LHRC yakemea Ukiukwaji wa Demokrasia Tanzania

LHRC yakemea Ukiukwaji wa Demokrasia Tanzania

Posted tokea miaka 5

Jumatatu Julai 15, 2019

Dar es Salaam

Kituo cha Sheria na Haki za Biunadamu (LHRC) kimetoa tamko Julai 15, 2019 jijini Dar es Salaam kukemea ukiukwaji wa demokrasia unaofanywa na jeshi la polisi kwa kuvuruga mikutano ya wanasiasa hasa wapinzani. Tamko hilo limetolewa kufuatia matukio ya hivi karibuni ya kubughudhiwa na kuzuiwa kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano ya vyama ikiwemo tukio la hivi karibuni liliotokea Julai 13 huko mkoani Simiyu ambapo jeshi la polisi limetuhumiwa kuvamia na kusambaratisha mkutano wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAVICHA). Matukio mengine ni pamoja na jeshi la polisi mkoani Bukoba kumshikilia bila kumpa dhamana Mbunge Halima Mdee (CHADEMA) pamoja na kuzuia mkutano wa Mbunge John Heche jimboni kwake tarime huku mikutano ya Chama cha Mapinduzi ikiendelea bila bughudha.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga amesema kitendo hicho na vitendo vingine vya kuwabughudi na kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni kinyume na misingi ya demokrasia na haki za binadamu. Bi. Anna Henga amesema matukio hayo yanakiuka haki za msingi za kiraia na kisiasa kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa 1969.

“Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu sasa tangu kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 tumeshuhudia muendelezo wa ukandamizaji na ukiukwaji wa Haki za Kiraia na Kisiasa jambo ambalo ni kinyume na misingi ya haki za binadamu, demorasia na utawala bora kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,1977 na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.” Ameseama Anna Henga.

Hata hivyo, Anna Henga ameshangazwa na kitendo cha jeshi la polisi kutokuzingatia misingi ya usawa kwa kuendelea kuwabughudhi wanasiasa wa upinzani na kuruhusu chama tawala kuendelea kufanya shughuli za kisiasa bila bughudha yoyote.

“Sisi kama watetezi wa haki za binadamu tunahakikisha kwamba haki za wananchi wote zinalindwa bila ubaguzi; kitendo cha jeshi la polisi kuzuia, kuingilia au hata kuwakamata wanasiasa wa upinzani na kuruhusu mikutano ya chama tawala kuendelea bila bughudha yoyote ni kinyume na misingi ya usawa. Kwa mfano Mbunge wa Tarime, John Heche (CHADEMA) amedai kuzuiwa kufanya mkutano jimboni kweke (Julai 14, 2019) wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kufanya mkutano jijini Dar es Salaam”. Amefafanua Anna Henga.

Anna Henga ametoa wito kwa wananchi kuungana kukemea vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati akilisihi jeshi la polisi kuzingatia sheria na kutekeleza majukumu yake kwa weledi. Henga amelisihi jeshi la polisi kumpa Mbunge Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanaweake CHADEMA dhamana kwani masuala anayotuhumiwa nayo yanadhaminika.