TAMKO LA KULAANI MAUAJI YA WANAWAKE NA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU

TAMKO LA KULAANI MAUAJI YA WANAWAKE NA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU

Posted tokea miaka 3

 

TAMKO LA KULAANI MAUAJI YA WANAWAKE NA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU

Mnamo tarehe 4/08/2021 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepokea kwa masikitiko mauaji ya kinyama yaliyofanyika katika mikoa ya Tabora na Tanga yaliyohusisha wanawake.

Katika tukio la Tabora, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 57 na mkazi wa kata ya Puge wilaya ya Nzega anadaiwa kuuawawa na kisha kuning’inizwa kwenye kamba ili aonekane amejinyonga. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, ACP Sophia Jongo, alisema tukio hilo lilitokea tarehe 4 Agosti 2021 katika Kijiji cha Isalalo tarafa ya Puge ambapo baba na mtoto wake walimuua mama huyo kwa madai ya kwamba walichoka kumuuguza na kutengeneza tukio hilo ili aonekane amejinyonga.

Katika tukio lingine wilayani Handeni mkoani Tanga imeripotiwa tukio la mwanamke mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa ni mjamzito wa miezi nane ambapo mumewe alimkatakata kwa mapanga huku sababu zikielezwa kuwa wivu wa mapenzi.

Vitendo hivi vya kinyama ni mwendelezo wa ukiukwaji wa haki za binadamu huku wanawake wakiwa wahanga wakubwa wa matukio hayo hapa nchini.

Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeainisha kuwa watu wote ni sawa na hakuna aliye juu ya sheria. Pia ibara ya 14 imeainisha haki ya kuishi na hifadhi ya maisha kutoka katika jamii.

Tanzania imetia saini mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Kupinga Aina Yoyote ya Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) pamoja na Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake wa Afrika (Maputo protocol) ambayo yote imetoa vifungu maalum vya kutetea na kulinda haki za wanawake.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufanya upelelezi na kuchukua hatua stahiki kwa wale wote waliohusika katika matukio hayo.

Imetolewa leo tarehe 07 Agosti 2021 na.

 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji