
TAMKO: KUKEMEA VITENDO VYA VIONGOZI WANAOJICHUKULIA SHERIA MIKONONI KWA KUTOA VIPIGO KWA WANANCHI
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinampongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga kwa kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Hydom kata ya Hydom Bi. Adella Kente kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbulu kwa kumshambulia mwananchi kwa jina la Bi Rose Danielson siku ya tarehe 12/01/2021 katika Kijiji hicho kwa tuhuma ya kutolipa michango ya Kijiji.
Ni wazi kuwa, tabia ya viongozi katika ngazi mbalimbali kujichukulia sheria mikononi imeshamiri hususani vitendo vya vipigo kwa wananchi wenye tuhuma za makosa ya jinai. Hali inazidi kudidimiza ustawi wa haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora nchini kwa mujibu wa viwango vya kimataifa hususani Mkataba wa Haki za Kirai na Kisiasa,1966 na kitaifa kama ilivyowekwa katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,1977.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuchukua hatua za makusudi kudhibiti vitendo hivyo ikiwemo kukemea, kusimamisha, kutengua uteuzi wa viongozi wa aina hiyo pamoja hivyo mara moja pale ambapo matukio hayo yanapotokea. Tuhuma zozote za makosa ya jinai au madai zinapaswa kuwasilishwa katika vyombo vya kisheria.
Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inaweka haki ya kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Pia Katiba inaeleza wazi kuwa ni Mahakama pekee ndio chombo cha utoaji Haki. Viongozi na wananchi wana jukumu kubwa la kulinda amani ya nchi kwa kufuata sheria na Katiba waliyoapa kuilinda.
Imetolewa leo Januari 20, 2021; na
Anna Henga,
Mkurugenzi Mtendaji