TAMKO KULAANI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA HUSUSANI KITENDO ALICHOFANYIWA MSANII ZUWENA MOHAMED (SHILOLE)

TAMKO KULAANI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA HUSUSANI KITENDO ALICHOFANYIWA MSANII ZUWENA MOHAMED (SHILOLE)

Posted tokea miaka 4

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vikali kitendo anachodai kufanyiwa Bi. Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole cha kupigwa na mumewe, kujeruhiwa mwili na kusababishiwa maumivu makali kama alivyotoa taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram. Kumekuwa na vitendo vya kikatili vikiwemo vipigo, ubakaji, matusi na vingine vingi ambavyo wanakutana navyo wanawake kwenye mahusiano yao au ndoa na kupelekea maumivu makali kwao na mara nyingine kifo.

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ya mwaka 2019 inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ilitoa taarifa ya zaidi ya wanawake 80,000 wamefanyiwa ukatili kuanzia mwaka 2017, ukatili ambao ulipelekea vifo kwa baadhi ya wanawake hao.

Sheria kuhusu Ukatili wa Majumbani

Tanzania imetia saini Mkataba wa Kimataifa wa kupinga aina yoyote ya Ubaguzi dhidi ya Wanawake (Convention on the Elimination of all Forms of Discrimination against Women of 1979) pamoja na Mkataba wa Nyongeza wa Afrika wa Haki za Wanawake (Option Protocol to the African Charter on the Rights of Women in Africa or Maputo Protocol of 1981) ambapo mikataba yote miwili inaelezea umuhimu wa kulinda haki za wanawake. Mikataba hii pia inasimamia kupinga ukatili wa kijinsia hasa ukatili dhidi ya wanawake.

Kwa kuwa nchini Tanzania hakuna sheria mahsusi dhidi ya ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani, makosa mengi ya ukatili yapo katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu (The Penal Code Cap. 16). Kosa hili analodai kufanyiwa Shilole ni kinyume na kifungu cha 225 cha Sheria hiyo na adhabu yake ni kifungo cha miaka 7. Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 pia inakataza kufanya vitendo vya kikatili kwa mwenza wako lakini wanaume wamekuwa wakiendelea kuwafanyia wenza wao vitendo kama hivi.

Mapendekezo

  1. Kuongeza ufanisi katika kutambua ukatili wa kijinsia unaofanywa na wenza
  2. Kutoa taarifa pale unapoona unafanyiwa ukatili mapema iwezekanavyo na kuomba msaada kwa kupaza sauti
  3. Elimu kutolewa kwa jamii kuhusu Haki za Binadamu, haki za wanawake na ukatili wa kijinsia.
  4. Kuachana na mila potofu na imani zinazoathiri usawa wa kijinsia na kuwafanya wanawake kuonekana dhaifu
  5. Kuongeza madawati ya jinsia na kuongeza pia muda wa kuhudumia
  6. Kuimarisha vyombo vya haki kuweza kusimamia vitendo vya kikatili
  7. Kuwa na sheria maalumu kuhusu Ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani
  8. Wanawake kuacha kuvumilia ukatili wanaofanyiwa na wenza wao

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunampogeza tena Shilole kwa kupaza sauti yake na tunaamini ujasiri wake huo utawakomboa wanawake wengine.

TUNASIMAMA NA SHILOLE, TUNASIMAMA DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

Imetolewa na;

Anna Henga

Mkurugenzi Mtendaji