
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI: Uamuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kumrudisha Bungeni aliyekuwa Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe kupingwa Mahakamani
Bwana Paul Revocatus Kaunda, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Yustino Ndugai(MB), aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bwana Cecil David Mwambe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 10 ya mwaka 2020; Wakili Kaunda anaiomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika ya kumtambua Bwana Mwambe kama mbunge halali, ilhali Mwambe aliushautangazia umma wa watanzania ya kwamba amejivua uanachama wa chama chake cha CHADEMA na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), kauli ambayo iliungwa mkono na katibu mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliyempokea rasmi Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM, na Mwambe naye kumkabidhi Katibu Mkuu wake mpya kadi yake ya CHADEMA.
Wakili Kaunda amesema, kitendo cha Spika kumtambua Bwana Mwambe kama mbunge halali wakati Bwana Mwambe ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama mbunge wa jimbo la Ndanda (2015-2020), ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa kumrudisha bungeni mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.
Kesi hiyo ya kikatiba imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu litakaloongozwa na Mheshimiwa Jaji Issa Maige. Majaji wengine ni Mheshimiwa Jaji Stephen Kirimi Magoiga na Mheshimiwa Jaji Seif Kulita.
Wakili Kaunda, katika kesi hiyo, atawakilishwa na jopo la mawakili sita litakaloongozwa na wakili mwandamizi Mpale Kaba Mpoki akisaidiwa na mawakili Daimu Halfani, Fulgence Massawe, Prisca Chogero, Stephen Msechu pamoja na Stephen Ally Mwakibolwa.
#SimamiaHaki
Kwa Jamii yenye Haki na Usawa