
Tamko Kupinga Adhabu za Kikatili Shuleni
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera aliyepoteza maisha kwa madai ya kuadhibiwa vikali na mwalimu kwa tuhuma za kuiba mkoba/pochi ya mwalimu. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vikali kitendo hicho ambacho ni mwendelezo wa adhabu za kikatili dhidi ya watoto shuleni, adhabu ambazo ni za kutweza na kinyume na haki za binadamu.
Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania 2017 inaonesha ongezeko la vitendo vya kikatili dhidi ya watoto na hii inadhihirishwa na ongezeko la vitendo vya kikatili vinavyotokea shuleni dhidi ya watoto. Katika kipindi cha karibuni, matukio kadhaa ya walimu kuwaadhibu wanafunzi hasa wa shule ya msingi kinyume na taratibu za utoaji adhabu mashuleni yameendelea kukithiri hali inayopekea uvunjifu wa haki. Taarifa za mwanafunzi wa darasa la nne (IV) katika Shule ya Msingi Kimamba huko wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kuadhibiwa vikali na kupelekea kupata athari za kimwili na kushindwa kuendelea na masomo ni moja ya matukio yaliyoripotiwa hivi karibuni.
Muundo wa Kisheria juu ya Adhabu Shuleni
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 13 (6)(e) inabainisha kwamba mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia misingi kwamba ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Ibara ya 14 ya katiba hiyo inaelezea haki ya kuishi ya kila mtu na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, chini ya kifungu cha 13 (1) inakataza mtu kumsababishia mtoto mateso, au aina nyingine ya ukatili au kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto. Kifungu kidogo cha (2) kinasema kwamba endapo adhabu ni mbaya au ni kubwa kwa kiwango cha mtoto kulingana na umri, hali ya kimwili, kiakili wake haitakuwa stahili kwa mtoto.
Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002` Kifungu cha 61(1)(v) kinampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakayokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo. Kupitia mamlaka hiyo, moja ya kanuni zilizotungwa ni The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N.294 ya mwaka 2002, zinazotoa mwongozo wa akutoa adhabu ya viboko, ikielezea wakati wa kutoa adhabu pamoja na kiwango cha adhabu hiyo kwa mwanafunzi. g Kanuni ya 3(1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote.
Sheria inamtaka Mwalimu Mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo. Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.
Kanuni ya 5 inataka kila adhabu ya viboko inapotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu. Na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na Mkuu wa shule.
Hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yao walimu hawazingatii kanuni hizi, hali hii imepelekea matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kujitokeza mara kadhaa na kupelekea wanafunzi kushindwa kufurahia haki ya elimu, kupata ulemavu na kupoteza maisha kama ilivyojitokeza kwa mwanafunzi aliyepoteza maisha huko Wilayani Bukoba. Ili kuondokana na adhabu za kikatili shuleni, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapendekeza mambo yafuatayo;
- Hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya walimu wanaotenda makosa ya jinai kwa wanafunzi ili kuwa fundisho kwa wengine.
- Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuona uwezekano wa kurejea kanuni za utoaji adhabu shuleni kwani mbali na uwepo wa idadi ya viboko, bado wanafunzi wamekuwa wakilalamikia baadhi ya walimu kuumiza wanafunzi kwa idadi hiyo ya viboko. Wizara izingatie kuweka mfumo mzuri wa wanafunzi kutoa malalamiko yao pale wanapofanyiwa kinyume na taratibu.
- Wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaamini kwamba shule inapaswa kuwa eneo salama zaidi kwa mwanafunzi ili aweze kufurahia haki yake ya msingi ya elimu. Endapo wanafunzi watawaogopa walimu kwa sababu ya adhabu za kikatili, inaweza kuchangia wanafunzi kutohudhuria shuleni na kuwakosesha watoto haki ya elimu. Serikali, jamii na kila mmoja atimize wajibu wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu ili kufikia Jamii yenye Haki na Usawa.
Imetolewa Agosti 29, 2018 na,
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji