
TAMKO KUKEMEA MAUAJI YA MAAFISA WA JESHI LA POLISI HUKO UVINZA,KIGOMA
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa maafisa watatu wa Jeshi la Polisi katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma. Katika taarifa hizo, mnamo Oktoba 16, 2018 Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka , wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma, Bwana Ramadhani Mdimi pamoja na askari wengine wawili waliuawa wakati wakitekeleza zoezi la kuwaondoa wananchi wanaosemakana kuvamia eno la ufugaji la Ranchi ya Taifa NARCO na kufanya shughuli za kilimo kinyume na sheria. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na familia za askari waliouawa.
Kufuatia tukio hilo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakemea vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kupelekea mauaji ambayo ni kinyume na haki ya msingi ya kuishi kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,1977. Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya maafisa wa jeshi la polisi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu; mnamo Oktoba 11, 2018 wanachi wa jamii ya wafugaji waliwashambulia na kuwaua askari wawili ambao walikuwa wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) katika hifadhi ya Ruaha iliyopo wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinawakumbusha wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kufuata taratibu za kisheria katika kudai haki zao. Kwa upande mwingine LHRC inawakumbusha maafisa wa Jeshi la Polisi kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu ili kuepusha migogoro baina ya Jeshi la Polisi na wananchi. LHRC pia inaikumbusha Serikali kutengeneza mpango madhubuti wa kutatua migororo ya ardhi inayoendelea kugharimu maisha ya watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.
Imetolewa Oktoba 23 na;
Bi. Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji