
LHRC YASHINDA MAPINGAMIZI KATIKA KESI YA KUPINGA WAGOMBEA KUPITA BILA KUPINGWA
LHRC, katika kesi Miscellaneous Civil Cause No.19/2021, ilipeleka maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, ikiomba vifungu vya Sheria ya Uchaguzi Mkuu unaohusu wabunge, madiwani na Rais, pamoja na vifungu vya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vifungu ambavyo vinatoa mwanya kwa wagombea kutangazwa washindi bila kupigiwa kura na wananchi kuwa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kwakuwa inanyima haki ya wananchi kushiriki katika zoezi la uchaguzi.
Awali, kesi hiyo iliwekewa pingamizi moja na mawakili wa serikali ambapo pingamizi hilo lilikubaliwa kusikilizwa na Mahakama Kuu kwa njia ya maandishi. Baada ya pande zote kupeleka nyaraka zao mahakamani, Mheshimiwa Jaji, John Mgeta alifanya maamuzi yaliyosomwa mbele ya mawakili wa pande zote.
Jaji Mgeta amesema kwamba pingamizi hilo limekuja wakati usio wake, kwani kulifanyia kazi pingamizi hilo kutasababisha kwenda kwenye kiini cha kesi ya msingi, kinyume na utaratibu wa mapingamizi ya awali unavyotaka. Pingamizi hilo la serikali limetupiliwa mbali na kesi ya msingi itaendelea kuskilizwa.
Imetolewa na;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu