
Tamko Kulaani Mauaji ya Wanawake Wanne huko Misungwi, Mwanza
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani mauaji yaliyoripotiwa mkoani Mwanza katika wilaya ya Misungwi ambapo miili ya wanawake wanne wakazi wa vijiji vitatu tofauti ambavyo ni kijiji cha Isakamawe, Misasi na Mabuki imeokotwa Agosti 3, 2018. Kwa mujibu wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza mauaji hayo yanasadikika kuhusishwa na imani za kishirikina kwani miili ya wanawake hao imenyofolewa baadhi ya viungo ikiwemo viungo vya siri.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinalaani vikali ukiukwaji huo mkubwa wa haki ya kuishi. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa rai kwa wananchi kuheshimu na kulinda haki za binadamu hususani haki ya kuishi ambayo ni haki ya msingi zaidi kwa kila binadamu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinawahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha zoezi la kuwatia hatiani wote walioshiriki ukatili huo. Pia, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa rai kwa Serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama kwa wananchi ili kuepuka vitendo vya kikatili vinavyozidi kushamiri nchini.
Imetolewa Jumamosi Agosti 4, 2018 na;
Bi. Anna Henga (Wakili)
Mkurugenzi Mtendaji