutofanya marekebisho kwa kuruhusu msamaha wa kodi ya mapato, kuacha sheria hiyo ibaki kama ilivyo ili mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi yabaki chini ya ridhaa ya Baraza la Mawaziri na si kwa Waziri wa Fedha na Mipango peke yake. Lengo ni kuongeza dhana ya uwajibikaji wa pamoja, pia kuimarisha utendaji kazi wa kitaaisisi kati mambo yenye maslahi mapana kwa Taifa. Ni imani yetu kwamba, Baraza la Mawaziri ni chombo muhimu katika kufanya maamuzi ya mambo yanayohusu msamaha wa kodi hususani kwa miradi mikubwa.

  1. Hitimisho

Pamoja na tamko la kufuta tozo ya asilimia 6% ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu (Retention Fee) kwa wanufaika wa mkopo, hotuba ya bajeti haijaakisi tazamio la kufuta penalti ya asilimia 10% kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kama ilivyojadiliwa awali na Waziri wa elimu. Pia, mapendekezo ya ukusanyaji wa kodi kwa njia ya LUKU ni vema yakatafakariwa kwa upana, ni ukweli kwamba, kuna nyumba zina mita ya LUKU zaidi ya moja, na kuna nyumba ambazo hazitumii umeme wa TANESCO.

Mwisho kutokana na athari ya janga la COVID-19 ni muhimu kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Bunge kuendelea kufanya tahimini na kupunguza ada, kodi na tozo mbalimbali kwa katika sekta ya utalii na biashara ili kuvutia wawekezaji.

Tunaamini kwamba, maoni yetu yanaweza kusaidia Wizara pamoja na Bunge katika kujadili na kupitisha mapendekezo ya makadirio ya bajeti kwa mwaka 2021/2022 ili kulinda haki za wananchi.

 

 

Imetolewa leo Juni, 14 2021 na;

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

 

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji