Tamko: Ulinzi wa Haki za Watoto Katika Tuhuma za Makosa ya Jinai

Tamko: Ulinzi wa Haki za Watoto Katika Tuhuma za Makosa ya Jinai

Posted tokea miaka 4

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimesikitishwa na taarifa za tuhuma za wizi wa madawati 108 ya Shule ya Sekondari Sinoni, Arusha. Tukio hilo linapaswa kufanyiwa upelelezi wa kina ili kubaini na kuwafikisha watuhumiwa wote kwenye vyombo vya sheria.

Hata hivyo, LHRC ina mtazamo tofauti kuhusiana na utaratibu uliotumika kushughulika na watuhumiwa wa tukio hilo kama iliyoonekana katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari mnamo Disemba 16, 2020. Tamko hili limeainisha mambo makuu mawili kwa kuzingatia aina ya watuhumiwa waliohusishwa katika tukio hilo;

Utoaji wa Adhabu ya Viboko Mashuleni
Sheria ya Elimu Sura ya 353 inampa mamlaka waziri wa elimu kutunga kanuni za kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo. Mwaka 2002 Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilitoa Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko. Waraka huu unatoa muongozo wa namna ya kutoa adhabu ya viboko na kufafanua ni nani anapaswa kutoa adhabu hiyo kwa mwanafunzi. Waraka unaelekeza kwamba adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Waraka pia unasisitiza kwamba adhabu ya viboko itolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote na ni mwalimu mkuu pekee anayepaswa kutoa au kukasimisha mamlaka ya utoaji wa adhabu kwa mwalimu mwingine kwa maandishi. 

Mamlaka ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya hayahusishi kuadhibu wanafunzi. Hivyo, kitendo kilichofanywa na mkuu wa Wilaya ya Arusha, Bw. Kenani Kihongosi ni kinyume na utaratibu. 

Utaratibu wa uendeshaji wa makosa ya jinai 
Tuhuma walizotuhumiwa nazo wanafunzi ni tuhuma za jinai ambapo kwa mujibu wa sheria mtu yeyote anapotuhumiwa kwa kosa la jinai anapaswa kufikishwa mahakamani. Mahakama ndio chombo chenye mamlaka ya kutoa adhabu katika makosa ya jinai. Kitendo alichofanya mkuu wa Wilaya ya Arusha, Bw. Kenani Kihongosi ni kinyume na Katiba na sheria alizoapa kuzilinda. 

Wito kwa viongozi
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kinatoa wito kwa viongozi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni kwa mujibu wa viapo vyao wakati wanapotekeleza majukumu. Viongozi wanapaswa kusimamia utawala wa sheria ili kuhakikisha jamii inakuwa na amani na utulivu.